VODACOM YATWAA TUZO YA KUWASILISHA MICHANGO NSSF

 Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar,Balozi Self Ali Idd,akimkabidhi Mkuu wa Vodacom Tanzania,Kanda ya kaskazini,Bw.Philemon Chacha tuzo ya mchangiaji bora wa michango ya wanachama katika mfuko wa pensheni wa NSSF kwa makampuni ya mawasiliano nchini.Vodacom imeshinda tuzo hiyo na kukabidhiwa wakati wa hafla ya ufunguzi wa mkutano wa tatu wa wadau wa mfuko wa NSSF uliofanyika Mount Meru Hoteli jijini Arusha. 
Mkuu wa Vodacom Tanzania,Kanda ya kaskazini,Bw.Philemon Chacha akionesha tuzo ya mchangiaji bora wa michango ya wanachama katika mfuko wa pensheni wa NSSF kwa makampuni ya mawasiliano nchini.Tuzo hiyo ilitolewa jana katika mkutano wa tatu wa wadau wa NSSF na Makamu wa pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Balozi Self Ali Idd.
 Mkuu wa Vodacom Tanzania,Kanda ya kaskazini Bw.Philemon Chacha akiwa na  Meneja wa uendelezaji biashara wa kanda hiyo Bw. Philemon Matoi na tuzo waliyokabidhiwa kwa niaba ya kampuni ya vodacom Tanzania baada ya kuongoza kwa makampuni yote ya mawasiliano katika uchangiaji wafanyakazi wake katika mfuko wa pensheni ya NSSF, tuzo hiyo ilitolewa na makamu wa pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Balozi Self ali Idd katika mkutano wa tatu wa wadau wa mfuko huo, Mount Meru hoteli jijini Arusha.
picha ya pamoja ya washindi wa tuzo za wachangiaji bora wa mfuko wa hifadhi ya jamii ya NSSF pamoja na Makamu wa  pili wa Rais wa Serikali ya mapinduzi Zanzibar Balozi, Self Alli Idd pamoja na viongozi wengeni wa mfuko wa NSSF. 
--
Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania imeshinda tuzo ya kampuni bora ya mawasiliano nchini inayowasilisha vema michango ya wafanyakazi wake katika Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii - NSSF.

Tuzo hiyo imekabidhiwa kwa Vodacom jana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd katika hafla ya ufunguzi wa mkutano wa tatu wa wadau wa NSSF unaofanyika jijini Arusha

Akizungumzia tuzo hiyo Ofisa Mkuu wa Rasilimali Watu wa Vodacom Dk. Fred Mwita amesema tuzo hiyo ni matokeo ya Vodacom kujali masilahi ya wafanyakazi wake ikiwemo suala la mafao.

"Pamoja na kwamba tunatekeleza wajibu huo kwa mujibu wa sheria lakini ushindi huu ni kielelezo cha udhati na umakini wetu katika kutimiza kila wajibu unaotuhusu kwa wafanyakazi wetu."Amesema Dk Mwita

Amesema Vodacom yenye wafanyakazi zaidi ya 500 imekuwa ikiweka kipaumbele cha upekee katika masilahi na masuala yanayowahusu wafanyakazi kwa kile inachoamini kuwa mafanikio ya kampuni yapo mikononi mwa wafanyakazi hao katika kujibidiisha katika majukumu yao.

Ameutaja ushindi huo kuwa ni ufahari kwa Vodacom kwani inatambua kuwa umepitia mchakato uliokuwa na vigezo vigumu vya ushindani na kwamba inaijengea Vodacom heshima na taswira chanya miongoni mwa jamii ndani na nje ya nchi.

"Vodacom imekuwa mwajiri mzuri ikivutia vijana na wanataaluma mbalimbali na kwamba kwetu sisi tuzo hii itazidi kudhihirisha hilo na kuwafanya wafanyakazi wetu kufanya kazi kwa kujiamini bila hofu juu ya mafao yao."

Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi za Jamii (NSSF), Crescentius Magori, akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo alisema kampuni ya Vodacom,wafanyakazi wake asilimia 95 wamekuwa wakilipiwa vyema makato yao.

"kampuni hii tunaikabidhi tuzo hii kutokana na umahiri wake katika kuwasilisha vyema michango ya wafanyakazi wake pamoja na wafanyakazi wake wote kuendelea kuwa wanachama wa NSSF licha ya baadhi kuhamishwa vitengo"alisema Magori.

Tuzo hiyo, ilipokelewa na Mkuu wa Vodacom Kanda ya Kaskazini, Philemon Chacha kutoka kwa Balozi Idd ambaye pia alipongeza kampuni hiyo ya Vodacom kwa utendaji mzuri na kuwa wachangiaji wazuri wa NSSF.

Makamu huyo wa Rais wa Zanzibar pia alitoa wito kwa waajiri nchini, kuwasilisha katika mifuko ya jamii makato ya wafanyakazi wao kwa wakati kwani kutowasilisha ni kosa la jinai.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo