RIPOTI ya mwaka huu ya Shirika la Kimataifa
linalopambana na ufisadi duniani (Transparency Intenational) inaeleza
kuwa rushwa imechochea kwa kiasi fulani mgogoro wa uchumi duniani, huku
Somalia na Korea Kaskazini zikiongoza.
Pamoja na kuwepo kwa kampeni mbalimbali na katika maeneo tofauti
duniani dhidi ya ufisadi, lakini faharasa ya rushwa ya shirika la
Transparency International inaonesha kuwa theluthi mbili kati ya mataifa
176 yamepata chini ya asilimia 50. Hiyo inamaanisha zimekithiri sana
kwa rushwa.
Ripoti hiyo inaeleza kwamba kukithiri kwa vitendo vya ufisadi ndiko
kulikochochea baadhi ya viongozi kulazimishwa kuondoka madarakani mwaka
jana, ingawa bado kiwango chake kimeendelea kuwa cha juu zaidi katika
mataifa mengi.
Mataifa matatu bora barani Ulaya
Kwa mara nyingine, Dernmark, Finland na New Zealand zimekuwa na
rekodi nzuri kwa mujibu wa Transparency International wakati Afghanstan,
Korea Kasikazini na Somalia zikisalia mkiani katika kadhia ya rushwa.
Kwa kuzingitia kipimo kinachoanisha sifuri – kama kiwango kibaya
zaidi cha rushwa – mpaka 100 – ikiwa ndiyo rekodi nzuri kabisa,
Dernmark, Finland na New Zealand zimefungana kwa kupata alama 90. Lakini
Afghanstan, Korea Kaskazini na Somalia kila moja imepata alama 8.
Hali ilivyo katika mataifa ya Kiarabu
Pamoja na hayo, ripoti hiyo imeonesha kumekuwa na mafanikio kidogo
sana katika mataifa ya Kiarabu yaliyokumbwa na vuguvugu la kisiasa.
Mataifa hayo ni pamoja na Misri na maeneo mengine ya Mashariki ya Kati.
Mataifa ambayo ni kiini cha mgogoro wa madeni yameendelea kupata alama
duni zaidi, ambapo tatizo hilo la mgogoro wa madeni limeonekana kama
chachu ya vitendo vya rushwa. Ugiriki imepata alama 36, Italia 42, Ureno
63 na Uhispania 65.
Mkurugenzi Mkuu wa Transparency International, Cobus de Swardt,
ameyataka mataifa yenye nguvu za kiuchumi duniani yanapaswa kuonesha
mfano kwa kuhakikisha taasisi zake zinasimamia uwazi na kwamba viongozi
wanawajibika katika hilo.
Mataifa ya Magharibi yanayoongoza kiviwanda, kama Uswis, Canada,
Australia na Sweden yanashikilia tena ile nafasi yake ya kuwa safi
katika kudhibiti tatizo la rushwa. Lakini China, kama taifa namba mbili
kwa nguvu za kiuchumi duniani limepata alama 39.
Taifa kubwa kabisa lenye nguvu za kiuchumi duniani Marekani limepata
alama 73 na Ujerumani, ambalo ni taifa lenye uchumi mkubwa kuliko yote
barani Ulaya, ikiwa na alama 79. Urusi, pamoja na kuwa na utajiri mkubwa
wa maliasili yake, inaonekana kufanya jitihada kidogo sana katika
kukabiliana na tatizo la rushwa. Taifa hilo limeshika nafasi ya 133
katika nchi 176 katika kudhibiti rushwa kwa mujibu wa utafiti wa mwaka
huu wa Transparency International.