Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Makete wametakiwa kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa zoezi la sensa ya watu na Makazi wilayani hapo linalotarajiwa kufanyika usiku wa kuamkia Agosti 26 mwaka huu
Akifungua
mafunzo yahusuyo sensa kwa madiwani wa halmashauri hiyo mwishoni mwa wiki,
mgeni rasmi katika mafunzo hayo Mkuu wa wilaya ya Makete Josephine Matiro
amesema madiwani hao wana nafasi kubwa ya kuisaidia serikali kukamilisha zoezi hilo kwa kuwaelimisha
wananchi waliopo kwenye kata zao
Pia
Matiro ameongeza kuwa zoezi la sensa ya watu na makazi halitaathiri shughuli za
wananchi za kujipatia kipato hivyo kuwataka madiwani hao kwenda kuwaelimisha
wananchi kuhusiana na umuhimu wa zoezi hilo
“Waheshimiwa
madiwani serikali inatambua nguvu mliyonayo kwa wananchi mnao waongoza,
tunategemea ushirikiano wenu pindi mnapokutana na wananchi huko, tafadhalini sana mtusaidie
kuielimisha jamii kuhusu suala la sensa ya watu na makazi itakayofanyika siku
chache zijazo” alisema Matiro
Kwa
upande wake mkufunzi wa mafunzo hayo Geofrey Masaki amesema serikali imelipa
kipaumbele zoezi la sensa ya watu na makazi na ndio maana imeweza kutoa mafunzo
kwa makarani wote watakao husika na utekelezaji wa zoezi hilo , na hata kwa wadau mbalimbali wakiwemo
madiwani
Amesema
wasisite kuielimisha jamii kushiriki katika zoezi hilo , na kutaka zoezi la sensa kutohusishwa
kisiasa
Akizungumza
mara baada ya kupatiwa mafunzo hayo diwani wa kata ya Iniho ambaye pia ni
makamu mwenyekiti wa halamshauri ya wilaya ya Makete Mh. Jison Mbalizi, amesema
anaamini yeye pamoja na madiwani wenzake wataielimisha jamii kuhusu umuhimu wa
sensa na pia hawatarajii kuhusisha suala la sensa na siasa kama inavyodhaniwa
na watu wengi
Pia
alitumia nafasi hiyo kuwataka wananchi kuondokana na dhana potofu kuwa sensa
haina umuhimu wowote na kuwataka wananchi hao kushiriki bila woga
Sensa
ya watu na makazi itafanyika usiku wa Agosti 25 kuamkia Agosti 26 ikiwa na
kauli mbiu isemayo sensa kwa maendeleo jiandae kuhesabiwa
