Mgeni rasmi akipanda mti wa uzinduzi
Jumla ya miti ya asili 4,377
ambayo ni rafiki kwa utunzaji wa mazingira ikiwemo vyanzo vya maji imepandwa
katika eneo lenye chanzo cha maji cha Ng’wenyo kata ya Tandala wilayani Makete
katika uzinduzi wa siku ya upandaji miti kiwilaya
Zoezi hilo limeongozwa na Afisa tawala wilaya ya
Makete Bw. Onespholia Mahenge kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Makete Mh.
Josephine Matiro ambaye alikuwa mgeni rasmi katika shughuli hiyo
Akizungumza mara baada ya kupanda
mti wa ufunguzi Bw. Ngogo amewataka wananchi waliofika eneo hilo kuendelea
kupanda miti hiyo katika eneo hilo kwa lengo la kutunza mazingira ya kata hiyo
Amesisitiza kwa kipindi hiki cha
masika ni vyema kila mwananchi akapanda miti mingi kadri awezavyo ili kuboresha
mazingira ikiwemo kutunza vyanzo vya maji ambavyo kwa kiasi kikubwa vimekuwa
vikiharibiwa na watu wachache
Zoezi hilo mbali na kupanda kiasi hicho kikubwa cha
miti lakini pia limefanyika zoezi la kuharibu miti ya kigeni ambayo inaharibu
vyanzo vya maji ikiwemo mipaini
Kwa upande wake afisa maliasili
na mazingira wilaya ya Makete Bw. Uhuru Mwembe amesema wilaya ya Makete imekuwa
na utaratibu wa kupanda miti kwa wingi hasa miti ya asili hasa kwenye vyanzo
vya maji huku akiutaka uongozi wa kata ya Tandala kuendelea kuitunza miti hiyo
iliyopandwa ili iote na kustawi
Amesema katika upandaji huo wa
miti miti 2,665 imetolewa na halmashauri ya wilaya ya Makete, miti 1,119
imetolewa na mheshimiwa diwani wa kata ya Tandala Egnatio Mtawa, na miti 521
imetolewa na Udiakonia tandala
Ameitaja aina ya miti iliyopandwa
ya kuhifadhi vyanzo ya maji kuwa ni Midobole, mitsalugasi, mitsa, mivengingi,
mihove, mienekilunga, milungu na mikuyu
Miti hiyo imepandwa na viongozi
kutoka wilayani, shirika la Sumasesu, chuo cha ualimu Tandala, shule ya msingi
tandala mazoezi, shule ya sekondari Lupalilo, pamoja na wananchi wa kata ya
Tandala