Waziri wa
Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe.
DAR ES SALAAM,
WAZIRI wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amemsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Ephraim Mgawe na viongozi wengine watatu kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali bandarini hapo.
Wengine waliosimamishwa kazi ni Wasaidizi wake wawili pamoja na
Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam.
Waziri Mwakyembe alitoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam
alipozungumza na waandishi wa habari baada ya juzi kuwa na kikao cha
dharura na viongozi wa mamlaka hiyo.
Alisema
kutokana na upungufu waliobaini wameona ni vema viongozi hao wakakaa
pembeni na kwamba ameunda kamati ya watu saba watakaochunguza masuala
hayo.
Hatua hiyo kusimamishwa kazi kwa viongozi hao ni mwendelezo wa
mikakati ya waziri huyo kusafisha uozo katika taasisi mbalimbali kwani
hivi karibuni kumsimamisha kazi Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Ndege
Tanzania (ATCL), Paul Chizi na wakurugenzi wanne kutokana na ukiukwaji
wa sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma, ambao umetishia uhai
wa shirika hilo.
Akizungumza, Mwakyembe alisema nafasi ya Kaimu Mkurugenzi
Mkuu wa TPA inashikiliwa na Mhandisi Madeni Kipande kutoka Wizara ya
Ujenzi na kwa nafasi nyingine akasema wawekwe watu wenye uadilifu.
“Nimeamua kumchukua mtu nje ya bandari kukaini nafasi ya
Mkurugenzi Mkuu ili kuondoa wasiwasi, maana angetoka ndani angeshindwa
hata kuingia ofisi.
“Najua uamuzi huu utahojiwa, lakini tuendelee kuzumiliana, kwani
ukweli haupingwi,” alieleza.
Pamoja na hatua hiyo, alisema ameunda kamati ya watu saba
kuchunguza tuhuma mbalimbali bandarini hapo.
“Wajumbe wa kamati hiyo sitawataja majina, kwa sababu tuna deal
na watu wenye hela…hadidu rejea itakiwa na maswali 50,” alisema.
Mbali na kuwasimamisha kazi watumishi hao, pia alisema ameiagiza
bodi ya mamlaka hiyo kuwasimaisha kazi watumishi wa kituo cha kupokea mafuta cha Kurasini (KOJ) ambao ni Meneja,
Meneja wa Jet na Injinia wa mafuta wa kituo hicho.