Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, Jaji Jospeh Warioba
Tume
ya Mabadiliko ya Katiba imetoa ufafanuzi kuhusu taarifa zilizoandikwa
na vyombo mbalimbali vya habari yakiwemo baadhi ya magazeti ya jana (Alhamisi, Januari 17, 2013)
ambazo zinaashiria kuwa Tume inakataa kupokea baadhi ya
maoni yanayowasilishwa kwake na makundi mbalimbali.
Taarifa
hizo za vyombo vya habari zimetokana na kauli ya Mkurugenzi Mkuu wa
Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) Dkt. Ramadhan Mlinga
aliyoitoa mara baada ya taasisi yake kuwasilisha kwa Tume maoni kuhusu
Katiba Mpya siku ya Jumatano, tarehe 16 Januari, 2013 katika Ukumbi wa
Karimjee jijini Dar es Salaam.
Kwa
mujibu wa taarifa hizo, mara baada ya PPRA kuwasilisha maoni kwa Tume,
Wajumbe wa Tume walisita kupokea maoni ya taasisi hiyo na badala yake
kuagiza PPRA kuandaa maoni tena na kuyawasilisha katika Tume ndani ya
wiki mbili kuanzia tarehe 16 Januari, 2013.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa leo (Alhamisi, Januari 17, 2013) kwa
vyombo vya habari na Katibu wa Tume hiyo Ndg. Assaa Rashid, taarifa hizo
siyo za kweli na kuwa Tume yake haina mamlaka ya kisheria ya kukataa
kupokea maoni.
“Tume
inapenda kuwataarifu wananchi, makundi, taasisi na wadau wengine wote
kuwa Tume haijakataa na haina mamlaka ya kisheria ya kukataa kupokea
maoni ya mtu, jumuiya, taasisi au kundi lolote,” alisema Ndg. Assaa
katika taarifa yake na kuongeza:
“Katika mikutano inayoendelea (na makundi
mbalimbali), kabla ya kuhitimisha mkutano husika, Tume huomba
chama cha siasa, jumuiya, taasisi au mtu aliyewasilisha maoni kutoa
ufafanuzi wa hoja mbalimbali zilizojitokeza katika kikao” alisema na
kufafanua kuwa ufafanuzi huu hutolewa kwa hiari palepale katika mkutano
au kwa maandishi baada ya siku kadhaa ambazo Tume hukubaliana na mtu au
kikundi kilichowasilisha maoni.
Akifafanua zaidi Ndg. Assaa ameseama kuwa mikutano inayoendelea kati ya Tume na Makundi mbalimbali
inafuatia kukamilika kwa mikutano ya kukusanya maoni binafsi ya wananchi
tarehe 19 Disemba mwaka jana (2012).
“Kwa
msingi huu, katika mkutano kati ya Tume na PPRA uliofanyika juzi, tarehe
15 Januari, 2013, Tume iliiomba
PPRA kuangalia uwezekano wa kutoa ufafanuzi wa masuala ya ziada ambayo
Tume ilitaka kupata maoni ya kitaalamu kutoka katika taasisi hiyo,”
alisema kiongozi huyo wa Tume na kuongeza kuwa ombi kama hilo pia
limetolewa kwa makundi mengine ambayo yameshakutana na Tume kutoa maoni
kuhusu Katiba Mpya.
Tume
ya Mabadiliko ya Katiba ilianza kazi rasmi tarehe 1 Mei mwaka jana
(2012) na wiki iliyopita ilianza kazi ya kukusanya maoni ya makundi na
watu mbalimbali kuhusu Katiba Mpya. Mikutano hii inatarajiwa kukamilika
tarehe 25 mwezi huu (Januari, 2013).