FILIKUNJOMBE AMUUMBUA DIWANI



 
 Mbunge  Filikunjombe (kushoto) akimchana  diwani  wa kata ya Madope Bw Mhagama (kulia) katikati ni mwenyekiti  wa CCM wilaya  Bw Kolimba  akisikiliza kwa umakini 
 Na Francis Godwin
KATIKA hali  isiyotegemewa mbunge  wa  jimbo la Ludewa  mkoani Njombe Deo Filikunjombe (CCM) amemkataa  mbele ya viongozi  wa  CCM na   wapiga  kura  diwani  wa kata ya Madope  jimbo la Ludewa kupitia chama cha mapinduzi (CCM) Godfrid Mhagama  kwa madai  kuwa ni  diwani anayeongoza  kwa  kumdanganya yeye kama mbunge pamoja na   wapiga  kura  wa kata  hiyo.

Mbunge  Filikunjombe  alisema  kuwa   diwani  huyo  amekuwa ni mmoja kati ya  watu  wanaoeneza  chuki ya ukabira katika kata  hiyo  kwa kuwabeza viongozi  wa  wilaya  na mbunge kutokana na kuwa  si wenyeji  wa kata  hiyo ni  watu kutoka ukanda  wa ziwani jambo ambalo ni hatari  kwa  maendeleo ya  kata  hiyo iwapo  siasa  za ukabira na ukanda  zitapewa nafasi.

Akizungumza katika mkutano maalum kijijini hapa mara  baada ya  kufunguza  ofisi ya  chama cha ushirika wa  kuweka na kukopa  ya  Farasa  Saccos  ,juzi Filikunjombe alisema  kuwa moja  kati  ya  kata  ambazo madiwani  wake  toka walipochaguliwa mwaka 2010 hawafanyi kazi ya kimaendeleo na badala yake  wamekuwa  wakieneza  chuki ya  kuwagawa  viongozi na  wananchi ni pamoja na kata  hiyo ya Madope ambapo  diwani amekuwa  akiendesha majungu mitaani na kuacha  kusimamia shughuli za kimaendeleo.

Alisema  kuwa  diwani huyo amekuwa ni kikwazo  kikubwa ndani ya CCM kutokana na  kushindwa  kusimamia  ujenzi  wa  shule ya Msingi Mangalanyena ,kushindwa  kusimamia ujenzi  wa Zahanati  katika kijiji  hicho pamoja na ujenzi  wa barabara na  kila anapoulizwa amekuwa akitoa majibu ya uongo mbele yake .

Mbunge  huyo alisema katika hali ya  kushangaza  diwani  huyo baada ya  kuulizwa  mkakati  wa kata katika  kusimamia  ujenzi wa Zanahati  ya kata  kijijini hapo alieleza  kuwa mkakati  wa  ujenzi huo na miradi  mingine  iliyosimama katika  kata  yake ya Madope  imeingizwa katika kipindi cha  fedha cha mwaka 2013 /2014 bajeti huku akitambua  kuwa huo ni uongo kwani bajeti ya mwaka wa  fedha wa 2013/2014 bado kupitishwa.

Hata  hivyo  alisema kupitia  diwani  huyo kata  hiyo  wamekuwa  wakiwachukia  viongozi  wa chama na  serikali ambao si wa  kabila la kwao huku  wakiendelea  kukwamisha miradi ya maendeleo katika kata  hiyo kama njia ya  kuwafanya  wananchi waungane nao katika  kuwachukia  viongozi  wa wilaya  hiyo .

“Nimechukizwa  sana na tabia ya mheshimiwa  diwani  wa kata  hii Bw Mhagama kwa  kushindwa  kufanya kazi za kimaendeleo badala yake anashinda  vijiweni  kuwaelewa  wananchi uongo  juu ya viongozi kuwa  si  wa ukanda  wao …..nasema diwani kama unataka kuendelea  kuendesha uongo na kushindwa  kufanya kazi yako ni vema ukakaa pembeni  ili  wananchi  waendelee kujiletea maendeleo….nchi  yetu na chama chetu hatuchaguani kwa  ukabila wala rangi  tunachangana kwa uwezo wa mtu na utendaji  sio hivyo unavyofanya  wewe”huku akishangiliwa na wananchi waliofika katika mkutano  huo

Filikunjombe aliwataka  wananchi  kutomsikiliza  diwani   huyo iwapo atashindwa  kubadilika na  kuendelea  kueneza  chuki katika kata  hiyo kati ya  viongozi  wa juu wa  wilaya na jimbo na  wananchi  wake .

Wakati kwa upande  wake  diwani Mhagama alipofuatwa na mwandishi  wa habari hizi  ili kujibu  tuhuma  hizo dhidi yake alisema kuwa  si kweli kama amekuwa akieneza siasa za ukabila katika kata  hiyo na kuwa wanaofanya  hivyo ni watu baki na sio yeye kama ambavyo mbunge amekuwa akimtuhumu .

Kuhusu  kukwama kwa miradi ya kimaendeleo katika kata yake ya Madope alisema  kuwa  kutokana na maelekezo ya mbunge  atahakikisha anakuwa mbele katika kusimamia miradi  hiyo na kuwa kwa upande  wake amekuwa akikwamishwa na  watendaji  wa Halmashauri ambao  wamekuwa  hawafiki  kufanya ukaguzi wa miradi katika kata  hiyo.

Katika hatu  nyingine  mbunge  Filikunjombe ameahidi  kusimamia ujenzi  wa zahanati  hiyo hadi ukakapokamilika ili  kuwawezesha  wananchi hao  wa kupata  huduma ya afya jirani  zaidi.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo