Na Mwandishi Wetu, Mara
WAKATI watu mbalimbali wakisherehekea siku ya
wapenda nao (Valentine Day), Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Mara, Japhet
Lusingu anasema wanawake watatu wameuwawa baada ya kupigwa na waume zao
katika matukio tofauti. Kuuwawa kwa wanawake hao kunatimiza idadi sita
ya matukio ya vifo mkoani Mara, huku wengine tisa wakijeruhiwa.
Akizungumza na wanahabari jana mjini hapa, Lusingu alisema matukio hayo yametokea kati ya mwezi Januari na Februari mwaka 2013.
Akifafanua matukio hayo Lusingu alisema tukio la kwanza lilitokea
Februari 10, 2013 majira ya saa 3:00 asubuhi Kijiji cha Tonyo Kata ya
Busumwa, Wilaya ya Butiama,ambapo mwanamke aliyetambulika kwa jina la
Happyness Lucas (25), alipigwa na mumewake, Rugera John (27) hadi
kusababisha kifo chake.
Alisema chanzo cha ugomvi huo ni ndala (kandambili) ambazo mume wa
marehemu alikuwa amemnunulia mke mdogo. Happyness Lucas ambaye kwa sasa
ni marehemu alipelekwa katika Hospitali ya Butiama kwa matibabu baada ya
kipigo lakini Februari 11 alifariki dunia.
Kaimu Kamanda Lusingu alisema tukio jingine lilitokea Januari 28,
2013 wilayani Bunda, Mtaa wa Chiringe, ambapo Rhobi Lucas (24) fundi
cherehani akiwa nyumbani kwake alifika mumewe aliyetajwa kwa jina la
Masumbuko Khamis akiwa na hawara yake, Joyce Manumbu.
Inadaiwa kuwa baada ya kufika mume wake alianzisha ugomvi na kuanza
kumshambulia mke wake kwa mateke huku akishirikiana na hawara yake.
Baada ya ugomvi Rhobi Lucas aliamua kuondoka nyumbani kwake na kwenda
kwa wazazi wake kutoa taarifa za kushambuliwa siku hiyo hiyo.
Aidha Kamanda Lusingu aliongeza kuwa Januari 30, 2013 mumewe pia
(Masumbuko) alifika Polisi kutoa taarifa kuwa ameshambuliwa na mkewe
baada ya taarifa hiyo mkewe alikamatwa na Januari 31 alifikishwa
mahakamani.
Aliongeza kuwa Februari 9, 2013 mwanamke huyo alizidiwa na hali yake
kuwa mbaya kutokana na kipigo alichokipata toka kwa mumewe kwa
kushirikiana na hawara yake na kupelekwa Hospitali ya DDH Bunda kwa
matibabu, lakini Februari 11 alifariki dunia. Polisi wanamshikilia
mwanaume huyo kuhusiana na kifo hicho.
Tukio lingine lilitokea Februari 9, 2013 saa 9:00 jioni Kijiji cha
Nambubi Tarafa ya Nansimo wilayani Bunda, ambapo mwanamke aliyejulikana
kwa jina la Edith Christopher (36) alishambuliwa na mumewe Elephasi
Maitabo (58) na mpini wa mundu kwa kupigwa tumboni, mgongoni na kifuani
na kufariki dunia akiwa njiani kupelekwa hospitali.
Chanzo cha mauaji hakijajulikana lakini mtuhumiwa huyo amekamatwa na
polisi na atafikishwa mahakamani mara taratibu zitakapokamilika.
Tukio la tatu, lilitokea Februari 11, mwaka huu saa 1:30 asubuhi
maeneo ya Kijiji cha Mkirira wilaya ya Butiama, ambapo mwanamke
aliyejulikana kwa jina la Ziada Sasita (35) mkazi wa Kijiji cha Kabegi
aliuawa kwa kunyongwa shingo kwa kutumia nguo yake (mtandio) hadi kufa
na watu wasiojulikana.
Marehemu alikuwa anatokea kwa mjomba yake maeneo ya Mkirira ambako
alikwenda kumsalimu na mauti yalimkuta akirejea Kabegi ambako alikuwa
ameolewa. Mwili wa marehemu ulikutwa na mtandio shingoni na ulimi wake
ukiwa umetoka nje. Hadi sasa hakuna anayeshikiliwa kutokana na tukio
hilo.
Tukio lingine ni ajali ya mwendesha pikipiki kugonga kizuizi cha
standi mpya ya mabasi wilayani Bunda ambapo mtu mmoja aliyejulikana kwa
jina moja la Maka umri kati ya miaka 18 hadi 20 akiwa na pikipiki isio
na namba za usajili, chanzo cha ajali ni mwendo kasi.
Tukio la lingine lilitokea Februari 10 mwaka huu saa 4:15 usiku
Kijiji cha Msinganyi, Bunda ambapo gari aina ya Fuso namba T 677 BLQ
mali ya Masunga Bugubugu mkazi wa Bariadi iliyokuwa ikiendeshwa na
dereva ambaye hajafahamika jina lake hadi sasa.
Gari hiyo ilikuwa inatokea Kijiji cha Kenyamonta Wilaya ya Serengeti
mnadani iliacha njia na kupinduka na kusababisha kifo cha Magoti umri
kati ya miaka 35 hadi 40, mfanyabiashara wa wilaya ya Butiama na wengine
tisa kujeruhiwa.
Kamanda Lusingu aliwataja waliojeruhiwa ni Grace Masoka (40), Prisca
Gwasi (42), Chausiku Mashara (35), Neema Hamis (25), Chacha Mwita (34),
jamwela Wambura (30), Hassan Bunge (34), Juma Komba (22) na mary Rashid
(37) wote wakazi wa Wilayani Bunda.
Kamanda Lusingu ametoa wito kwa wanaume wa Mkoa wa Mara kuacha
kutumia nguvu na mabavu kwa wake zao kwani matukio ya aina hiyo
yamezidi.
Chanzo Binda News
Chanzo Binda News
