JOHNNESBURG, South Africa
MWANARIADHA nyota wa mbio za walemavu Oscar Pistorius,
hatimaye leo Ijumaa mchana ameachiwa kwa dhamana, kutokana na kesi ya mauaji ya
mpenzi wake inayomkabili.
Umauzi wa Pistorius kupewa dhamana
ulitolewa na Jaji Desmond Nair, na kuamsha
furaha miongoni mwa wanafamilia wa Pistorius na mashabiki wake ndani na nje ya
Mahakama ya jijini Pretoria, huku mwenyewe akiwa amesimama imara kama
aliyenyimwa dhamana hiyo.
Kuachiwa kwa Pistorius kunafuatia
wiki nzima ya usikilizaji wa maelezo ya namna mwanariadha huyo alivyompiga risasi
na kumuua mpenzi wake Reeva Steenkamp wakiwa
katika jumba lao la kifahari, asubuhi ya Siku ya Wapendao Februari 14.
Waendesha mashtaka wamesema Pistorius,
26, anakabiliwa na kesi ya kujibu kutokana na kupiga risasi nne kwenye mlango
wa bafu ukiwa umefungwa, huku mpenzi wake akiwa ndani. Steenkamp, 29, alikutwa
na majeraha ya risasi katika kichwa chake, mkononi na kwenye nyonga.
Upande unaomtetea Pistorius
umeendelea kusisitiza kuwa mkali huyo alimuua mkewe kimakosa, wakisema alifanya
hivyo kutokana na kuhisi kuwa amevamia na jambazi, wakataka apewe dhamana
kuweza kujiandaa, kuikabili kesi hiyo iliyoteka hisia za wengi duniani.
Kesi kamili inayomkabili nyota huyo
inaweza kuanza kusikilizwa miezi kadhaa ijayo, na Pistorius nyota wa Olimpiki
na Paralimpiki, ambaye hana miguu yote miwili, anakabiliwa na hatari ya kifungo
cha maisha kama akikutwa na hatia ya mauaji.
Dhamana hii imefungua milango ya
matumaini miongoni mwa wanafamilia na mashabiki wake, kuwa anaweza kushinda
vita ya kuepuka kifungo cha maisha.