Na: Rashid Nchimbi wa Jeshi la
Polisi Arusha
Mkuu wa Polisi wilaya ya
Arusha Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Gilles Muroto amewaambia wakazi wa
Mtaa wa Sanawari waliopo Kata ya Sekei iliyopo halmashauri ya jiji la
Arusha waunganishe nguvu zao pamoja ili waweze kuushinda uhalifu.
Hayo aliyasema jana katika mkutano kati
jeshi la Polisi na wananchi hao uliofanyika katika uwanja wa wazi uliopo
mtaani hapo ikiwa ni muendelezo wa mkakati wa jeshi hilo juu ya utoaji
wa elimu ya polisi jamii kuanzia ngazi ya mtaa na vitongoji vya Mkoa huu
wa Arusha.
Mkuu huyo wa Polisi wilaya alisema
kitendo cha watu wachache kujitokeza kuhudhuria katika mkutano huo ambao
ulikuwa unajadili mambo mbalimbali ya maendeleo ya mtaa pamoja na
masuala ya ulinzi ni dalili tosha kwamba baadhi ya wakazi wa eneo hilo
hawana umoja.
“Hii inashangaza yaani mkutano ambao
umetangazwa karibu kila nyumba na una lengo la kujadili maendeleo ya
mtaa ambao umehudhuriwa na viongozi wa mtaa pamoja na Diwani wa kata
lakini watu wachache, hii ni hatari na hamtaweza kusonga mbele.” Alionya
Mkuu huyo wa Polisi wilaya.
Alisema hali hiyo ya utengano ndio
inayotoa mwanya kwa wahalifu kufanya uhalifu kwani mpaka hivi sasa mtaa
huo hauna vikundi vya ulinzi shirikishi kwa kuwa wananchi hawahudhurii
katika mikutano ili waweze kushirikiana na jeshi la Polisi kujadili
suala hilo.
Mrakibu huyo Mwandamizi wa Polisi
alisema kwamba, suala la ulinzi si la kiitikadi za kisiasa bali watu wa
vyama vyote wanatakiwa washiriki kwani mhalifu anapovamia sehemu
hamuulizi mwenye mali kama ni kiongozi, mwanachama au shabiki wa chama
gani bali anaangalia kile anachokiihitaji.
Aliwataka wananchi wa Mtaa huo kuanza
kuchukua hatua za kupambana na wahalifu kwa kuanzisha kikundi cha ulinzi
shirikishi ambacho kitaendeshwa kwa michango ya kila mkazi ambaye
atapaswa kufanya hivyo kwa ajili ya kuwalipa posho walinzi pamoja na
ununuzi wa vifaa kama vile tochi, sare na kadhalika.
Aliongeza kwa kusema ili kikundi
kikamilike inatakiwa wawe na silaha ya moto ambayo itawasaidia katika
shughuli za doria badala ya kutumia marungu pekee. Alisema kikundi hicho
kitakuwa kinafanya kazi hiyo kwa kushirikiana na jeshi la polisi ambapo
pale wanapoona kuna matatizo watakuwa wanawasiliana na yeye au viongozi
wengine wa jeshi hilo moja kwa moja ili waongezewe nguvu.
Mkutano huo uliohudhuriwa na Diwani wa
Kata ya Sekei Mh. Chrispin Tarimo, Mwenyekiti wa mtaa huo Godfrey
Mollel, Mkuu wa Kitengo cha Polisi Jamii Mkoa wa Arusha Mrakibu wa
Polisi Mary Lugola, Polisi Tarafa ya Themi Mkaguzi Msaidizi wa Polisi
Zuhura na askari wengine toka kitengo hicho ni utekelezaji wa ahadi
aliyoitoa Mkuu huyo wa Polisi wilaya kwa wenyeviti wa mitaa ya
halmashauri ya jiji Arusha ya kufanya mikutano na wananchi ili
kuimarisha ulinzi ndani ya wilaya ya Arusha.
Chanzo: www.mjengwablog.co.tz