Mwenyekiti wa bodi ya maji bonde la Rufiji Bw. Bakari Mbonde (Kushoto) akiwa na mkurugenzi msaidizi wa idara ya rasilimali maji Bw. George Lugomela, katika warsha hiyo.
Na Oliver Motto
VIONGOZI wazembe, wasiozingatia
sheria za utunzaji wa vyanzo vya maji, wametajwa kuwa ni chachu ya kukauka kwa
maji katika mto Ruaha mkuu, na hivyo kukwamisha juhudi mbalimbali zinazofanywa
na serikali kwa zaidi ya mika 20.
Hayo yamezungumzwa na wadau wa
mazingira nchini katika warsha ya kujadili utatuzi endelevu wa changamoto za
usimamizi wa rasilimali za maji kwa maeneo yanayouzunguka mto Ruaha mkuu, kikao
kilichofanyika katika ofisi za Bonde la Rufiji mjini Iringa.
Akilalamikia hatua ya kukwama kwa
jitihada za kuunusuru mto Ruaha mkuu, Bw. Nicholaus Kalinga Mwenyekiti wa
UMURAME amesema viongozi wa aina hiyo ni
changamoto katika kuuokoa mto huo, na hivyo wananchi kukosa usimamizi katika
utunzaji wa vyanzo vya maji.
Bw. Idris Msuya ofisa maji bonde la
Rufiji amesema kilimo cha Vinyungu katika Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa na
kilimo cha Mpunga katika bonde la Usangu Wilayani Mbarali ni sababu zinazochangia
maji kupungua katika Mto Ruaha mkuu.
Bw. Zakaria Chonya ofisa kutoka
katika ofisi za bonde la Rufiji amesema uhifadhi wa rasilimali maji na suala zima
la kurudisha mtiririko wa maji katika
Mto mkuu Ruaha, zinahitajika jitihada
mbalimbali za wadau katika kukabiliana na uharibifu wa vyanzo vya maji.
Chonya amesema sekta binafsi na idadi
kubwa ya wanawake kutoshiriki katika vikao na mafunzo mbalimbali ya udhibiti wa
rasilimali maji, pia ni changamoto inayozikwamisha jitihada hizo.
Bw. Abel Mwasajone mdau wa
mazingira kutoka mkoani Mbeya, amesema mabadiliko ya tabia nchi yanachangia
uwepo wa changamoto ya upungufu wa maji katika mto huo.
MKurugenzi msaidizi wa idara ya
rasilimali maji Bw. George Lugomela amesema kuna mpango wa kujenga Bwawa katika
mto Lyandembela ili kuunusuru mto Ruaha mkuu, na kuwa shughuli za kiuchumi ni chanzo kikuu cha
kukauka kwa maji katika mto huo.
Aidha mwenyekiti wa bodi ya maji
bonde la Rufiji Bw. Bakari Mbonde amesema udhibiti na usimamizi hafifu wa
vyanzo vya maji unachangia uwepo wa changamoto rukuki katika mto Ruaha mkuu.
Hata hivyo wadau hao wa mazingira wamelitaka
shirika la Umeme Tanesco kub uni njia mbadala, tofauti na maji katika kufua
nishati ya Umeme, ikiwa pamoja na kujikita katika chanzo cha Gasi au Upepo, ili
kuepukana na mabadiliko ya tabia nchi
yanayochangia maji kupungua kwa kasi katika mito mbalimbali na mabwawa.