HALI
ya
afya ya msanii mkongwe nchini, Fatuma Bint Baraka, maarufu Bi Kidude ni
mbaya na akiwa amehamishwa kutoka Zanzibar hadi katika hospitali ya
Hindu
Mandali Dar es Salaam na jana watu walikuwa wanazuiwa kwenda kumuona.
Bi
Kidude
alianza kusumbuliwa na maradhi mwezi uliopita, lakini baadaye akapata
ahueni na kufanya mahojiano hadi na vyombo vya habari, lakini ghafla
mambo
yamebadilika tena na amerudi hospitali.
Bi
Kidude
ni gwiji wa muziki katika Bara la Afrika, katika fani ya muziki wa
mwambao ambao hujulikana kwa jina la Taarabu. Muziki huu ambao ni
mchanganyiko
wa muziki toka nchi za Kiarabu na vionjo vya muziki wa Kiafrika umekita
sana
katika mwambao wa Afrika Mashariki yaani Zanzibar, Mombasa, Lamu na
kwingineko.
Fatuma
binti
Baraka au Bi Kidude, alizaliwa katika kijiji cha Mfagimarigo Zanzibar
katika familia ya watoto saba (7). Baba yake Mzee Baraka alikuwa ni
mfanyabiashara wa nazi, zao ambalo ni la kutumainiwa sana Zanzibar.
Bi
Kidude
anasema hafahamu tarehe halisi aliyozaliwa, isipokuwa anachojua ni
kwamba alizaliwa wakati rupia ikitumika kama fedha, na vilevile ana
hakika ni
kabla ya Vita Kuu ya Kwanza ya Ulaya.
Wataalamu
wa
mahesabu baada ya kupata taarifa hizo wakampigia mahesabu na kumkabidhi
miaka yake kwamba ni zaidi ya miaka 90.
Bi
Kidude
anasema uimbaji aliuanza tangu alipokuwa na umri wa miaka 10 na
alijifunza kutoka kwa msanii mkongwe na aliyetamba sana enzi hizo Sitti
Binti
Saad. Anasema wageni wengi kutoka sehemu mbalimbali walikuwa wakifika
Zanzibar
kuja kumwona Sitti, na kwa vile Bi Kidude na Sitti walikuwa wako karibu
basi
yeye alikuwa akiwapeleka wageni wale nyumbani kwa Bi Sitti, wakifika
huko
wageni walikuwa wakiingia ndani na yeye kubakia nje, kule ndani Bi Sitti
alikuwa akiwaimbia wale wageni, na yeye huku nje alikuwa akimsikiliza
kwa
makini na kumfuatiza jinsi alivyokuwa akiimba. Aliendelea hivyo hadi
akawa
mahiri sana katika uimbaji.
Alipokuwa
na
miaka 13, kwa mara ya kwanza alitoroka nyumbani kwao Zanzibar na
kukimbilia
Tanzania Bara, baada ya kulazimishwa kuolewa. Lakini alipokuwa kigoli wa
kutosha kuolewa aliolewa ingawa ndoa hiyo nayo haikudumu kutokana na
manyanyaso
aliyokuwa akiyapata, hivyo aliamua kukimbilia kaskazini mwa Misri ikiwa
ni
katika miaka ya 1930, huko aling'ara sana katika fani yake ya uimbaji na
uchezaji ngoma. Lakini ilipofika miaka ya 1940 aliamua kurudi nyumbani
Zanzibar
ambako aliendelea na shughuli zake uimbaji.
Bi
Kidude
hategemei kazi moja tu ya kuimba, kwani pia ni mfanyabiashara ya
'wanja'
na 'hina' ambavyo anavitengeneza yeye mwenyewe, pia ni mtaalamu wa
matibabu kwa
dawa za mitishamba na zaidi ya hayo ni mwalimu mzuri sana wa 'Unyago' na
ameanzisha chuo chake mwenyewe na anasema katika wanafunzi wake wote
hakuna
aliyepata talaka kutoka kwa mumewe.
Watu
wanasema
'Utu uzima dawa' Bi Kidude ana upeo mkubwa sana wa akili kwani pamoja
na kukulia katika mazingira yaliyogubikwa na tamaduni za kiarabu ambapo
mwanamke anatakiwa wakati wote akiwa hadharani ajifunike, Bi Kidude
aliliona
hili katika upeo mwingine kwamba ni sheria tu ya kitamaduni toka
Uarabuni,
hivyo aliamua kuvunja sheria hiyo na kuondoa hijabu mwilini mwake, na
sasa hivi
anavaa kama Mtanzania na si kama Mwarabu.
Lakini hakubakia hapo alivunja
na
miiko mingine zaidi ya kutokunywa na kuvuta, kwani Bi Kidude anakunywa
pombe na
kuvuta sigara jambo ambalo si kawaida kwa wanawake Zanzibar.
Bi
Kidude
amekwisha tembelea nchi nyingi sana ikiwa ni pamoja na Oman, Ufaransa,
Hispania, Ufini, Ujerumani na Uingereza.
Amekwisha
pata
tuzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ile ya Tamasha la Filamu la Nchi za
Jahazi (ZIFF) mwaka 1999 tuzo ni ya maisha. Pia mwaka jana tuzo ya WOMAX
ilienda kwake.
Nyimbo
alizowahi
kuimba ni pamoja na Muhogo wa jang'ombe, na anaimba kwa Kiswahili na
Kiarabu. Hakuwahi kupata elimu nyingine zaidi ya Kurani.
Mtandao huu unalaani vitendo vya watu kuanazisha habari wasizo na uhakika nazo, kwani bi Kidude kazushiwa kuwa amefariki dunia
