Mwenyekiti
wa taifa wa Chadema, Freeman Mbowe, amekibebesha Chama Cha Mapinduzi
(CCM) vurugu na mauaji ya kidini huku akiwaonya viongozi wa Chadema
watakaoshiriki na kuhamasisha chuki dhidi ya dini nyingine kuwa
watafukuzwa kwenye chama hicho asubuhi na mapema.
“Udini ni sera ya CCM, wamelikoroga, sasa tunataka walinywe,”
alisema jana wakati akifungua mkutano wa viongozi wa majimbo 33 na
mikoa ya Kanda ya Kaskazini inayojumuisha mikoa ya Manyara, Arusha,
Kilimanjaro na Tanga, ikiwa ni sera yao ya majimbo.
Pamoja
na kuwaonya viongozi, Mbowe pia aliwataka wanachama wa Chadema popote
pale walipo wasishiriki kuwabagua wenzao kwa imani ya dini bali
waheshimu imani za watu wengine.
Aidha
Mbowe alisema; “Chadema inalaani vikali mauaji ya viongizi wa dini
yanayotokea maeneo mbalimbali nchini…tunaitaka CCM na serikali yake
kuwajibika dhidi ya mauaji hayo.”
“Kuona
kiongozi wa dini akimwagiwa tindikali, akipigwa na hata kuuawa kwa
sababu za kidini sio mambo ya kujivunia hata kidogo…CCM ndiyo iliyokuwa
ikilea udini na hapo ndipo ilipotufikisha…tunataka CCM na serikali yake
iwajibike kwa hilo.”
Alisema
Mkristu hana haki ya kumhukumu Mwislamu na wala Mwislamu hana haki ya
kumhukumu Mkristu, hivyo Chadema kimeamua kuchukua hatua kali dhidi ya
mwanachama ye yote bila kujali wadhifa wake atakayehamasisha chuki za
kidini.
Alisema
sera ya udini iliaasisiwa na CCM kama mbinu yao ya kuwafanya waendelee
kubakia madarakani lakini hali inavyoonekana sasa inatisha amani na
umoja wa taifa.
