MTAALAMU ALIYETEULIWA KUUWA MBWA WANAOZAGAA WILAYANI BUKOMBE MR.MAGAI
MKAMA AKIENDELEA KUTOA DOZI KWA MMBWA WANAOZAGAA MJINI USHIROMBO.
GEITA
Zoezi la kuuwa mbwa
wanaozagaa ovyo ambao wanadhaniwa kuwa
na kichaa cha mbwa wilayani Bukombe mkoani Geita,huwenda likachelewa kukamilika
kutokana na changamoto ya watoto kujaa katika maeneo yanayofanyika mauaji hayo.
Mratibu
wa zoezi hilo Dr.Sosthenes Nkombe amesema kuwa watoto wilayani humo wamekuwa ni
kikwazo cha ufanisi wa zoezi hilo kutokana na kujaa katika maeneo ya tukio hali
ambayo ni hatari kwa uhai wa watoto hao.
Nkombe amesema watoto
wamekuwa kikwazo kwa sababu wanasimama mbele ya mdomo wa bunduki ambayo
inatumika kuulia mbwa hao hali inayowalazimu kuwafukuza kwanza kitendo
kinachowafanya mbwa hao kukimbia.
Akiendelea kufafanua Nkombe
amesema kuwa changamoto nyingine ni wananchi kutoelewa maana ya kichaa cha mbwa
na madhara yake pamoja na kufuga mbwa bila kuwapa matibabu ikiwemo chanjo.
Katika hatua nyingine Nkombe
amewashukuru wananchi kwa ushirikiano wanaoutoa ikiwa ni pamoja na kutoa
taarifa za mahali walipo mbwa na kuwataka wazazi na walimu kuwakataza watoto
kusimama katika maeneo ambayo zoezi hilo linaendelea.
Kwa upande wao baadhi ya
wananchi wa wilaya ya Bukombe wameishukuru halmashauri kwa kutekeleza zoezi
hilo na kwamba mbwa hao wamekuwa tishio sana hususan kwa watoto wadogo.
Zoezi la kuuwa mmbwa wanaozagaa
linatarajia kuendelea katika maeneo ya Lunzewe,Masumbwe na Lulembela ambapo kwa
mji wa ushirombo mpaka sasa zaidi ya mbwa 214 wameuwawa.