MADIWANI wa Halmashauri
ya Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya wamekubali kupendekeza azimio la kuugawa
Mkoa wa Mbeya kama walivyoagizwa na Rais Jakaya Kikwete na kukubaliana kuwa Mkoa
mpya uitwe Rungwe na makao makuu ya Mkoa yawe Tukuyu.
Pendekezo hilo limetolewa jana katika kikao maalum cha
Baraza hilo kilichojadili kuugawa mkoa huo ambapo pendekeza hilo liliwasilishwa
na Mkurugenzi wa Halmashauri wa Wilaya ya Rungwe Noel Mahyenga kwa madiwani na
kusema kuwa kutokana na agizo la Rais kutaka kuugawa Mkoa wa Mbeya na wao
kutaka Mkoa mpya uitwe Rungwe.
Alisema kuwa kikao cha kamati ya fedha uongozi na mipango kilijadili suala hilo kupitia mapendekezo ya
wataalam ambayo yalikidhi vigezo vyote na kuwa kutokana na historia ya Wilaya
hiyo ilivyokuwa na Jiografia nzuri katika shughuli za kiuchumi ipo haja ya
kupitisha azimio la Wilaya hiyo kuwa Mkoa.
Aliongeza kuwa Wilaya ya Rungwe inavivutio vingi vya utalii
vipatavyo 19 miongoni mwa maeneo hayo ni kambi ya uvuvi ya Isongole,daraja la
mungu ziwa ngozi na mlima Rungwe na pia kuna uwanja wa ndege (airstrip) ambao
unaweza kutumiwa katika shughuli za kiutawala,kibiashara na kitalii
zitakazopanuka na kuongeza pato mara dufu.
Kutokana na hali hiyo madiwani walipitisha azimio hilo la
Rungwe kuwa Mkoa kwa asilimia 90 na kuzitaja wilaya zitakazounda Mkoa huo kuwa
ni Ileje,Kyela,Rungwe na Busokelo ambayo itapandishwa hadhi kuwa Wilaya kamili
badala ya Halmashauri kama ilivyo sasa,
Baada ya kumalizika
kwa baraza hilo la madiwani,Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Chrispin Meela aliitisha
kikao cha Baraza la ushauri (DCC)akiwashirikisha maafisa watendaji wa kata
wenyeviti wa vyama vya siasa wakuu wa idara na wananchi wa kawaida kwa lengo la
kujadili suala la Mkoa Mpya.
Katika kikao hicho wananchi na viongozi wote wa Serikali na
Taasisi binafsi waliunga mkono suala
hilo na kutoa azimio la kutaka Rungwe ipandishwe hadhi ya kuwa Mkoa kama walivyopendekeza madiwani katika baraza
lao.
Waliongeza kuwa Wilaya za Mbarali,Mbozi,Momba,Chunya na
Mbeya zibaki kuwa Wilaya huku Mkoa uwe Rungwe na Wilaya zake ziwa Kyela,Ileje
Rungwe na Busokelo na makao makuu ya Mkoa yawe Tukuyu ka walivyopendekaza
Madiwani katika kikao chao.
Na Ibrahim Yassin