Marehemu Mzee Amos Kaguta Museveni, ambaye ni baba mzazi wa Rais Yoweri Museveni wa Uganda.
KAMPALA, Uganda
“Rais Museveni na
familia yote ya Kaguta, inasikitika kutangaza kifo cha baba yao mpendwa Mzee
Amos Kaguta, 96, ambacho kimetokea leo Februari 22 saa 1 asubuhi kwenye Hospitali
ya Kimataifa ya Kampala”
MZEE Amos Kaguta Museveni, baba mzazi wa Rais Yoweri Museveni wa Uganda
(pichani kulia), amefariki dunia leo asubuhi, taarifa kutoka Ikulu zimethibitisha kifo hiki.
Amos Kaguta amefariki akiwa katika Hospitali ya Kimataifa ya
Kampala,
alikokuwa amelazwa kwa siku kadhaa kwenye Wodi ya Wagonjwa Mahututi (ICU).
Baba huyo wa Rais, alikimbizwa hapo kutokana na matatizo ya
tumbo aliyokuwa nayo, na kulazimisha familia yake kumkimbizia hapo kwa matibabu
zaidi.
“Rais Museveni na familia yote ya Kaguta, inasikitika
kutangaza kifo cha baba yao mpendwa Mzee Amos
Kaguta, 96, ambacho kimetokea leo Februari 22 saa 1 asubuhi kwenye Hospitali ya
Kimataifa ya Kampala.
“Familia inawashukuru madaktari wote kwa kujitoa na
kupigania maisha ya Mzee Kaguta hadi umauti ulipomkuta.
“Taarifa zaidi juu ya mazishi yake zitatangazwa baadaye. Apumzike
kwa Amani Mzee Kaguta,” ilisomeka taarifa fupi kutoka kwa Katibu Mkuu Msaidizi
wa Idara ya Habari Ikulu, Lindah Nabusayi Wamboka.
Daktari wa familia, Diana Atwine alisema kuwa Mzee Kaguta
alikimbizwa Hospitali baada ya kuanza kulalamika mamumivu ya tumbo, huku habari
nyingine zikieleza kuwa marehemu alikuwa na matatizo ya kichwa.
Imeelezwa pia kwamba, Rais Museveni alikuwa akitembelea mara
kwa mara hospitalini hapo, kujua maendeleo ya hali ya baba yake, hadi kifo
kinamfika.
Kifo cha Amos Kaguta, kinamuacha Rais Museveni bila wazazi,
baada ya mama yake mzazi Esteri Kokundeka kutangulia mbele ya haki mwaka 1997.
Mungu alitoa, Mungu ametwaa –
Jina lake lihimidiwe, pia ailaze roho ya marehemu mahali pema PEPONI, Ameen.