BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara limeagiza watumishi wa halmashauri hiyo kufuatilia mchakato wa ujenzi wa eneo huru la biashara (EPZ) Mirerani kwani ni ahadi ya Rais Jakaya Kikwete.
Aidha madiwani hao walisema kuwa
wakati wa kampeni ya uchaguzi wa mwaka 2010 Rais Jakaya Kikwete na
Makamu wa Rais Dk Gharib Bilal,kwa nyakati tofauti wilayani humo walitoa
ahadi ya ujenzi wa EPZ kwenye mji mdogo wa Mirerani.
Waliongeza kuwa eneo
linalopaswa kujengwa EPZ lilishatengwa kwa muda mrefu,hivyo mchakato wa
ujenzi wake ulitakiwa kuanza tangu hapo awali,lakini hadi hivi sasa
hakuna hatua zozote zilizofanyika ikiwemo upimaji na michoro ya ujenzi.
Naye Diwani wa kata ya Mirerani Justin Nyari aliongeza kuwa amefuatilia
suala hilo muda mrefu kwenye Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya
Makazi ili kubaini hatma ya mradi huo na anajibiwa kuwa wanasubiri
taarifa ya halmashauri.
Alisema
kuwa Halmashauri inatakiwa ifuatilie hili suala kwani nimekuwa nikipiga
simu wanadai kuwa wanatusubiri majibu ya halmashauri juu ya matumizi
bora ya aridhi,wenzetu wa Kia wapo kwenye mchakato wa upimaji.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo,Peter Tendee alisistiza kuwa hivi
karibuni kwenye kikao cha ushauri cha mkoa huo (RCC) alizungumzia
kuhusiana na EPZ ya Mirerani na akaelezwa kuwa viongozi hao
watalishughulikia.
“Kwa kweli suala
hili tulishalifikisha mkoani wakatujibu kuwa ngazi za juu
wanashughulikia,tunapaswa kusubiri utekelezaji wake kwani mradi huu
umechukua muda mrefu na hadi sasa ujenzi wake haujaanza,” alisema
Tendee.
Kwa
upande wake Diwani wa kata ya Naberera,Sumleck Ole Sendeka alisema
utekelezaji wa ujenzi wa EPZ ya Mirerani,ulitakiwa kuanza ili
kuinufaisha wilaya hiyo kupitia mradi huo lakini hadi hivi sasa mchakato
wake umechukua muda mrefu kutekelezwa.
Alibainisha
kuwa EPZ imekuwa hadithi ndefu kwani madiwani wa kipindi cha mwaka
2005/2010 walikwenda Dar es salaam kuona pamoja na kujifunza kupitia EPZ
ya Ubungo ili iwe somo kwao sasa mbona ahadi ya Rais haitimizwi.