HOTUBA YA MHE. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NA MWENYEKITI WA CCM KWENYE UFUNGUZI WA MKUTANO MKUU WA NANE WA CHAMA CHA MAPINDUZI, UKUMBI WA KIZOTA – DODOMA, TAREHE 11 NOVEMBA, 2012

Utangulizi
 Mheshimiwa Dkt. Amani Abeid Karume, Makamu Mwenyekiti
    wa CCM na Rais Mstaafu wa Zanzibar;
Ndugu Pius Msekwa, Makamu Mwenykiti wa CCM wa Bara;
Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, Ndugu Benjamin William Mkapa;
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Waziri Mkuu;
Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ;
Viongozi Wakuu Wastaafu;
Katibu Mkuu wa CCM, Ndugu Wilson Mukama;
Ndugu  Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM;
Wageni wetu waalikwa kutoka vyama rafiki,
 Ndugu zetu wa Vyama vya Siasa Nchini;
Waheshimiwa Mabalozi,
Viongozi wa Dini,
 Wageni Waalikwa,
 Mabibi na Mabwana; 


Kama ilivyo ada, naomba tuanze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kukutana hapa Dodoma, siku ya leo, kwenye Mkutano Mkuu wa Nane wa Chama cha Mapinduzi.

Ndugu Wajumbe;        
Karibuni Dodoma.  Karibuni Mkutanoni.  Nawapeni pole kwa safari.  Tunamshukuru Mungu kwa kutuwezesha kufika salama na tuombe turejee makwetu salama. Kwa niaba yenu, niruhusuni niwashukuru wenyeji wetu, yaani wana-CCM na wananchi wote wa Dodoma, wakiongozwa na Alhaji Adam Kimbisa, Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Dodoma na Mkuu wa Mkoa Dkt. Rehema Nchimbi, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa.  Tunawashukuru kwa kutupokea vizuri na kwa ukarimu wao unaotufanya tujisikie tuko nyumbani katika huu mji ambao ndiyo Makao Makuu ya nchi yetu na Chama chetu.
Ndugu Wajumbe;
Napenda kuchukua nafasi hii kutoa pongezi nyingi kwa Halmashauri Kuu ya Taifa kwa matayarisho mazuri ya Mkutano huu wa Nane wa Taifa wa CCM.  Natoa pongezi maalum kwa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa chini ya uongozi mahiri wa Katibu Mkuu Ndugu Wilson Mukama na Kamati  zote za Maandalizi ya Mkutano kwa kazi kubwa na nzuri waliyofanya ya kuwezesha Mkutano huu kufanyika.  Kwenu nyote nasema hongereni na asanteni sana.
Ndugu Wajumbe;

Karibuni tena Kizota.  Nasikitika kwamba matumaini yangu ya kufanya Mkutano Mkuu katika ukumbi wetu wenyewe hayakutimia.  Hii ni kwa sababu kazi ya matayarisho imechukua muda mrefu kuliko nilivyotazamia.  Tumechelewa kupata kiwanja kilichokidhi mahitaji yetu na matazamio yetu.  Kwanza tulipata kiwanja nyuma ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).  Lakini tukaona ni mbali mno na walipo wananchi.  Tukaja kupata kiwanja kingine juu ya Kilimani Club ambacho hakikuwa kikubwa cha kutosha.  Mapema mwaka huu ndipo tulipopata kiwanja eneo la Makulu  ambacho kinakidhi sifa za kuwa kikubwa cha kutosha na kuwa karibu na katikati ya mji wa Dodoma.  Tumekiafiki  na matayarisho ya kuanza ujenzi yamekamilika.  Leo asubuhi tumeweka jiwe la msingi kuzindua ujenzi wa Ukumbi wa Mkutano (Dodoma Convention Centre).  Baadae utafuta ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya CCM na jengo la Hoteli ya Kisasa.

Wageni Karibuni
Ndugu Wajumbe;        
Kama mjuavyo Chama cha Mapinduzi kina marafiki wengi Afrika na kwingineko duniani.  Tumekuwa na mazoea ya kualikana katika mikutano mikuu yetu.  Safari hii tumefanya hivyo tena.  Kwa niaba yenu niruhusuni niwashukuru sana wageni wetu wote wa kutoka vyama rafiki Afrika na duniani kwa kukubali mwaliko wetu na kuja kujumuika nasi siku ya leo. Kuwepo kwao ni kielelezo tosha cha udugu na urafiki uliopo baina ya vyama vyetu na nchi zetu ambao hatuna budi kuudumisha, kuuendeleza na kuukuza.    Hali kadhalika, nawashukuru Mabalozi wa Nchi za Nje na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa walioweza kuja kushiriki nasi katika sherehe za ufunguzi wa Mkutano wetu.

Ndugu Wajumbe;
Tunawakaribisha kwa furaha na upendo mkubwa viongozi na wawakilishi wa vyama vya siasa vya hapa nchini kwa kukubali mwaliko wetu na kuja kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM  siku ya leo.  Tunawashukuru kwa moyo wao wa uungwana kwani tofauti za vyama si uadui.  Wamethibitisha jinsi demokrasia ya vyama vingi inavyozidi kustawi na kukomaa hapa nchini.
Nawashukuru sana pia, viongozi wetu wa dini na wananchi mbalimbali waliojumuika nasi.  Kuwepo kwao ni jambo la faraja kubwa.  Dua za viongozi wa dini zitasaidia kuponya na kuupa baraka mkutano wetu uende salama, uwe wa mafanikio  na kuwafanya wale wote wasiokiombea mema Chama chetu watahayari na kufadhaika.
Karibuni Diaspora
Ndugu Wajumbe;
          Napenda kuwatambua na kuwakaribisha viongozi na wananchama wa Chama chetu waliopo nje, Marekani, Italia, India na Uingereza. Ndugu zetu hawa kwa upenzi wao kwa Chama wamesafiri masafa marefu kuja kushiriki nasi.  Hawa wanastahili pongezi maalum kwa jinsi wanavyopeperusha bendera ya CCM na kueneza sera zake. Naomba tuwape makofi ya nguvu.

Agenda ya Mkutano
Ndugu Wajumbe;
Agenda ya Mkutano Mkuu wa Taifa wa Nane wa Chama cha Mapinduzi ina mambo makuu manne.  Kwanza kufanya marekebisho ya Katiba ya Chama cha Mapinduzi.  Mengi ya marekebisho hayo yanatokana na uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Taifa katika kikao chake cha trehe 11 – 12 Aprili 2011 wa kufanya mageuzi ndani ya Chama.  Miongoni mwa matunda ya mageuzi hayo ni kuundwa kwa Baraza la Ushauri na Wajumbe wa NEC kuchaguliwa Wilayani badala ya Mikoani.
Kwa mujibu wa Katiba ya CCM, Halmashauri Kuu ya Taifa ina mamlaka ya kufanya marekebisho ya Katiba na marekebisho hayo kutumika.  Hata hivyo, marekebisho hayo hayana budi kuletwa katika Mkutano Mkuu wa Taifa ili yaingizwe rasmi kwenye Katiba.

Ndugu Wajumbe;
Jambo la pili litakuwa ni kwa Serikali zetu mbili kutoa taarifa za maendeleo ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya 2010 – 2015 tangu baada ya uchaguzi mkuu hadi sasa.  Vile vile, tutapokea Taarifa ya Halmashauri Kuu ya Chama kuhusu kazi za Chama kwa miaka mitano iliyopita.  Jambo la nne na la mwisho ni kufanya uchaguzi wa Mwenyekiti, Makamu wake wawili na Wajumbe wa NEC wa Kundi la Zanzibar na Tanzania Bara.

Ndugu Wajumbe;
Tofauti na mikutano iliyopita, Halmashauri Kuu ya Taifa inapendekeza kuwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wajigawe katika makundi matano kujadili taarifa ya kazi za Chama na zile za utekelezaji wa Ilani.  Kisha kila kikundi kitatoa taarifa ya maoni na mapendekezo yake.  NEC ilifikiria iwe hivyo ili kutoa muda wa kutosha kwa wajumbe kujadili taarifa hizo muhimu katika utaratibu wa zamani wa mtu mmoja kila mkoa kuitwa kusoma, wajumbe hawapati fursa ya kutosha ya kuzijadili taarifa zinazotolewa.

Kuimarisha Chama Kazi Endelevu
Ndugu Wajumbe;
Katika hotuba yangu ya kushukuru baada ya kuchaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi kwenye Mkutano Mkuu wa Taifa Maalum wa tarehe 25 Juni, 2006, pamoja na kuzungumzia mambo mengine, nilisisitiza umuhimu wa kuimarisha Chama chetu.  Nilitoa maoni yangu kwa upana kiasi kuhusu mambo ya kuzingatia.  Leo tena, katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu huu narudia kusisitiza jambo hili.  Nafanya hivyo kwa sababu hilo ndiyo jukumu la kudumu na jukumu la kwanza na la msingi kwa kila kiongozi na kila mwanachamawa CCM.  Isitoshe, kwa hali ilivyo sasa, kuimarisha Chama cha Mapinduzi lazima iwe agenda kuu ya kila mmoja wetu.  Ni ukweli ulio wazi kuwa ustawi na uhai wa Chama unategemea viongozi na wanachama kufanya kazi ya ziada kuimarisha Chama chao.


