Baadhi ya wanafunzi wa Sekondari ya Kwagunda moja ya shule za kata wakizungumzia changamoto mbalimbali za elimu
Mwalimu wa Taaluma wa Sekondari ya Kwagunda, Halila Mohamed akizungumza na mwandishi wa Thehabari.com (hayupo pichani)
Na Mwandishi wa Thehabari Korogwe Vijijini
UTORO wa kudumu kwa idadi kubwa ya wanafunzi wa
Sekondari hasa zile za Kata katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe
unatishia maendeleo ya elimu eneo hilo. Uchunguzi uliofanywa na
mwandishi wa habari hizi juzi kwa baadhi ya sekondari umebaini hali hiyo
sasa inatisha kwani inaongezeka kwa kasi karibuni katika kila shule za
sekondari eneo hilo.
Katika sekondari za Kwagunda, Kwashemshi, Mulungui pamoja na Bungu
vitendo vya utoro wa kudumu kwa wanafunzi vinaongezeka kwa hali ya juu
jambo ambalo linakwamisha maendeleo ya elimu eneo hilo.
Akizungumzia
hali ya utoro, Mwalimu wa Taaluma wa Sekondari ya Kwagunda, Halila
Mohamed alisema shule hiyo hupokea wanafunzi 180 wanaojiunga kidato cha
kwanza kila mwaka lakini wanaofika kidato cha nne ni 80 pekee, huku
idadi kubwa wakiishia kutoroka.
Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mlungui iliyopo Kata ya Bungu wilayani Korogwe, Sylvester Msigwa akizungumza shuleni hapo
Alisema idadi kubwa ya watoro hukimbilia kufanya vibarua katika machimbo ya matofari ya kuchoma kijijini hapo huku wengine wakifanya vibarua kwa wakulima na wafugaji wanaozunguka eneo hilo.
“Kibaya zaidi hutoroka na baadhi yao kuonekana kwenye mitihani
tu…kimsingi mwamko wa elimu eneo hili bado upo chini sana kwa wanafunzi
wenyewe pamoja na wazazi wao…,” alisema Bi. Mohamed.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Kwashemshi, Ezra Gweya alisema kipindi cha kilimo idadi kubwa ya wanafunzi shuleni kwake hukimbilia mashambani jambo ambalo huathiri maendeleo ya taaluma shuleni hapo.
“Utoro hapa shuleni kwetu upo, wengine huamua kutoa taarifa kabisa
shuleni kwamba wanaandaa mashamba ya wazazi wao kwa ajili ya
kilimo…wakati mwingine ukiangalia wanasema wanategemea kilimo kwa kipato
hivyo wanalazimika kwenda mashambani,” alisema Gweya.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Bungu, Dismas Kimweli alisema kati ya Januari hadi Juni 2012 shule yake ina jumla ya wanafunzi 226 kutoka kidato cha kwanza hadi cha nne ambao ni watoro wa kudumu.
Naye Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mlungui iliyopo Kata ya Bungu wilayani Korogwe, Sylvester Msigwa alisema idadi kubwa ya wanafunzi watoro wanaishi peke yao kwenye ‘mageto’ hivyo kuwa na uhuru mkubwa.
“Wanafunzi hawa huwa na uhuru kupindukia, pia wanakuwa hawana nidhamu kwasababu wanakuwa mbali na walimu..hii ni changamoto kubwa sana..lakini natoa wito kwa wale wanaowapangisha wanafunzi nao wabebe jukumu la kuwalea wale watoto ipasavyo, wakiona mtoto anakwenda kinyume na maadili wawakemee,” alisema Msigwa.
Short URL: http://www.thehabari.com/?p=25694