WALIMU wa Shule ya Sekondari ya Kata ya Ruaruke
wilayani Rufiji, Mkoa wa Pwani, wameitelekeza shule hiyo kutokana na
kukithiri kwa vitendo vya baadhi ya wanafunzi kuwadhalilisha kimapenzi,
ikiwamo kuwabaka baadhi yao.
Habari
zimeeleza kuwa mbali na udhalilishaji huo, wanafunzi hao wamekuwa
wakiwatishia maisha walimu wao kwa namna mbalimbali. Katika moja ya
vitisho hivyo, wamechoma moto nyumba zao tatu.
Habari hizo zimeeleza kwamba walimu hao wamelazimika kuikimbia shule
hiyo baada ya baadhi ya walimu wa kike kutongozwa na wanafunzi, kupigwa
mabusu kwa nguvu hadharani, kutishiwa kuchomwa visu na kuchorwa vikatuni
vya kudhalilisha.
Mmoja wa walimu hao ambaye hakutaka kutajwa gazetini akihofia
kushughulikiwa na wanafunzi hao alisema amelazimika kuikimbia pamoja na
walimu wenzake wote, kwa kuwa wameshindwa kudhibiti tabia hiyo kutokana
na vijana hao kuungwa mkono na wazazi wao.
Akizungumza kwa simu akiwa Dar es Salaam, mwalimu huyo alisema shule
hiyo yenye wanafunzi 485, imepoteza mwelekeo, haitawaliki na mazingira
yake hayavutii walimu, hasa wa kike, kuishi na kufanya kazi.
Hata hivyo, mwalimu huyo hakuwa tayari kueleza kwa undani kuhusu vitendo hivyo vya ubakaji lakini alieleza kwamba vimekuwa vikitokea walimu hao wanapokuwa katika matembezi usiku. Vitendo hivyo vimekuwa vikitokea baada ya wanafunzi hao kuwatongoza walimu wao na kukataa kufanya nao mapenzi.
Mwalimu huyo alidai kuwa walimu wamekuwa wakitishiwa kuchomwa visu na
nyumba zao kuchomwa moto, huku walimu wanne wa kike wakidhalilishwa
kimapenzi kwa kupigwa mabusu na kutongozwa na wanafunzi.
Alipoulizwa kuhusu tukio hilo, Ofisa Elimu Sekondari, Adnan Mwenda alisema asingependa kuzungumzia tatizo hilo kwa kuwa siyo msemaji. Akashauri atafutwe mkurugenzi wa wilaya… “Unaweza kuzungumza mambo mengine yakakuletea matatizo,” alisema Mwenda kabla ya kuelekeza atafutwe mkurugenzi.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji, Leonard
Rwegasira alithibitisha walimu hao kuikimbia shule hiyo na kusema kuwa
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, itakutana hivi karibuni kujadili
suala hilo.
“Ni kweli shule hiyo imetelekezwa, walimu wamekimbia na wanafunzi hawaendi shule. Tatizo tunalifahamu na Mkuu wa Wilaya anafanya jitihada mbalimbali kurekebisha tatizo hilo,’ alisema.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ruaruke, Hemedi Mpullu pia alithibitisha
walimu hao kuitelekeza shule hiyo na kusema Mkuu wa Wilaya ya Rufiji,
Nurdin Babu ameagiza kufanyika kwa kikao cha dharura ili kupatikana
mwafaka kati ya walimu hao, wanafunzi na wazazi.
SOURCE:MWANANCHI