Ndugu Wajumbe;
Bahati nzuri, chini ya uongozi wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Ndugu Lt. Yusuf Rajab Makamba tarehe 19 Desemba, 2006 ulianzishwa Mradi wa Kuimarisha Chama.  Mradi huo ndiyo uliokuwa dira na mwongozo wetu wa kufanya kazi za Chama tangu wakati huo mpaka leo.  Wajibu wa kila kiongozi na kila mwanachama na kila kikao cha kila ngazi vimeainishwa vizuri.  Pia, uliwekwa utaratibu mzuri wa kufuatilia utekelezaji wake. Bila ya shaka mtakumbuka kuwa utaratibu maalum uliwekwa wa kutoa tuzo kwa Mikoa iliyofanya vizuri katika utekelezaji wa vipengele mbalimbali vya uimarishaji wa Chama kwa mujibu wa Mradi huo.

Ndugu Wajumbe;
Kazi ya kuimarisha Chama chetu ni jukumu endelevu kwa kila mwanachama wa CCM, kila kiongozi wa CCM na kila mtumishi wa CCM.  Kwa sababu hiyo, Mradi wa Kuimarisha Chama ni mchakato usiokuwa na ukomo.  Ni kazi ya kudumu na wala siyo tukio lililoanzishwa na Katibu Mkuu Lt. Yusufu Rajabu Makamba na kukoma siku alipostaafu.

Tuongeze Wanachama
          Kazi ya kuingiza wanachama wapya ni ya kudumu katika uhai wa Chama cha Mapinduzi.  Hii siyo kazi ya msimu wa uchaguzi wa ndani ya Chama au wakati wa kura za maoni na hivyo kugeuzwa kuwa ni kwa ajili ya kuwapigia debe watu wanaotafuta vyeo.  Lazima wakati wote tuwe tunaingiza wanachama wapya lakini pia lazima tuzingatie utaratibu ulioelekezwa na Katiba ya CCM.  Hatuna budi kuhakikisha kuwa tuna wanachama walio waumini wa kweli na wapenzi wa dhati wa CCM, itikadi yake na sera zake na zile za Serikali zake.

Ndugu Wajumbe;
Wanachama ndiyo nguvu kuu ya uhai na ushindi wa CCM.   Lazima Chama chetu kiwe na Jeshi kubwa la wanachama walio tayari kukijenga, kukisemea na kukipigania.  Kuwa na Wanachama wengi ambao ni waumini wa kweli wa Chama chetu ina maana ya kuwa na kura nyingi za msingi za kuanzia katika uchaguzi wa dola.  Pia wanachama ni nyenzo muhimu ya CCM kupata kuungwa mkono na wananchi hasa pale ambapo wanachama wataifanya ipasavyo kazi ya Chama ndani ya umma.  Kila mwanachama akifanya kwa mafanikio kazi ya kushawishi wananchi kupigia kura wagombea wagombea wa CCM tutapata kura nyingi za uhakika.

Tuwe na Viongozi Wazuri
Ndugu Wajumbe;
Kazi ya kuhakikisha kuwa Chama cha Mapinduzi kina viongozi wazuri ni ya kudumu na wala siyo ya msimu wa kuchuja majina ya wagombea.  Lazima Chama chetu kiwe na viongozi ambao ni waumini wa dhati wa itikadi yetu na wanaozijua vyema sera za Chama cha Mapinduzi na Serikali zake.  Wao ndio wanaotarajiwa kuonesha njia kwa kuelimisha wanachama na wananchi.  Viongozi wa CCM lazima wawe hodari wa kufafanua sera na masuala mbalimbali yahusuyo Chama chetu na Serikali zake.  Hawataweza kufanya hivyo kama wao wenyewe ni maamuma.  Kiongozi mzuri wa Chama cha Mapinduzi ni yule ambaye ni jasiri kukitetea Chama cha Mapinduzi na kama hapana budi yuko tayari kujitolea muhanga.  Kuwa na kiongozi ambaye haguswi wala kusikitishwa na hali mbaya ndani ya Chama au hujuma dhidi ya Chama ni sawa na kutokuwa na kiongozi.  Bora asiwepo.  Na kuwa na kiongozi ambaye yeye mwenyewe anafanya vitendo viovu dhidi ya CCM na Serikali zake ni kuwa na nyoka ndani ya nyumba.  Ni jambo hatari lisilokubalika na halistahili kuvumilika.  Tukiwajua tuwaseme, tuwashughulikie, wachague wanapotaka kwenda.


Ndugu Wajumbe;
Kiongozi mzuri wa CCM lazima awe muaminifu na muadilifu na lazima wanachama na jamii imuone hivyo.  Chama chetu kinashindania kushinda akili na mioyo ya Watanzania na hiyo ndiyo kazi tunayomtarajia kiongozi wetu afanye katika jamii.  Hii ndiyo hasa kazi ya Chama ndani ya umma.  Lakini, ili kiongozi wetu aweze kuifanya kwa mafanikio taswira yake mbele ya jamii ni kitu muhimu.  Awe na taswira nzuri mbele ya wananchi.  Kama jamii inamuona kuwa si mtu muadilifu itakuwa taabu sana kwake kufanikisha jukumu la msingi la Chama chetu.  Hivyo ndugu zangu, lazima tuhakikishe kuwa viongozi wetu wanakuwa waadilifu ili wasigeuke kuwa balaa na hasara kwa Chama.

Ndugu Wajumbe;
Baada ya kukamilisha mchakato wa uchaguzi ngazi ya taifa, tutatengeneza na kutekeleza programu maalum ya kutoa mafunzo kwa viongozi wa Chama kuanzia ngazi ya Tawi hadi Taifa.  Hali kadhalika, tutaendeleza na kukamilisha kazi ya ukarabati na upanuzi wa Chuo cha Ihemi ili kiwe kitovu cha kutoa mafunzo ya siasa kwa makada na viongozi wa Chama na Jumuiya zake kama ilivyokuwa inafanywa katika Chuo cha CCM cha  Kivukoni na vyuo vyake vya kanda.

Ndugu Wajumbe;
Bahati nzuri vyama vya ukombozi vya nchi za Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika vimekubaliana kuwa Chuo cha Ihemi kiwe Chuo cha Mafunzo ya siasa kwa makada wa vyama vyao pia.  Ni heshima kubwa kwa CCM, lakini pia inakipa Chama chetu wajibu mkubwa wa kuhakikisha kuwa Chuo hicho kinawekwa katika viwango vya kimataifa.  Tuko tayari na tutajipanga ipasavyo kutimiza wajibu wetu huo wa kihistoria.

Vikao Vifanyike Ipasavyo
Ndugu Wajumbe;
Ni kazi endelevu kwetu sote, wanachama na viongozi, kuhakikisha kuwa vikao vinafanyika kwa wakati na kwamba mikutano inaendeshwa vizuri na ina agenda zenye maslahi ya kujenga Chama na kuendesha nchi.  Pia, ni muhimu kuhakikisha kuwa kinachoamuliwa kinatekelezwa ipasavyo.  Naamini kwamba mafunzo tutakayotoa kwa viongozi na watendaji wa Chama kuhusu wajibu wao na jinsi ya kuutekeleza yatasaidia sana kuimarisha CCM.

Watendaji Mahiri
Ndugu Wajumbe;
Kwa Chama chetu kuwa na watendaji wazuri ni jambo lisilokuwa na mjadala.  Lazima tuwe na watendaji ambao ni makada wazuri na watu mahiri kwa kazi zao.  Wawe ni watu ambao wana uelewa mzuri wa sera za Chama na kwamba wanaweza kuzifafanua, kuzieneza na kuzitetea.  Pia, wawe ni watu wanaojua vyema kazi yao ya utendaji, kwa mujibu wa shughuli zao wanazozifanya.  Ni vyema kwa kazi za kitaalamu tukapata watu wataalamu wa kazi hizo.  Ni muhimu sana tukayazingatia haya kwani utendaji mzuri katika Chama ni nguvu muhimu sana ya kukifanya Chama chetu kuwa imara.  Chama chetu kiwe na mipango thabiti ya kuwaendeleza watumishi wake na kama hapana budi kuwadhamini wakasome. Tufanye hivyo.
Bila ya shaka mtakumbuka kuwa tarehe 3 Novemba, 2007, pale Kizota, niliahidi kuwa tutaboresha maslahi ya watumishi wa Chama.  Tumetimiza ahadi hiyo.  Leo nasema kuwa tutajitahidi kuendelea kuboresha maslahi ya watumishi wetu kadri uwezo utakavyoruhusu.



JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright 2025 EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo