UJENZI WA VYOO SHULE YA MSINGI MALEUTSI WILAYANI MAKETE WAENDELEA VIZURI


Na mwanahabari Furahisha Nundu,MAKETE

Wananchi wa kijiji cha Maleutsi wilayani Makete wametoa ushirikiano mzuri wa kifedha kwa ajili ya ujenzi wa choo cha shule ya msingi Maleutsi kijijini hapo.

Akizungumza na mwandishi wa mtandao huu wa eddymoblaze ofisini kwake Afisa mtendaji wa kijiji hicho Bw.Michael Sanga amesema kwamba ujenzi wa choo hicho umeanza mwezi huu ambapo shimo moja kubwa limeshakamilika na wanatarajia kuanza uchimbaji wa shimo dogo shuleni hapo.

Bw.Sanga ameongeza kuwa wananchi wametoa michango yao ambapo kila mmoja amekuwa akichangia shilingi elfu kumi ikiwa shimo hilo limegharimu kiasi cha shilingi milioni tatu ambapo mpaka kukamilika ili kianze kutumiwa na wanafunzi choo hicho kitagharimu zaidi ya shilingi milioni tisa.

“Ndugu mwandishi wa eddymoblaze kimsingi mambo ya ujenzi yanakwenda vizuri ukizingatia hii ni huduma muhimu kwa wanafunzi shuleni hapa, nashukuru wananchi wanatoa michango yao kwa wakati na ndio maana ujenzi huu unafanikiwa” alisema Bw. Sanga

Katika hatua nyingine Bw. Sanga amesema fedha zitakazomalizia ujenzi wa choo hicho wanatarajia kuuza msitu wa shule hiyo ili kukamilisha sehemu iliyobaki kwa ajili ya kuanza kutumika mwezi  January 2013 na choo hicho kitatumia maji ambayo yataingizwa muda mfupi ujao kuanzia sasa.

“Uzuri ni kwamba shule hii ina vitegauchumi vingi na kimojawapo ni msitu, hivyo tunatarajia kuuza msitu wa shule na fedha zitakazopatikana tutazitumia kumallizia choo hicho, na nakushukuru sana mwandishi wa eddymoblaze.blogspot.com kwa kufika kijijini kwetu kunihoji kuhusu ujenzi huu kwa kweli tunafarijika sana ukizingatia kijiji hiki kilivyo mbali na mjini” alisema

Hata hivyo amewashukuru wananchi wa kijiji hicho kwa kutoa ushirikiano mzuri baina yao wakati wa uchangishji wa mchango wa choo hicho ambapo watatimiza ndoto zao mapema  kama ilivyotarajiwa tokea hapo awali.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo