UJANGILI WAPUNGUA HIFADHI YA TARANGIRE

 
Imebainishwa kuwa matukio ya ujangili kwenye Hifadhi ya Taifa ya Tarangire mkoani Manyara yamezidi kupungua kwani kwa muda wa miezi sita iliyopita hakukuwepo na matuki makubwa ya kuuawa tembo wa hifadhi hiyo.
 
Hayo yamebainishwa na aliyekuwa mkuu wa hifadhi ya Tarangire Martin Loibooki ambaye hivi sasa ni mkurugenzi wa uhifadhi wa hifadhi za Taifa (Tanapa) wakati akizungumza kwenye tafrija ya kumuaga na kuukaribisha mwaka mpya iliyofanyika hifadhini hapo mkoani manyara. 
 
Alibainisha kuwa hivi sasa ujangili umepungua kwa kiasi kikubwa kwenye hifadhi hiyo ambayo sehemu yake kubwa ipo wilayani Babati mkoani Manyara na eneo la wilaya Kondoa mkoani Dodoma na wilayani Monduli mkoani Arusha.
Alisema kuwa ujangili huo umepungukua kwa kiasi kikubwa kutokana na ushirikiano wanaopewa na jamii inayozunguka eneo hilo,askari wao na askari polisi kwani walifanikiwa kukamata silaha mbalimbali ikiwemo bunduki kubwa na risasi.
 
Aliendelea kusema kuwa wanashukuru hivi sasa mgogoro huo umefikia tamaki kwani mwenyekiti wa kijiji hicho na wananchi wake wametambua umuhimu wa hifadhi hii ya Taifa ya Tarangire ambayo ni ya tatu kwa kuingiza mapato nchini.
 
Aidha alitaja miongoni mwa changamoto zinazowakabili ni migogoro ya mipaka baina ya hifadhi hiyo na vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo ikiwemo kijiji cha Kimotorok cha kata ya Loiborsiret wilayani Simanjiro.
 
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Manyara Elaston Mbwilo alisema kuwa baadhi ya watu wanaohujumu hifadhi za Taifa kwa kufanya ujangili hawana uzalendo na hawatangulizi maslahi ya Taifa kwani hifadhi zinaingiza fedha nyingi za kigeni.
 
Aliongeza kuwa kila mmoja kwa nafasi yake ajitahidi kuboresha Hifadhi ya Taifa ya Tarangire ili kuweza kuongeza mapato kwani kwa asilimia kubwa mishahara ya watumishi inatokana na pato la utalii.
 
‘’Jamani fedha za kuwalipa mishahara walimu,madaktari,askari wetu na watumishi wengine wa Serikali zinatokana na fedha zinazoingia kupitia utalii hivyo jamii inapaswa kutunza hifadhi ili hifadhi nazo zitutunze,” alisema mkuu wa mkoa wa Manyara. 
 
Alimalizia kwa kusema kuwa ni lazima elimu itolewe kwa jamii kuhusu uhifadhi wa wanyama pori ili wawatunze na kuheshimu mipaka ambayo imewekwa sehemu ya hifadhi ili kuepuka hasara za kuharibu mipaka ya Tarangire.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo