SENSA HUENDA IKASUASUA BABATI


Imesemekana kuwa zoezi  la Sensa katika Wilaya ya Babati na halmashauri ya mji wa Babati mkoa wa Manyara,huenda likashindwa kufanikiwa kutokana na baadhi ya vifaa kupungua ama kuisha wakati zoezi hilo likiwa linaendelea.
Taarifa hiyo imetolewa na  Mratibu wa sensa wa Halmashauri ya mji wa Babati,Bw.John Malle katika kikao cha  wajumbe wa kamati ya Sensa ya wilaya  kilichofanyika  jana katika Ofisi ya Mkuu wa wilaya  ya Babati mkoani Manyara.
 Alibainisha  kuwa kwa upande wake vitendea kazi vimekuwa vichache ikiwemo dodoso refu kwani mpaka kufikia Agosti 27 yalikuwa yamekwisha.
Alisema kuwa kama vifaa hivyo havitoweza kupatika kwa haraka itafika wakati zoezi hilo likasimama kwa muda  hadi vifaa hivyo vitakapoingia na  muda waliopewa wa zoezi la sensa ni siku saba tu na hadi kufikia agosti 28 ni  siku ya tatu vifaa hivyo vimeisha.
Aidha aliongeza   kuwa kumekuwepo kwa changamoto mbalimbali ikiwemo baadhi ya makarani kudai kutaka kuongezewa posho kwani posho walizopewa hazilindani na kazi wanazozifanya  zimekuwa ngumu hali inayowapelekea kufanya kazi hadi usiku.
Pia alisema kuwa kufuatia hayo alidai kuwa amefuatilia hadi kwa mratibu wa sensa mkoa huo, Bwana Juma Shabani ambapo alidai kuwa vifaa hivyo vipo njiani na vitawasili wakati wowote,hata hivyo alimuomba Mkuu wa Wilaya ya Babati,Bw,Khalidi Mandia kufuatilia ili wahusika waweze kuharakisha kufika kwa vifaa hivyo.
Kwa upande wake  Mratibu Msaidizi wa Sensa wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati,Bw.Selemani Shanti alibainisha  kuwa huenda siku saba walizopewa kwa ajili ya zoezi hilo likaisha bila ya kufanikiwa kwani tatizo lililojitokeza kwa Halmashauri ya mji ndilo lililopo katika Halamashauri yake.
Alieleza kuwa  licha kuwepo kwa upungufu wa madodoso,pia kumekuwepo na changamoto ya watendaji wa kata na vijiji kujichukulia mamlaka yao wenyewe ya kuwateua watu wanaowafahamu kwa ajili ya kuwaongoza makarani kwenye kaya kwa lengo la kupata posho huku wakiwasahau wenyeviti wa vitongoji ambao ndio wanaofahamika.
Naye  Mkuu wa Wilaya ya Babati Khalidi Mandia ambaye ndiyo mwenyekiti wa Kamati ya Sensa  amewataka  waratibu hao kuhakikisha wanafuatilia kwa haraka vitendea kazi vilivyopungua ili kuepushia gharama zingine Serikali kwa siku zitakazoongezwa.Hata hivyo alisema licha ya kuwepo kwa changamoto hizo lakini hakuna tatizo lolote lililojitokeza la watu kugoma kuhesabiwa kama ilivyo kwa mikoa mingine na wilaya zake


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo