Wizara ya Maliasili na Utalii
inashiriki kwenye maonyesho ya Biashara ya Kimataifa ya SABASABA mwaka
huu yanayofanyika katika viwanja vya Mwalimu Julius.K.Nyerere, Saba
Saba, Barabara ya Kilwa.
Wizara
inawakaribisha wananchi wote wenye kiu ya kuona na kuelimika kuhusu
shughuli za Utalii, Ufugaji Nyuki, Uhifadhi wa Misitu, Malikale na
Wanyamapori. Ikumbukwe
kuwa Banda la Maonesho la Wizara miaka yote huwavutia watu wengi
wanaoshiriki katika maonesho ya Viwanda na Biashara hali
ilinayowapelekea watu wengi kushindwa kuingia ndani kuona wanyama
kutokana na umati mkubwa wa watu wanaofurika hasa inapokaribia kilele
cha maonyesho.
Wizara inapenda
kuwajulisha wananchi wanaopenda kujielimisha na kuona shughuli
mbalimbali za Wizara kutembelea banda kuanzia Mwanza wa maonyesho badala
ya kusubiri siku ya ufunguzi Julai 4 mwaka huu ambapo watu hufulika
kiasi cha wengi kushindwa kutii kiu zao wafikapo bandani.
Aidha, katika kuimalisha
utalii wa ndani Wizara imeandaa safari za kutembelea Hifadhi ya Taifa
ya Mikumi kwa gharama nafuu ambapo mtu mzima atalazimika kulipa Tsh
15,000/- na mtoto Tsh 5,000/- ikiwa ni gharama za usafiri kutoka
viwanya vya Sabasaba hadi hifadhini na kurejea siku hiyo hiyo jijini Dar
es Salaam.
Sambamba na hilo Wizara
imetoa ufadhili kwa vikundi vya asali kutoka wilaya zote nchini zenye
wafugaji nyuki ili kutoa fursa kwa wananchi kujifunza juu ya umuhimu wa
asali mwilini. Vikundi hivi vinapatikana katika Banda la Asali
litakalokuwa na maonyesho ya asali na bidhaa zitokanazo na nyuki.
Wizara haijawasahau
wananchi wanaopenda kutunza mazingira kwa kupanda miti ya matunda,
kivuli pamoja na mapambo kwa kuhakikisha inawaletea miche mbalimbali
bandani inayouzwa kwa bei nafuu.
Ndani ya banda wananchi
watapata fursa ya kukutana na wadau mbalimbali wa sekta ya utalii,
wanyamapori na mambo ya kale watakaokuwa wanatoa elimu juu ya jambo
lolote litakalokuwa linamtatiza mwananchi aliyefika bandani hapo.
Miongoni mwa wanyamapori hai watakaokuwepo ni kama vile Chui, Nyoka, Ndege wa aina mbalimbali pamoja na mfalme wa pori SIMBA.