WAZEE WA MTWARA WATINGA DAR, KISA GESI ISITOKE MTWARA

Sakata la kugundulika kwa gesi asilia mkoani Mtwara, linazidi kupamba moto baada ya wazee wanaodai kutoka mkoani Mtwara kuwasili jijini Dar es Salaam na kutoa tamko wakiitaka serikali kuacha mara moja mpango wake wa kuisafirisha gesi hiyo kutoka mjini Mtwara hadi jijini Dar es Salaam. Badala yake, wazee hao kutoka Manispaa ya Mtwara-Mikindani, wametaka kijengwe kituo cha kusafishia gesi hiyo mkoani Mtwara. 
Akisoma tamko la wazee hao mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Suleiman Mademu, wazee hao wamesema kuwa, wanawawakilisha wananchi wa mkoa huo pamoja na vyama tisa vya siasa vilivyoungana vya ADC, APPT-Maendeleo, Chadema, DP, NCCR-Mageuzi, Sau, TLP na UDP. Mademu amesema kuwa, serikali inafanya kinyume cha ilivyowaahidi wananchi wa Mtwara hapo awali wakati gesi hiyo inapogundulika ambapo serikali imeahidi wananchi wa Mtwara watakuwa wa kwanza kunufaika na gesi hiyo kwa kujenga kituo cha kuisafisha. 
Kutokana na hali hiyo, ameunga mkono hatua ya wananchi wa Mtwara kufanya maandamano Desemba 27, mwaka jana kupinga gesi hiyo kusafirishwa kwenda Dar es Salaam na kusema kuwa, maandamano hayo yamefuata taratibu za nchi na kuwa, hatua hiyo ni moja ya njia za kufikisha vilio na matatizo yanayowakabili wananchi. Amesema kuwa, katika kufanya maandamano hayo, hawakuwa na dhamira mbaya kwani maandamano yalikuwa ya amani na yamelenga kufikisha kilio chao serikalini. 

Ameongeza kuwa, wanachohitaji ni vitendo kutawala badala ya ahadi kama ilivyozoeleka nchini huku akisema kuwa, wanazo rekodi mbalimbali za kupewa ahadi ambazo hazitekelezeki ambazo ni kujengewa barabara, kuwekewa umeme, kuimarishwa kwa bandari, mikopo kwa ajili ya ujasiriamali na viwanda vidogo kwa ajili ya kubangua korosho. 


 

Katika tamko hilo, wazee hao wameitaka serikali kuratibu mchakato mzima wa matumizi ya rasilimali gesi kwa kuishirikisha mikoa ya Kusini kwa hatua zote na kwa uwazi na kituo cha kufua umeme kijengwe mjini Mtwara. Aidha wazee hao wamevitaka vyama vya siasa kutojitafutia umaarufu binafsi kwa ajenda hiyo ya gesi, badala yake vishirikiane kwa njia ya kuleta maendeleo kwa taifa, kwani kaulimbiu yao ni “gesi kwanza vyama baadaye.”
 
Chanzo:The chief


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo