WEZI WAFUKUA KABURI NA KUIBA MAITI


KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, familia ya Said Abdallah inayoishi Buguruni jijini Dar es Salaam imelazimika kutokwa machozi upya baada ya maiti ya mtoto Sophia Said (1) aliyefariki dunia kwa ugonjwa wa malaria, kuibwa na watu wasiojulikana na kaburi lake kuachwa wazi, Uwazi limechimbua.
 
Tukio hilo la aina yake na lililoacha maswali mengi, lilitokea usiku wa Julai 20, 2013 kwenye Makaburi ya Buguruni Kwamkanda, Mtaa wa Mnyamani jijini Dar es Salaam. Marehemu alizikwa Juni 20, 2013.
 
Uwazi lilifika eneo la tukio na kukuta umati, ikiwemo familia ya Said ukitokwa machozi huku wakiliangalia kaburi hilo likiwa wazi.
 
Mbao na miti iliyotumika kwenye mazishi ya mtoto huyo vilikutwa pembeni ya kaburi.
 
Wakati watu wakiendelea kumwaga machozi huku wakiulizana nini maana ya tukio hilo, Said ambaye ndiye baba mzazi wa marehemu alifika na kushuhudia maajabu hayo ambapo naye alishindwa kujizua na kuanza kulia.
Baada ya hali kutulia kidogo, mwandishi wetu alihojiana na mfiwa huyo ambapo alikuwa na haya ya kusema:
 
“Nashindwa hata kuelezea vizuri kwani tangu nizaliwe sijawahi kuona kaburi limefukuliwa, maiti haipo na isijulikane ilikopelekwa.
 
“Nikiwa kazini muda si mrefu uliopita nilipigiwa simu na shemeji yangu Said Masoud ambaye anaishi maeneo haya, akaniambia kaburi lipo tupu na haoni maiti ndani yake.
 
“Akasema mbaya zaidi, mbao na miti iliyotumika siku ya mazishi viko pembeni kuashiria kwamba waliofanya kitendo hiki ni watu waliokusudia.
 
“Niliishiwa nguvu, baadaye nilijikaza na kuja hapa. Ndiyo nimefika kama hivi na kukuta watu wengi nao wanashangaa.
“Nilipochungulia kaburi niliona ni kweli lilibaki tupu. Marehemu alikuwa ni mtoto wangu wa kwanza, niliwazaa mapacha na kwa sasa amebaki mwenzake aitwaye Salah.
 
‘Kinachonishangaza ni kwamba, marehemu tulimzika Juni 20 na kaburi limefukuliwa Julai 20, ina maana ni mwezi mmoja umepita.
 
“Sijajua kwa nini imetokea hivi! Mpaka sasa hakuna mtu ninayemshuku kuhusika na tukio hili, inawezekana ni mambo ya kishirikina, nakwenda kutoa taarifa polisi na kisha tutarudishia mchanga kaburini.
 
“Kusema ule ukweli inauma sana jamani! Mwanangu yuko wapi? Hata kama ni marehemu lakini nijue alipo.”
Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mnyamani, Jabir Sanze ambaye alikuwa katika eneo la tukio, alipoulizwa na mwandishi kuhusu kitendo  hicho, alisema:
 
“Hili ni tukio la ajabu, polisi wanahaha kutafuta maiti na wanafanya uchunguzi wa kina kwani tukio hili linaonekana halikufanywa na mtu mmoja.”
 
 CHANZO:SWAHILI TZ


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo