WAKRISTO WATAKIWA KUJIEPUSHA NA BIASHARA HARAMU

Mara baada ya ibada ya kubariki moto, mshumaa wa Pasaka ukiwa umewashwa na kuelekea kanisani


WAKRISTO nchini wametakiwa kujiepusha na biashara zisizo za halali zinazowaumiza wengine kwa kuhatarisha amani, upendo na mshikamano vilivyo tunu kuu ya nchi hii.

Mwandishi wa mtandao huu Gustav Chahe anaripoti kuwa haya yamezungumzwa na Mhashamu askofu Tarcisius Ngalalekumtwa wa Jimbo Katoliki la Iringa alipokuwa akihubiri katika Misa ya Mkesha wa Pasaka iliyofanyika katika Kanisa la Bikira Maria Consolata Parokia ya Mshindo jimboni humo.

Ngalalekumtwa alisema wapo baadhi ya watu wanaofanya biashara haramu huku wakijua kuwa wanawaumiza wengine bila kujali.

Askofu Ngalalekumtwa ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania alisema binadamu ananuka kwa kufanya matendo ya aibu na kuwafanya wengine kuwa kama watumwa.

“Tunanuka, tumeoza na uchafu uliogandamana kwa miaka mingi unaotokana na matendo machafu ya kuwafanya wengine kama watumwa” alisema.

Alisema Mungu anawataka kuwa ni watu wenye kulinda utu wao na uumbaji wake kwa kufanya yale ambayo kila mmoja anayapokea na kuridhika katika maisha yake.

“Sisi ni watoto wa aliye chanzo cha wema na aliye na utakatifu. Hivyo, tusiwe wafu na “tulemwakuva twivafu”, tutumie akili zetu kutenda yale yaliyo na maana kwa manufaa ya upendo na haki kwa kila mmoja” alisema.

Amewataka kutokuwa na hofu ya kuilinda imani yao kwa kuwa Mungu pekee ndiye mwenye mwokozi wa kweli na kuwataka wapuuze yale yasiyoijenga jami iwe kwa maneno, vitendo au kwa kulazimishwa.

“Simameni imara katika kuikiri imani yenu ili iweze kuratimu mawazo, matendo, maneno hata mahusiano sisi kwa sisi na mahusiano yetu na Kristo ikiwa ni pamoja na mahusiano ya kisiasa hata kidini” alisema.

Alisama kwa Mkristo heshima, utii na upendo ni zawadi ya pekee waliyo jaliwa na Mungu kwa ajili ya kuziunganisha jamii katika kitu kimoja zinazoelewana bil kudharauliana na kufarakana katika maisha.

“Kuweni watu wema, wapenda haki, heshima, huruma, upole, wema na unyenyekevu usio na unafiki. Msiache upepo wa dunia hii izimishe mwanga, upendo wenu, huruma yenu, utii wenu na upole wenu. Jivisheni vazi la haki lenye kutenda mema” alisema.

Hata hivyo alisema mtu asiyekuwa na imani ni sawa na kuwa uchi na ndicho chanzo cha kufanya mambo machafu na ya ajabu yasiyompendeza Mungu na wanadamu wenzake.

“Kama huna imani ni sawa na kuwa uchi tena uko ovyo. Kristo anayamulikisha maisha yetu kwa nuru ya utukufu wake ili tuachane na giza. Hakuna mwokozi mwingine wa wandamu isipokuwa Yesu wa Nazareti” amesema.

Katika Misa hiyo vijana 15 walipewa Sakramenti ya ubatizo na Kipaimara.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo