Kaimu
kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP)
Zuberi Mwombeji na Mkuu wa askari wa hifadhi ya wanyama pori kwa Jamii
kutoka Enduimeti Bw. Joseph Laizer wakionyesha madawa ya kulevya aina ya
bangi ambayo yalikamatwa eneo la Mbuga nyeupe lililopo wilaya ya
Longido Mkoani Arusha.(Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi
Arusha)
Na: Rashid Nchimbi wa jeshi la Polisi Arusha
Mtu mmoja aitwaye Joseph Loiruku Manina Mkazi wa Losinoni wilayani
Arumeru anashikiliwa na jeshi la Polisi Mkoani hapa baada ya kukutwa na
magunia 26 ya madawa ya kulevya aina ya bangi ambayo yalikuwa
yanasafirishwa kwa kutumia wanyama aina ya Punda toka eneo la Losinoni
lililopo wilaya ya Arumeru kwenda nchi jirani ya Kenya ambapo kila Punda
alikuwa amebeba magunia mawili. Hayo yameelezwa na
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Mrakibu Mwandamizi wa Polisi
(SSP) Zuberi Mwombeji alipokuwa anaongea na waandishi wa habari nje ya
jengo la Makao Makuu ya Jeshi hilo Mkoani hapa na kufafanua kwamba,
tukio hilo lilitokea juzi tarehe 11/02/2013 muda wa saa 9:30 alasiri
katika eneo la Oldonyondari lililopo Mbuga Nyeupe wilayani Longido.
Kaimu Kamanda huyo alisema kwamba, mtuhumiwa huyo akiwa na wenzake
wanne walikuwa wamepumzika katika boma mojawapo ndipo ghafla askari hao
walitokea eneo hilo na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja huku wengine
wanne wakifanikiwa kukimbia. Alisema mafanikio hayo yalitokana a
taarifa zilizotolewa na raia wema toka tarehe 09/02/2013 ambazo
zilifanyiwa kazi na hatimaye kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo.
Mara baada ya mahojiano ya awali, mtuhumiwa huyo alikiri kuhusika na
tukio hilo na bado jeshi hilo linaendelea na upelelezi ili kuweza
kuwakamata watuhumiwa wengine waliokimbia.
Kufuatia mafanikio hayo Kaimu kamanda huyo ameendelea kuwashukuru
wananchi wa Mkoa huu kwa ushirikiano mkubwa kwa jeshi hilo na kuwaomba
waendelee kutoa taarifa zinazohusu uhalifu na wahalifu.
Ukiachana na mafanikio ya ukamataji wa madawa ya kulevya aina ya
mirungi yaliyopatikana hivi karibuni baada ya jeshi hilo kukamata magari
mawili kwa nyakati tofauti yakiwa na viroba 374, hivi karibuni jeshi
hilo limekamata magunia 117 ya madawa ya kulevya aina ya bangi hivyo
kufanya jumla ya magunia 143 yaliyokamatwa kwa muda wa mwezi mmoja
pamoja na tukio hili.