Jumla ya Shilingi Bilioni 12
zimetumika kutekeleza Miradi ya Maendeleo 820 inayofadhiliwa na Mfuko wa
Maendeo ya Jamii TASAF kwa Awamu ya Pili ya Mfuko huo Unguja na Pemba.
Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Khalid
Suleiman ameyasema hayo leo katika Warsha ya siku mbili ya kuwajengea
uelewa wa Awamu ya Tatu ya TASAF juu ya ‘Mpango wa Taifa wa kunusuru
Kaya Maskini’ kwa Wajumbe wa Kamati za uongozi na menejiment za TASAF
–Zanzibar huko...
ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar
Beach Mazizini.
Amesema katika Miradi hiyo
jumala ya Miradi 433 imetekelezwa kwa upande wa Unguja na Pemba
imetekelezwa 387 ambapo Wananchi wa Zanzibar kwa ujumla wao waliweza
kuchangia Shilingi Bilioni 1.3 za Miradi hiyo.
Aidha amefahamisha kuwa
Zanzibar kwa ujumla iilifanya vyema katika kutekeleza Miradi hiyo licha
ya changamoto mbalimbali zilizojitekeza kwa kipindi hicho cha Awamu ya
pili ya TASAF.
Akifungua Warsha hiyo Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd amewataka wasimamizi wa
TASAF kuhakikisha kuwa Fedha zinazotolewa kwa ajili ya miradi hiyo
zinatumika ipasavyo ili kutimiza maelengo ya Mfuko huo.
Amesema licha ya Zanzibar
kufanya vyema katika Awamu ya Pili ya TASAF viongozi hao wanapaswa
kuyaendeleza mema yote yaliyofanywa katika Awamu mpya ikiwa ni pamoja na
kuziba mianya yote ya ubadhirifu wa pesa za miradi hiyo.
Balozi Seif ameongeza kuwa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea na azma yake ya kuunga
mkono utekelezaji wa Mpango huo katika Shehia za Unguja na Pemba ili
kuondoa umasikini kwa manufaa ya Jamii na Taifa kwa ujumla.
Amefahamisha kuwa Mpango huo
wa Kunusuru Kaya Maskini utaimarisha uwazi, uwajibikaji na kutoa fursa
kwa makundi mbalimbali kushiriki kwa kutumia mfumo madhubuti wa kubaini
Walengwa katika Shehia.
Balozi Seif amewataka
Washiriki wa Semina hiyo kushiriki kikamilifu na kuwa makini ili
kufahamu vyema taratibu na miongozo ya utekelezaji wa Awamu hiyo ya Tatu
ya Mfuko huo na hatimaye kufanyia kazi kikamilifu.
Awali akitoa Shukrani zake
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Ladislaus Mwamanga ameishukuru Serikali na
Wananchi kwa ujumla kutokana na ushirikiano walioutoa katika Awamu
zilizopita na kuomba mashirikiano hayo yaendelezwe kwa Awamu ya Tatu.
Aidha Mkuu wa Mkoa wa Kusini
Pemba Juma Kassim Tindwa akitoa shukrani kwa niaba ya Washiriki
amemuahidi Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif kuwa watatumia uwezo wao
wote kuhakikisha Miradi ya maendeleo ya TASAF inasimamiwa vyema na
kufikia lengo lililokusudiwa.
Warsha hiyo ya TASAF Awamu ya
Tatu inaongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Abdallah Mwinyi na
kuwashirikisha Wakuu wa Mikoa ya Unguja na Pemba,Wakuu wa Wilaya na
Menejiment za TASAF –Zanzibar ambapo mada mbalimbali zitawasilishwa
kuwajengea uwezo viongozi hao kuhusu awamu hiyo Mpya.
IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR
22/01/2013