MKUU wa Wilaya
ya Bagamoyo, mkoani Pwani, Ahmed Kipozi ameitaka jamii kuhakikisha
inashughulikia suala la kuwalinda watoto ikiwemo suala la ukatili, mila
kandamizi na utumikishaji usiofaa.
Kipozi alisema hayo jana
jumapili alipokuwa mgeni rasmi wakati wa maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika
inayofanyika kila mwaka Juni 16.
Akihutubia wananchi,
pamoja na watoto wakiwemo kutoka shule mbalimbali za msingi za
Wilaya hiyo, alisema kuwa Jamii inajukumu kubwa ya kuakikisha suala la ulinzi
linatekelezwa kwa pamoja hasa katika kumlinda mtoto.
“Kumlinda mtoto na mila
kandamizi ni jukumu letu, nasi hatuna budi kuwahakikishia hilo pamoja na
kutokomeza vitendo viovu dhidi yao” alisema Kipozi. Pia alieleza kuwa wajibu
wa kila mmoja ni kuhakikisha watoto wanakuwa kwenye ustawi bora katika makuzi
yao ilikuweza kutimiza malengo yao mbalimbali pindi watakapofika ukubwani.
kwa upande wake, mmoja wa
wazee wa Mila wilayani hapa, Rashid Yusufu Sekamba alisema kuwa
watahakikisha wanaachana na mila potofu ilikuendana na wakati ikiwemo suala la
unyago kwa watoto wa kike.
“Tumesikia sana kilio
chenu watoto, juu ya mila potofu hasa unyago, tutachukua hatua na hata
kulimaliza..Mimi sijui huko kwenye unyago wanafundisha mambo gani, ila kama
namcheza mtoto bado yupo shule, ni lazima aende akajaribu kwa vitendo
hili si sawa. Sasa unadhani hili ni sawa?, si sawa wazee wa mila tutaangalia
namna ya kuachana nalo” alisema Sekamba.
Katika maadhimisho hayo,
ambayo yaliratibiwa na Halimashahuri ya Bagamoyo kwa kushirikiana na wadau
mbalimbali, Mkuu wa Wilaya alikabidhi baiskeli moja ya walemavu (wheelchair),
pamoja na kupokea kandambili pea 300, vyote vilivyoolewa na Asasi ya TRACED. Sherehe za mwaka huu za
mtoto wa afrika yenye kauli mbiu, “Kuondoa mila potofu zenye kuleta madhara kwa
watoto: Ni jukumu letu sote”.
Kwa upande wao wajumbe
mbalimbali waliotoka asasi za kiraia ndani ya wilaya hiyo walipongeza shughuli
hiyo. Asasi hizo ni pamoja na
HELP Foundation, Mkombozi, TRACED, HakiMtoto Foundation, BAKA, Compassion na
wengine wengi.
Kwa upande wa watoto hao
waliweza kuelezea na kutoa kero mbalimbali dhidi ya vitendo wanavyofanyiwa na
jamii ikiwemo unyanyasaji na ukatili huku wakiomba kutambua watoto ni taifa la
leo hivyo linahitaji kulindwa.
Kupitia risala yao,
watoto hao mbele ya DC, walitaka kuthaminiwa,ulinzi, kusikilizwa na yale yote
ya msingi.
