Na Walter Mguluchuma-Blogs Za mikoa
Mpanda.
Mtu mmoja mkazi wa kijiji cha Kapanga kata ya Katuma Gilbert James (39) anashikiliwa na jeshi la polisi mkoa wa Katavi kwa tuhuma za kumuua mwalimu wa shule ya msingi Kapanga Godfrey William (29) kutokana na wivu wa mapenzi.
Kaimu
kamanda wa polisi wa mkoa wa Katavi Joseph Myovela alisema kuwa
mtuhumiwa alitenda kosa hilo hapo February 9 mwaka huu majira ya saa
tano usiku.
Siku
hiyo ya tukio marehemu Godfrey alikwenda nyumbani kwa Gilbert pasipo
kujua kama mwenye nyumba yupo na kugonga dirishani ili aweze kufunguliwa
mlango na mke wa mwenye nyumba ambae anadai kuwa alikuwa na mahusiano
ya kimapenzi na marehemu Godfrey .
Kaimu
kamanda alisema baada ya mwenye nyumba kusikia sauti ya Godfrey
alijiandaa na kutoka na silaha ya jadi aina ya mundu (fyekeo) na kuanza
kumkimbiza marehemu.
Pamoja na kukimbizwa marehemu huyo hakuweza kupiga hata mayowe ya kuomba msaada kwa majirani.
Myovela
alieleza Gilbert aliweza kufanikiwa kumkimbiza na alipomkuta alimfyeka
kwa mundu sehemu ya juu ya mguu juu ya paja la kulia hali ambayo
ilimfanya marehemu alale chini na kuanza kupiga mayowe ya kuomba msaada
kwa majirani.
Majirani walifika katika eneo hilo na kumkuta marehemu akiwa amelala chini huku akiwa akimwaga damu ambapo alifariki muda mfupi.
Kaimu
kamanda alisema majirani hao baada ya kutokea kifo hicho walitaka kujua
chanzo cha tukio hilo ndipo Gilbert alipowaeleza kuwa marehemu alifika
nyumbani kwake na kugonga dirisha na alipotakiwa ajitambulishe hakufanya
hivyo hali iliyopelekea amdhanie kuwa ni mwizi.
Myovela alisema kuwa uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa marehemu huyo alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na mke wa Gilbert.
Alisema na ndio maana siku hiyo aliandaa mtego baada ya kuwa na taarifa kuwa mkewe anamahusiano ya kimapenzi na mwalimu Godfrey na siku hiyo marehemu alikuwa akijua kuwa mwenye nyumba huyo hayupo yuko shambani.
Mshitakiwa anategemewa kufikishwa mahakamani wiki ijayo mara upelelezi utakapokuwa umekamilika.
