Baada ya kuondoka katika mkutano wa viongozi wa kundi la mataifa nane
yaliyoendelea kiviwabda G8 mjini Belfast, Ireland ya Kaskazini, Obama
alitua kwa ndege yake ya Air Force One katika uwanja wa ndege wa Tagel
mjini Berlin majira ya saa mbili jioni, akisindikizwa na mkewe Michell
na mabinti zao wawili.
Usalama wa mji huo mkuu wa Ujerumani umeimarishwa
zaidi wakati wa ziara hii ambapo askari polisi 8,000 wamepelekwa
kuhakikisha hakuna jambo lolote baya linalotokea.
Obama atafanya mazungumzo leo na Kansela Angela Merkel, kabla ya kutoa
hotuba kwa hadhira ya waalikwa tu katika uwanja wa Pariser uliyoko mbele
ya Geti la Brandenburg, ambao ni eneo maalumu katika historia ya
urafiki wa Ujerumani na Marekani. Pia atakutana na rais wa Ujerumani
Joachim Gauck, na mgombea wa kiti cha ukansela kwa tiketi ya chama kikuu
cha upinzani, SPD Peer Steinbrück.
Maafisa mjini Berlin walisema Obama atahutubia hadhira ya wageni
waliochaguliwa 4,000, lakini gazeti moja limesema orodha hiyo iliongezwa
na kufikia majina 6,000 baada ya kupata idhidi kutoka mjini Washington.
Hotuba ya Obama inakuja karibu miaka 50 baada ya hotuba maarufu
iliyopewa jina la 'Ich bin ein Berliner" iliyotolewa na mtangulizi wake
rais John F. Kennedy.
Sakata la udukuzi wa mawasiliano
Wakati maafisa kutoka pande zote wamesisitiza kuhusu uhusiano wa
kihistoria uliopo baina ya Marekani na Ujerumani, ziara ya Obama imekuja
wakati ambapo Wajerumani wengi wanapaza sauti za ukosoaji, kuhusiana na
ufichuaji wa siri za udukuzi wa mawasiliano ya simu na mtandao
unaofanywa na serikali ya Marekani.
Kansela Merkel, ambae anakabiliwa na
uchaguzi mkuu mwezi Septemba, ameapa kutafuta majibu kutoka kwa Obama
kuhusiana na udukuzi huo.
Habari za udukuzi wa mawasiliano ziliwakasirisha raia wengi wa
Ujerumani, ambao bado wana kumbukumbu ya kuchunguzwa na serikali chini
ya tawala za madikteta wa kinazi na wakomunisti.
Wanaharati wameomba
ruhusa kwa polisi kufanya maandamano leo, ya kuanzia watu 50 hadi 500,
kupinga vitendo hivyo vya idara ya usalama wa taifa ya Marekani NSA.
Merkel alisema katika mahojiano siku ya Jumatatu, kwamba vidokezo vya
Marekani viliisaidia Ujerumani kuzuiwa njama za ugaidi, likiwemo jaribio
la kuripua maslahi ya Marekani nchini Ujerumani mwaka 2007. Lakini
alisema atamuuliza Obama ni kwa kiasi gani mawasiliano ya mtandaoni ya
Ujerumani yamekuwa yakidokolewa.
Kiongozi huyo mwenye ushawishi mkubwa zaidi barani Ulaya katika wakati
ambapo bara hili linakabiliana na mgogoro wa madeni, pia yuko makini
kujadili matarajio ya mapatano ya ushirikiano wa kibishara na uwekezaji
kati ya mataifa ya Ulaya na Marekani, TTIP.
Vita vya Syria na
Afghanistani navyo vinatarajiwa kuchukuwa nafasi kubwa katika mazungumzo
yao. Obama na Merkel watazungumza katika mkutano na waandishi wa habari
majira ya saa sita mchana.
Tukio kuu la ziara ya Obama
Lakini tukio kuu la ziara yake litakuwa hotuba katika lango lakihistoria
la Brandeburg, ambalo wakati mmoja lilikuwa sambamba na ubamba wa ukuta
wa Berlin, uliyotenganisha pande mbili za Ujerumani mashariki na
magharibi za mji huo mkuu.
Mwaka 1987, rais Ronald Reagan alimtaka
kiongozi wa Kisovieti kuvunja ukuta huo katika hotuba aliyoitoa akiwa
upande wa magharibi wa lango lango hilo.
Merkel alimkataza Obama, wakati huo akiwa Seneta wa jimbo la Illinois,
kuzungumza mbele ya lango hilo mwaka 2008. Na badala yake alihutubia
wafuasi wake karibu 200,000 katika bustani ya karibu ya Tiergarten.
Mwaka huu atasimama katika uwanja wa Pariser, katika upande wa mashariki
wa lango hilo, na kutoa wito kwa Ujerumani, Ulaya, na Marekani, kutumia
historia yao inayofanana ya ushirikiano imara, kutatua changamoto za
karne ya 21.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/dpae,afpe, DW
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman