Imebainishwa kuwa kwa muda wa miaka minne mfululizo wilaya
ya Simanjiro mkoani Manyara ilikuwa inashika nafasi ya kwanza kwa
kiwango cha ufaulu mkoani humo imejipanga kurudia nafasi hiyo baada ya
mwaka jana kushika nafasi ya tano.
Hayo yamebainishwa na mwenyekiti
wa halmashauri ya wilaya hiyo Peter Tendee wakati akifunga kikao cha
kawaida cha baraza la madiwani hao kilichofanyika mji mdogo wa Orkesumet
wilaya simanjiro mkoani Manyara.
Alibainisha kuwa tangu
mwaka 2008 wilaya hiyo ilikuwa inakamata nafasi ya kwanza mkoani humo
kwa kufaulisha vizuri wanafunzi wanaomaliza darasa la saba na kuingia
kidato cha kwanza lakini mwaka jana walishika nafasi ya tano.
Aliongeza kuwa jitihada
na juhudi za makusudi zinahitajika kufanyika kwa ushirikiano wa
viongozi,walimu,wazazi,walezi na wanafunzi wenyewe ili waweze kurudia
tena kwenye nafasi yao ya kwanza kama miaka iliyopita.
Alisema kuwa zipo changamoto mbalimbali zinazowakabili kwenye wilaya hiyo ikiwemo
wanafunzi kupata ujauzito,utoro na umbali wa shule na makazi hivyo
wanapaswa wapambane ili kuweza kuzimaliza changamoto hizo.
Kwa upande wake mmoja wa mjumbe wa Kamati ya Elimu Afya na Maji Clempu Ole Kinoka alisisitiza kuwa kaimu
Mkurugenzi wa halmashauri Patrice Saduka aandike barua kwa kamati ya
mitihani ya mkoa juu ya wanafunzi waliodaiwa kufaulu na hawajui kusoma
na kuandika,wana uwezo huo baada ya kufanya mtihani.
Aliendela kusema kuwa orodha
ya wanafunzi wa darasa la saba ambao hawakufanya mtihani wa Taifa mwaka
jana,ichambuliwe na maofisa watendaji wa vijiji,kata na waratibu ili
wazazi wanaostahili kupelekwa Mahakamani wajulikane.
Alisema
kuwa orodha ya wazazi wanaotakiwa kupelekwa Mahakamani kutokana na
watoto wao kutofanya mtihani wa darasa la saba mwaka 2012 ipelekwe
kwenye Kamati ya Fedha Uongozi na mipango mwezi huu wa Februari.
Aidha matokeo ya darasa la saba ya mwaka 2012 yalisababisha
madiwani kumkataa aliyekuwa Ofisa elimu wa wilaya hiyo,Jackson Mbise
aliyewashusha vyeo walimu wakuu 15 wa shule zilizofaulisha wanafunzi
wasiojua kusoma na kuandika.
Pia mwaka
2012/2013 halmashauri ya mji wa Babati ilishika nafasi ya kwanza mkoani
humo kwa kiwango cha ufaulu na kufuatiwa na halmashauri za wilaya ya
Mbulu,Babati vijijini,Hanang’,Simanjiro na Kiteto.