Umati wa watoto wa kata ya Ipelele waliofurika kwenye maadhimisho ya siku ya mtoto wa afrika
Mgeni rasmi ambaye ni mkuu wa wilaya ya Makete Josephine Matiro akihutubia wananchi waliofika kumsikiliza
======
Wazazi na walezi wanaojihusisha kimapenzi na watoto
wametakiwa kuacha vitendo hivyo mara moja na badala yake watumie muda huo
wanaoutumia kuwarubuni kuwafundisha watoto hao stadi za maisha ikiwemo namna ya
kujikinga na maambukizi ya virusi vya UKIMWI pamoja na kuzingatia masomo yao
shuleni
Sanjari na hayo kina mama wengi ambao pia wanafumbia macho
vitendo vya unyanyasaji na ukatili wanavyofanyiwa watoto kuacha mara moja kwa
kuwa mkono wa sheria hautawaacha pindi watakapobainika
Kauli hiyo imetolewa na mgeni rasmi ambaye pia ni mkuu wa
wilaya ya Makete Mh. Josephine Matiro katika hotuba yake aliyoitoa kwenye maadhimisho
ya siku ya mtoto wa afrika ambayo kiwilaya yameadhimishwa katika kata ya
Ipelele tarafa ya Magoma wilayani hapo
Mbali na hayo pia mh Matiro amekemea tabia inayoendekezwa na
baadhi ya wazazi na walezi hivi sasa ya kwenda na watoto sehemu za starehe hasa
vilabuni kwa kuwa tabia hiyo inawajengea watoto hao mazingira na tabia mbaya
hapo baadaye huku akiagiza viongozi na mamlaka husika kuchukua hatua dhidi ya
wazazi na walezi wanaofanya hivyo
“Kwa kweli hii ni aibu kubwa hivi vitu kama hivi ni mpaka
tukemewe kwani hamuono kama hamtendi haki kwa watoto? Sote tunajua wazazi
wakiwa vilabuni tena wakiwa wamelewa mambo wanayofanya kwa kweli hayajengi na
wale watoto wanashuhudia, baadaye wakikua wanaanza kufanya hivyo hivyo, hivi
tunajenga taifa gani?”amesema Matiro
Amesema hivi sasa wazazi na walezi wanatakiwa kuwa karibu na
watoto wao kwa kuwa watoto wanahitaji ukaribu kutoka kwao pamoja na kuwa na
moyo wa kusaidia watoto yatima na si kuyaachia mashirika pekee kwa kuwa muda
wowote pasipo taarifa suala ya uyatima linaweza kuikumba familia yako
Awali mtoto Alpani Abdani akisoma risala kwa niaba ya watoto
wa wilaya ya Makete walimwaomba mkuu wa wilaya kukemea vitendo vinavyofanywa na
baadhi ya wazazi na walezi kwa kkwenda na watoto vilabuni ama baa pamoja na
wale wanaojihusiha kimapenzi na watoto kwani vitendo hivyo ni hatari ikiwemo
watoto kupata maambukizi ya virusi vya Ukimwi
Katika maadhimisho hayo watoto wapatao 60 wanaoishi katika
mazingira hatarishi ambao wanatoka kwenye vijiji vya kata ya Ipelele walikabidhiwa
zawadi za madaftari na kalamu
Katika wilaya ya Makete jumla ya watoto yatima 42,628 ambapo kati yao 6,745 wanaishi katika mazingira hatarishi