Waombolezaji nane ambao sita kati yao ni wa familia moja waliokuwa
wakitoka kuzika katika kitongoji cha Mlembule kilichopo kata ya Tongwe
wilayani Muheza wamejeruhiwa vibaya baada ya gari aina ya Toyota
lililokuwa limebeba sanduku la marehemu kupinduka.
Ajali hiyo imetokea katika kijiji cha Kwasemgaya kilichopo kata ya
Misongeni wilayani Muheza baada ya dereva wake kumpita dereva aliyekuwa
na gari dogo la abiria aina ya Hiace katika kona kali hatua ambayo
ilishindikana baada ya kuona kuna gari kubwa linakuja mbele yake ndipo
alipoamua kwenda pembeni mwa barabara na kusababisha gari kupinduka.
Kwa mujibu wa daktari wa zamu aliyepokea majeruhi wa ajali hiyo Dr,
Viviani Waluye amesema amepokea majeruhi nane lakini kati yao wawili
wamejeruhiwa vibaya ambao wametambulika kwa majina ya Joseph Frank
aleyejeruhiwa vibaya sehemu za mbavuni baada ya kuminywa na bomba la
bodi ya gari na Mohamed Mbaruk ambaye amevunjika miguu yake yote ukiwemo
wa kulia mara mbili ambao baada ya kufika hospitali teule wilayani
Muheza wamehamishiwa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Tanga Bombo.
Hata hivyo baadhi ya ndugu na wazazi wa majeruhi waliokuwepo katika
hospitali teule ya wilaya ya Muheza wamelamikia kuchelewa kwa utoaji
huduma ambapo mtaalam wa huduma ya picha aina ya X-ray alichukua zaidi
ya saa moja kufika hospitali hapo.
NA ITV