Polisi mkoani Rukwa
inawashikilia watu wawili, akiwemo askari polisi mwenye nambari G 1305
Ladislaus, maarufu kwa jina la Zinja, kwa tuhuma ya kumshambulia,
kumpiga na kumsababishia mauti kijana aliyetuhumiwa kuwa ni mwizi wa
baiskeli.
Kamanda wa Polisi mkoa wa
Rukwa, Jacob Mwaruanda alikiri kutokea kwa mkasa huo.
Pia, alithibitisha kuwa
watuhumiwa wote wawili, wanashikiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi na
uchunguzi wa tukio hilo unaendelea .
Alisema askari huyo
ambaye anafanya kazi katika kituo cha polisi mjini hapa, wakati mkasa
huo wa mauaji ukitokea, alikuwa likizo.
Mwaruanda alisema
aliyeuawa alitambuliwa kuwa ni Ally Thomson “Okocha’ (35),
anayetuhumiwa kuiba baiskeli ya David Mwaipopo "Mwaisa" (38) miezi
miwili iliyopita na taarifa ya tukio hilo iliripotiwa Kituo Kikuu cha
Polisi mjini hapa.
Inaelezwa kuwa tukio hilo
limetokea juzi saa nane na nusu mchana kwenye kitongoji cha Mazwi mjini
hapa.
Siku hiyo askari polisi
huyo akiwa na Mwaisa, walimkamata mtuhumiwa huyo na kuanza kumshambulia
kwa ngumi na mateke huku wakimpeleka kituo cha polisi.
Habari zinadai kuwa
wakiwa njiani, Okocha alianza kuishiwa nguvu kwa maumivu makali
mwilini. Walipomfikisha kituo cha polisi alipatiwa Fomu ya Matibabu
(PF3) na kupelekwa Hospitali ya Mkoa wa Rukwa mjini Sumbawanga kwa
matibabu, lakini alifariki dunia baada saa 10 jioni siku hiyo.
Taarifa za awali za
kipolisi zinadai kwamba Thomson alikuwa amefunguliwa kesi ya wizi wa
baiskeli yenye thamani ya Sh 100,000 miezi miwili iliyopita, lakini
alikuwa akijificha. Taarifa nyingine zilidai kwamba mtuhumiwa huyo
ametoroka na kukimbilia mkoani Mbeya.
Inadaiwa kwamba baada ya
Mwaisa kumuona ‘mwizi’ wake huyo akirandaranda mjini hapa, alimpigia
simu askari huyo ambaye tangu awali alikuwa akipeleleza kesi hiyo ili
aweze kumkamata na ndipo walipotumia nguvu kubwa katika kukabiliana
naye na kumsababishia kifo chake.
Pia tangu juzi kulikuwa
na taarifa za ndugu wa marehemu huyo waligoma kuchukua mwili wa
marehemu wao huyo, kwa madai ya kushinikiza kukamatwa kwa askari
polisi huyo, kwani hadi jana askari huyo alikuwa hajakamatwa huku
mtuhumiwa mwenzake (Mwasa), alikuwa tayari amekamatwa mara baada ya
kuthibitika kuwa Ally alifariki dunia akiwa anatibiwa.
Kwa mujibu wa mganga
aliyeufanyia uchunguzi wa kitabibu mwili huo, kwa masharti ya
kutoandikwa jina lake, alidai kuwa hata hivi tunaenda mitamboni
bado ndugu wa marehemu hawajafika mochwari kuchukua mwili wao
licha ya kuruhusu ufanyiwe uchunguzi .
“Kutokana na utata
uliojitokeza jana baada ya ndugu wa marehemu kuususa mwili wa
marehemu wao endapo kama utafanyiwa uchunguzi wa kitabibu bila
wao kushirikishwa basi hawatakuwa tayari kuuchukua wataachia
mamlaka kuuzika .. hivyo tuliwashirikisha na wakaafiki afanyiwe
uchunguzi wa kitabibu.
Lakini hadi sasa bado
hawajarudi kuuchukua labda ni kutokana na shinikizo walilotoa kuwa
lazima na askari aliyehusika naye akamatwe …“ alisema.
Hata hivyo hakuwa
tayari kuweka bayana kilichosababisha kifo cha marehemu huyo
licha ya kukiri kuwa alikuwa amepigwa kwa madai kuwa taarifa hiyo
itatolewa mahakamani wakati atakapotakiwa kutoa ushahidi na si
vinginevyo.
Chanzo kingine cha
kipolisi kinadai kuwa kutokana na hasira za wananchi wanaomlalamikia
askari huyo kusababisha kifo cha raia huyo endapo kama
atabainika kuwa hana hatia ni muhimu akapewa uhamisho kwani
maisha yake yatakuwa hatarini .
Kwa kile ninachoelezwa
kuwa ni shinikizo la wananchi wenye hasira kali pamoja na
wanandugu kususa mwili wa marehemu huyo, Jeshi la polisi mkoani
hapa limesalimu amri kwa kumkamata askari huyo ambaye sasa pamoja
na mtuhumiwa mwenzake (Mwasa) wanahojiwa kuhusiana na mkasa huo.
