Kila
sifa njema anastahiki Mwenyezi Mungu Mtukufu Mlezi wa Viumbe. Sala na
salamu zimfikie Mtume wetu Mtukufu Muhammad (S.A.W), jamaa zake,
maswahaba zake waongofu na wote wanaowafuata kwa wema hadi Siku ya
Malipo.
Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar lililokaa Jumapili tarehe 23/2/2013 katika kikao cha kutathmini matukio ya kushambuliwa na kuuliwa viongozi wa Dini yakiwemo ya karibuni ya kupigwa risasi na kuuliwa Padri Mushi pamoja na kupigwa mapanga na kuuliwa Sheikh Ali Khamis Bin Ali Khatibu wa Mwakaje na kuendelea kutolewa kwa kauli za uchochezi dhidi ya Zanzibar linatamka ifuatavyo:
1.
Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar linalaani vikali na
kwa nguvu zote matukio ya kushambuliwa na kuuliwa viongozi wa Dini
likiwemo tukio la karibuni la kupigwa risasi na kuuwawa Padri Mushi
kulikofanywa na wahalifu wasioitakia mema Zanzibar.
2.
Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar linapenda kuweka wazi
kuwa uhai ni tunu kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu aliyotunukiwa
binaadamu hivyo hakuna mwenye mamlaka ya kuiondoa haki hiyo isipokuwa
yeye mweyewe Mwenyezi Mungu. Kutokana na ukweli huu ndio maana Sheria za
Kiislamu zimeweka wazi mtu mwenye kumuuwa mwenziwe naye auliwe kama
inavyoelezwa katika Kitabu kitufu cha Quran kama ifuatavyo:
“Na humo (katika Taurati) tuliwaandikia ya kwamba mtu (huuwawa kwa sababu ya kuuwa mtu) kwa mtu, ……….” (5:44)
“Na humo (katika Taurati) tuliwaandikia ya kwamba mtu (huuwawa kwa sababu ya kuuwa mtu) kwa mtu, ……….” (5:44)
Hivyo, vitendo vya kiharamia vya kushambuliwa viongozi wa Dini
kulikoanzia kwa kumwagiwa tindi kali Sheikh Soraga, kupigwa risasi Padri
Ambrose Mkenda, kuuliwa Padri huko Musoma, kupigwa risasi na kuuwawa
Padri Mushi na kushambuliwa kwa mapanga na kuuliwa Sheikh Ali Khamis Bin
Ali Khatibu wa Mwakaje kwa dhulma kulikofanywa na wahalifu ni jambo
lisilokubalika na Uislamu na Waislamu wenyewe. Aidha wahusika wa matendo
haya wawe wafuasi wa Dini yoyote ile bado watahesabika ni wahalifu
kwani vitendo vya kihalifu na kiharamia kamwe haviwezi kunasibishwa na
Dini fulani.
3.
Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar linaviomba vyombo
husika kufanya upelelezi wa kina kuhusu matukio haya kwa kuzingatia
uadilifu na misingi ya kazi zao ili kuwabaini wahalifu na kufikishwa
katika vyombo vya kisheria. Aidha Baraza linavitahadharisha vyombo hivyo
kuepuka kufanya kazi yao kwa kusukumwa na matashi binafsi, jazba,
chuki, matashi ya baadhi ya wanasiasa na viongozi wa Dini pamoja na
shindikizo la baadhi ya vyombo vya habari.
4.
Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar linalaani na kupinga
kwa nguvu zake zote kauli aliyoitoa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania
na baadhi ya vyombo vya habari kuihusisha Zanzibar na ugaidi kutokana
na tukio la kuuliwa Padri Mushi. Kauli hii inaonesha kuwa Mheshimiwa
Waziri anaibagua Zanzibar katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kwasababu tunavyoelewa sisi suala la usalama wa nchi ni suala la
Muungano hivyo huwezi kuihusisha Zanzibar pekee na suala la ugaidi.
Hivyo, Baraza linaona kuwa kauli hizi zinazotolewa ni mbinu za makusudi
za kuichafua Zanzibar katika Jumuiya ya Kimataifa kutokana na chuki
binafsi dhidi ya Zanzibar na watu wake.
5.
Aidha Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar linamtaka
Mheshimiwa Waziri kwa kulinda heshima yake kuwajibika kwa Watanzania kwa
kujiuzulu kutokana na kushindwa kulinda usalama wa wananchi wakiwemo
viongozi wa Dini ambao ndio walezi wa jamii.
6.
Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar linalaani kauli za
uchochezi zinazoendelea kutolewa na baadhi ya vyombo vya habari
zinazochochea chuki, uadui, hasama na mtafaruku kati ya Waislamu na
Wakristo na kusahau kuwa Waislamu wameishi na Wakristo kwa amani,
mapenzi na mashirikiano hapa Zanzibar karne na karne. Baraza linaona
kuwa vyombo hivyo vya habari vinatekeleza ajenda ya kuivuruga Zanzibar
kwa kuchochea vita vya kidini ili kufikia malengo yao wanayoyajua
wenyewe. Hivyo, Baraza linaiomba Serikali kuvidhibiti kwa kuvichukulia
hatua vyombo vyote vinavyotumia matukio haya kuchochea uadui na chuki
kati ya Waislamu na Wakristo.
7.
Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar linaviomba vyombo vya
habari vya Zanzibar kuwajibika kwa Wazanzibari wanaolipa kodi kwa
kuwapasha taarifa sahihi juu ya matukio muhimu yanayotokea katika jamii
yao badala ya wananchi kutegemea kupokea taarifa za upotoshaji na
uchochezi kutoka katika vyombo vya habari visivyotutakia mema.
8.
Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar linaziomba Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya
Zanzibar kuwasilisha kwa Watanzania taarifa ya wazi ya matokeo ya
uchunguzi wa matukio haya kwa kuanzia na lile la kumwagiwa tindi kali
Sheikh Soraga, kupigwa risasi Padri Ambrose Mkenda, kuuliwa Padri huko
Musoma, kupigwa risasi na kuuwawa Padri Mushi na kushambuliwa kwa
mapanga na kuuliwa Sheikh Ali Khamis Bin Ali Khatibu wa Mwakaje.
9.
Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar linawaomba
Wazanzibari wote kuwa watulivu katika kipindi hichi ambapo upelelezi wa
matukio haya ukiendelea. Aidha Baraza linawasihi Wazanzibari wote bila
ya kujali tofauti zao za kidini kulinda umoja wao na kudumisha amani
pamoja na kukataa kugawanywa ili kuwatoa katika ajenda yao ya msingi ya
kudai Mamlaka Kamili ya Zanzibar katika Muungano.
MOLA WETU MTUKUFU TUNAKUOMBA UINUSURU ZANZIBAR NA WATU WAKE DHIDI YA MAADUI WA NDANI NA NJE WASIOITAKIA MEMA NCHI YETU
Imesainiwa na:
Sheikh Ali Abdalla Shamte
Amir wa Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar
Amir wa Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar