TARIME
WAZEE wa mila
kutoka katika koo 13 za kabila la wakurya, wilayani Tarime mkoani Mara,wameanza
mazungumzo na viongozi wa kanisa la Anglikana Tanzania dayosisi ya Tarime ya
kusaka amani ya kudumu.
Wazee hao pia wameahidi
kusaidiana na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Tarime na Rorya katika kudhibiti
vitendo vya uhalifu na uhalifu katika wilaya hiyo.
Wazee hao
wameyasema hayo katika kongamano ambalo limeitishwa na Askofu wa Kanisa la
Anglikana Dayosisi ya Tarime Dk. Mwita Akiri kwenye Kituo cha Maendeleo ya
Kilimo Mogabiri, wilayani humo limehudhuriwa pia na Kamanda wa Polisi mkoa wa
Kipolisi wa Tarime/ Rorya, Kamishna Msaidizi Justus Kamugisha.
Aidha wazee hao
wa mila pamoja na wachungaji wa kanisa hilo la Anglikana, wameahidi kutoa
ushirikiano utakaosaidia kudumisha amani na usalama katika kukabiliana na
uhalifu.
Akifungua
kongamano hilo, Askofu Dk. Mwita amewasisitizia wazee hao wa mila kuhakikisha
wanasimamia haki, ambayo itazaa amani na hatimaye kuleta maendeleo badala ya
wao kuwa chanzo cha kuchochea migogoro na uhasama dhidi ya koo nyingine.
Kwa upande wake,
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Tarime na Rorya ACP Justus Kamugisha,
amesema jeshi lake limekuwa likishirikiana na wazee wa mila katika kurejesha
amani wilayani humo, kwa kudhibiti mapigano ya koo na koo, wizi wa mifugo
ulioambatana na mauaji pamoja na kilimo cha bangi.