Ndugu Wananchi,
Kama ilivyo ada naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa
Rehma, kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kumaliza nusu ya kwanza ya
mwaka 2012 salama. Kwa kutumia utaratibu wetu wa kuzungumza nanyi kila
mwisho wa mwezi, leo napenda kuzungumzia mambo mawili. Jambo la kwanza
ni suala la usafirishaji haramu wa binadamu nchini na la pili ni la
mgomo wa madaktari.
Usafirishaji
Haramu wa Binadamu Nchini
Ndugu Wananchi;
Bila ya shaka mtakuwa mmezisikia taarifa za tukio
la kushtusha na kuhuzunisha la kukutwa maiti 43 za watu
wasiojulikana, zilizotupwa katika kichaka kilichopo kijiji cha Chitego,
Wilayani Kongwa, Mkoa wa Dodoma tarehe 26 Juni, 2012. Pamoja na maiti
hao, walipatikana watu 84wakiwa hai lakini wote wakiwa
wamedhoofu na baadhi yao wakiwa mahututi. Hatua za haraka zilichukuliwa
kuwasafirisha watu hao hadi Dodoma ambapo wale waliokuwa mahututi
walifikishwa Hospitali Kuu ya Mkoa wa Dodoma kwa matibabu na wengine
walihifadhiwa katika Kituo cha Kati cha Polisi, Dodoma. Maiti
22 zilipelekwa Dodoma na 21 zilipelekwa
Morogoro kuhifadhiwa.
Taarifa zilizopatikana kutoka kwa wale walionusurika zimebainisha
kuwa watu hao ni raia wa Ethiopia ambao walikuwa safarini kwenda Malawi
na baadaye Afrika ya Kusini ambako wangetengenezewa utaratibu wa kwenda
kuishi Marekani na Ulaya. Kwa mujibu wa maelezo yao, safari yao ilianza
miezi mitano iliyopita. Mwezi mmoja waliutumia Ethiopia na miezi minne
waliitumia Kenya kabla ya kuletwa Arusha ambako walipakiwa kwenye lori
na kuanza safari ya kuelekea Malawi lakini ikaishia Chitego. Lori
walilopanda lilikuwa limezibwa kabisa na hivyo kusababisha vifo kwa
kukosa hewa.
Tukio la Chitego, Dodoma la wahamiaji haramu kukamatwa na wengine
kukutwa wamekufa si la kwanza kutokea hapa nchini. Kwa jumla, katika
kipindi cha takriban miaka 10 sasa kumekuwepo na tatizo kubwa la
wahamiaji haramu kuingia nchini. Kwa mfano, kati ya mwaka 2005 na hivi
sasa jumla ya wahamiaji haramu 19,683wamekamatwa.
Karibu wote wameshaondoshwa nchini na hivi sasa wapo karibu watu 1,500 tu
magerezani wanaotumikia adhabu na kusubiri kurejeshwa makwao. Wengi wa
watu hao wanatoka Ethiopia na Somalia na baadhi kutoka Pakistan na
Bangladesh.
Wahamiaji haramu wamekuwa wanaingia nchini kwa kupitia njia zisizo
rasmi. Wapo wanaotumia nchi kavu hasa kupitia mikoa ya Mara, Arusha,
Kilimanjaro na Tanga. Na, wapo wanaopitia baharini kwa kutumia fukwe za
Pemba, Unguja na za mikoa ya ukanda wa Pwani ya Tanzania Bara yaani
Tanga, Pwani, Lindi na Mtwara.
Ndugu Wananchi;
Kwa mujibu wa kauli zao, watu hao wamekuwa wanaeleza kuwa hawaji
nchini kuhamia bali wao ni wapita njia tu. Wanaelekea Afrika ya Kusini
ambako wameahidiwa kuwa watatengenezewa mipango ya kuhamia Marekani na
Ulaya. Watu hao pia wamethibitisha kuwepo kwa watu maalum
wanaojihusisha na usafiri wao tangu nchi watokako na zote wanazopitia
mpaka kule waendako. Aidha, wamesema kuwa wao wanawalipa watu hao ili
wawasafirishe na hakika si kiwango kidogo. Kwa jumla ni kwamba hili si
suala la uhamiaji haramu bali ni la biashara haramu ya kusafirisha
binadamu.
Ndugu Wananchi;
Kufuatia vyombo vyetu vya usalama kuwa makini na watu wengi kukamatwa
ndipo wasafirishaji walipobuni njia za kuwasafirisha kama mizigo.
Makontena, malori yaliyofunikwa nyuma na matenki ya mafuta na ya maji
yamekuwa yanatumika kwa ajili hiyo. Usafiri wa aina hiyo ndiyo
uliosababisha vifo vilivyotokea Dodoma tarehe 26 Juni, 2012 na vya watu
21 vilivyotokea mwezi Desemba, 2011 Mkoani Morogoro, na vile
vya watu 12 vilivyotokea katika matukio mawili ya Mkoa
wa Mbeya, mwezi Mei, 2012.
Ndugu Wananchi;
Tarehe 27 Juni, 2012 nilikutana na wakuu wa vyombo vya ulinzi na
usalama nchini kuzungumzia tukio la Chitego na suala zima la biashara
hii haramu na hasa mbinu mpya inayotumiwa na wasafarishaji. Nilitoa
pongezi kwa vyombo vya dola kwa kazi nzuri waifanyayo kudhibiti shughuli
za biashara hii haramu hapa nchini. Tulielewana kuwa waendelee
kuimarisha udhibiti huo kwa lengo la kukomesha kabisa biashara hii.
Niliagiza pia kwamba kikundi kazi nilichokiunda mwaka 2006
kushughulikia ujambazi sasa kielekeze sehemu ya nguvu zake kukabili
tatizo hili. Aidha, kwa pamoja tulikubaliana kuwa nchi yetu ishirikiane
na wenzetu wa Ethiopia, Kenya, Malawi, Msumbiji na Afrika ya Kusini
kutambua mawakala na kuwabana kwa mujibu wa sheria. Tayari nimeshaanza
kufanya mawasiliano na baadhi ya Wakuu wa Nchi hizo kuhusu ushirikiano
huo. Nashukuru wote wameafiki nchi zetu zishirikiane kwa pamoja kuvunja
mtandao huu mchafu na kutokomeza biashara hii haramu na inayodhalilisha
utu wa mwanadamu.
Ndugu Wananchi;
Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru wenzetu, wakazi wa vijiji vya
Chitego na Mkoka kwa kazi nzuri walioifanya. Kwa kweli, wenzetu
wameonesha uzalendo wa hali ya juu kwa kutoa taarifa mapema juu ya jambo
lenyewe, lakini pia wameonesha utu kwa kuwajali wageni waliokumbwa na
janga hili. Naushukuru pia uongozi wa Mkoa wa Dodoma na Morogoro ikiwa
ni pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kulishughulikia tatizo
hilo kwa umakini mkubwa. Nimefurahishwa sana na ushirikiano
ulioonyeshwa na vyombo na taasisi mbalimbali za Serikali katika
kushughulikia suala hili.
Mgomo
wa Madaktari
Ndugu Wananchi;
Jambo la pili ni kuhusu mgomo wa Madaktari unaoendelea nchini hivi
sasa. Nilipozungumza na Wazee wa Dar es Salaam katika Ukumbi wa Diamond
Jubilee tarehe 12 Machi, 2012, kuhusu mgomo wa Madaktari uliokuwa
unaendelea wakati ule pamoja na kuelezea chimbuko la mgomo na hatua
iliyokuwa imefikiwa, nilielezea mazungumzo yangu na viongozi wa Chama
cha Madakari wakiwemo pia viongozi wa Jumuiya ya Madaktari. Nilitoa
taarifa kuwa tumeelewana kuwa watasitisha mgomo na watarudi kwenye meza
ya majadiliano na Serikali. Siku ile pia nilielezea matumaini yangu
kuwa mgomo ule utakuwa wa mwisho katika nchi yetu. Bahati mbaya
matumaini yangu hayo hayakuwa na hivi sasa tunashuhudia tena wagonjwa
wakiteseka, kuhangaika na wengine kufa kwa sababu ya kukosa huduma
wanazostahili kwa vile madaktari wao wamegoma tena.
Ndugu Wananchi;
Kama walivyoniahidi, madaktari waliacha kugoma na viongozi wao
walirudi kwenye mazungumzo na Serikali. Kama ilivyoagizwa na Mahakama
Kuu, Kitengo cha Kazi tarehe 8 Machi, 2012, kwa mujibu wa Sheria ya
Mahusiano Kazini, Namba 6 ya mwaka 2004. Chama cha Madaktari na
Serikali walifika katika Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (Commission for
Mediation and Arbitration) kwa ajili ya majadiliano. Kwa pamoja na kwa
ridhaa yao wote, pande hizo mbili ziliiomba Tume hiyo iwape fursa ya
kuzungumza wao wenyewe na wakimaliza mazungumzo wataenda kusajili
makubaliano yao. Tume ikawakubalia. Ni vizuri ikakumbukwa kuwa siku
ile ya tarehe 8 Machi, 2012 Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi, ilitoa zuio
la mgomo pamoja na kuagiza kuwepo mazungumzo baina ya pande mbili.
Ndugu Wananchi;
Kati ya tarehe 10 Aprili, 2012 na tarehe 30 Mei, 2012, vilifanyika
vikao sita vya majadiliano kati ya Serikali na Chama cha Madaktari.
Katika mazungumzo hayo hoja au madai 12 ya madaktari yalizungumzwa.
Mambo hayo ni haya yafuatayo:
1. Posho ya kuitwa kazini (on call allowance) iweasilimia
10 ya mshahara.
2. Posho ya kufanya kazi katika mazingira hatarishi (Risk
allowance) iwe asilimia 30 ya mshahara.
3. Madaktari wapatiwe nyumba grade A au posho ya makazi ambayo
iwe asilimia 30 ya mshahara.
4. Posho ya kufanya kazi katika mazingira magumu iwe asilimia
40 ya mshahara.
5. Madaktari walipwe posho ya usafiri ya asilimia 10 ya
mshahara au wakopeshwe magari.
6. Madaktari wanaoanza kazi walipwe mshahara washilingi
3,500,00/= kwa mwezi.
7. Madaktari wapatiwe Green Card za Bima ya afya.
8. Hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi ya Watendaji Wakuu wa
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
9. Viongozi wa Kisiasa kulazimisha kupewa rufaa nje.
10. Madaktari waliofukuzwa warudishwe kazini.
11. Huduma za afya ziboreshwe nchini.
12. Posho ya uchunguzi wa maiti iongezwe.
Ndugu Wananchi;
Katika mambo hayo 12 pande zote mbili zilifikia
muafaka na kukubaliana wa pamoja kwa mambo saba. La kwanza, ni
kuhusu usafiri wa kwenda na kurudi kazini. Serikali ilieleza kuwa upo
utaratibu kwa mujibu wa Waraka wa Utumishi wa Serikali Na. 3 wa mwaka
2011 wa kuwakopesha wafanyakazi wa Serikali fedha za kununulia magari au
pikipiki, samani na matengenezo ya magari. Ilikubaliwa kuwa madaktari
waitumie fursa hiyo.
Jambo la pili, ni kuhusu madaktari kupatiwa Green
Card za Bima ya Afya. Jambo hili lilikubaliwa na Serikali na Wizara ya
Afya imekwishachukua hatua za utekelezaji wake.
Jambo la tatu, ni kuhusu hatua za kinidhamu
kuchukuliwa dhidi ya Watendaji Wakuu wa Wizara ya Afya. Kwa pamoja
walikubaliana kuwa suala hilo liko nje ya mamlaka ya Kamati yao ya
pamoja, waziachie mamlaka husika za uteuzi. Uongozi wa juu wa Wizara
umebadilishwa na sasa kuna uongozi mpya. Lakini, jambo la kustaajanisha
hata Waziri mpya wa Afya alipowataka waonane kuzungumzia hoja walikataa
kumuona. Kwanza walisema hawaoni sababu kwa vile wameyazungumza na
Kamati yake kwa miezi mitatu bila ya mafanikio
Jambo la nne walilokubaliana ni kuhusu viongozi
kulazimisha kupewa rufaa ya kutibiwa nje. Walikubaliana mambo mawili. Kwanza, kwamba
maelekezo ya Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda kuwa madaktari wazingatie
maadili ya kazi zao na kukataa kutoa rufaa kwa mtu asiyestahili awe
kiongozi au asiwe kiongozi. Pili, walikubaliana kuwa
hospitali zilizopo ziboreshwe ili viongozi watibiwe hapa nchini. Ukweli
ni kwamba kufanya hivyo ndiyo sera ya Serikali. Nililieleza hili mwezi
Desemba 30, 2005 katika hotuba yangu ya kuzindua Bunge baada ya
kuchaguliwa kwa mara ya kwanza kuongoza nchi yetu.
Tumeiongeza sana bajeti ya sekta ya afya kutokashilingi
bilioni 300 2005/2006 hadi shilingi trilioni 1.2mwaka
2011/12 na imekuwa ya tatu baada ya miundombinu na elimu.
Tumeziimarisha hospitali za Mikoa kwa vifaa tiba na wataalamu wa afya.
Kazi inaendelea katika hospitali za Wilaya. Tumewekeza katika Hospitali
ya Muhimbili. Hospitali hiyo ilivyo leo sivyo ilivyokuwa miaka sita
nyuma. Na kazi inaendelea hasa katika maeneo ambayo tunapeleka wagonjwa
nje. Matunda yake yanaanza kuonekana kwa upande wa figo, moyo, kinywa
na mipango inaendelea kwa upande wa ubongo na mishipa ya fahamu.
Tunaendelea kuimarisha mafunzo ya madaktari na madaktari bingwa, yote
kwa nia hiyo hiyo. Hivi sasa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba,Muhimbili
kinachukua wanafunzi wengi zaidi ya ilivyokuwa siku za nyuma na makazi
mapya ya chuo yanaendelea kuandaliwa ili kuchukua wanafunzi wengi zaid.
Mwaka 2005 tulikuwa na madaktari bingwa 46 mwaka huu
tunao 520.
Ndugu Wananchi;
Jambo la tano ambalo pande zote mbili zilikubaliana
ni kuhusu madaktari waliofukuzwa. Hawa ni wale Internswaliokuwa
wamerudishwa Wizarani kutoka Muhimbili na kupangiwa hospitali za
Temeke, Ilala, Mwananyamala na Lugalo. Hili ni jambo ambalo lilikuwa
limemalizika kitambo na wote walikuwa wamerudi Muhimbili.
Jambo la sita ni kuhusu mapendekezo mbalimbali
yaliyotolewa na madaktari kuhusu kuboresha huduma ya afya. Mapendekezo
hayo yalihusu kutathmini sera na mpango wa afya ya msingi, bajeti ya
afya kuwa asilimia 15ya bajeti ya Serikali, kuwepo na
utaratibu mzuri wa kuajiri madaktari na kuboresha viwango vya ubora wa
madaktari na kadhalika. Serikali imeyaafiki mapendekezo hayo na
yatafanyiwa kazi.
Jambo la saba, ambalo pande zote walilokubaliana ni
kuhusu kuongeza posho ya uchunguzi wa maiti. Hili ni jambo jipya
halikuwepo mwazoni. Hata hivyo, Serikali imelikubali na posho hiyo
imeongezwa kutoka shilingi 10,000/= hadi kufikia shilingi
100,000/= kwa daktari nashilingi 50,000/= kwa
wasaidizi wake.
Ndugu Wananchi;
Kuna masuala matatu ambayo yamekuwa na muafaka kwa
kiasi fulani na kutoafikiana kwa baadhi ya mambo. La kwanza ni
suala la kufanya kazi katika mazingira hatarishi. Serikali imekubali
hoja ya kuchukua hatua ya kuwalinda madaktari wanaofanya kazi katika
mazingira hatarishi. Serikali iliwaeleza kuwa watumishi wa kada zote za
afya watapatiwa chanjo dhidi ya maambukizi ya Hepatitis B na
fedha zimetengwa katika bajeti ya 2012/13.
Aidha, Serikali imeeleza dhamira ya kurudisha posho ya mazingira
hatarishi kwa watumishi wa umma wanaostahili. Utekelezaji wake
utafanyika baada ya uchambuzi wa kina wa kubainisha mazingira hatarishi
ni yepi, viwango stahiki viwe vipi na nani hasa wahusike. Madaktari
wamekataa hili la kufanya uchambuzi, wanataka kiwango kiwe kama
wanavyotaka wao, yaani asilimia 30 ya mshahara na
kianze mara moja.
Jambo la pili ambalo wamekubaliana nusu nusu ni kuhusu nyumba za
kuishi. Serikali imekiri wajibu wake wa kuwapatia madakari nyumba za
kuishi. Aidha, imeeleza mpango ulioanza wa kujenga nyumba 700 za
madaktari kote nchini na kwamba hivi sasa ujenzi wa nyumba 90unaendelea, 50 katika
mkoa wa Mtwara na 40 katika mkoa wa Rukwa.
Kwa maeneo ambayo madaktari wanalipwa posho ya pango Serikali imesema
waajiri wataendelea kufanya hivyo kwa mujibu wa taratibu zilizopo kwa
watumishi wa umma wenye stahili ya kupewa nyumba. Jambo hilo
limekataliwa na Madakari na kutaka lazima walipwe asilimia 30 ya
mshahara kama posho ya nyumba. Serikali kwa upande wake imeona vigumu
kufanya hivyo na kuwasihi wakubali wanayotendewa wafanyakazi wengine
wote wa umma.
Jambo lingine ambalo lilikuwa na makubaliano ya nusu
nusu ni kuhusu posho ya kufanya kazi katika mazingira magumu. Pande
zote mbili ziliafikiana kuwa yapo baadhi ya maeneo nchini yanayo
mazingira magumu kwa watumishi wa umma hivyo hatua zichukuliwe
kuwasaidia watumishi hao. Serikali imekubali wajibu wa kuweka utaratibu
wa kuboresha maisha ya watumishi katika maeneo hayo. Kwa ajili hiyo,
Serikali itatoa mwongozo kwa mamlaka za ajira kuhusu namna ya kuwasaidia
watumishi hao kupunguza makali ya maisha katika kila eneo badala ya
kutegemea posho peke yake.
Kuhusu posho, Serikali imeeleza kuafiki kuwepo posho ya aina hiyo ila
itatekelezwa baada ya kufanya uchambuzi wa kuainisha mazingira husika,
kutambua watumishi waliopo na gharama zake.
Madaktari hawajakubali kusubiri zoezi la uchambuzi lifanyike,
wanataka Serikali ilipe posho hiyo sasa. Tofauti hapa si posho hiyo
kuwepo, bali ni rai ya Serikali ya kubaini maeneo yenyewe na kupanga
aina ya hatua na viwango vya posho kulingana na mazingira halisi ya
maeneo. Madaktari hawaoni haja ya kufanya hayo.
Ndugu Wananchi;
Mambo mawili hayakuwa na muafaka kabisa kati ya pande zetu mbili.
Jambo la kwanza ni posho ya kuitwa kazini (on call allowance). Kwanza
sina budi kueleza kuwa Serikali imekubali kuongeza posho hiyo. Tangu
Februari, 2012 posho iliongezwa kutoka shilingi 10,000/= hadi
shilingi25,000/= kwa daktari bingwa (Specialist), shilingi
20,000/=kwa dakari mwenye usajili wa kudumu (Registrars) nashilingi
15,000/= kwa madaktari waliohitimu ambao wapo katika kipindi
cha mafunzo kazini (Interns). Viwango hivyo vya posho vinatumika hivi
sasa.
Madaktari kwa upande wao hawakukubali uamuzi huo wa Serikali na
kusisitiza walipwe asilimia 10 ya mshahara. Ugumu wa
kukubali pendekezo la madakari ni kuwa sharti la malipo haya ni mtu
kuitwa kazini. Ukitaka ilipwe kiwango cha mshahara ina maana kuwa hata
kama daktari hakupangwa kuitwa au alipangwa na hakutokea aendelee
kulipwa. Hili haliwezi kuwa sahihi kufanya. Linaweza kuwafanya baadhi
ya madaktari kutokutimiza wajibu wao kwa vile wana hakika mwisho wa
mwezi malipo yako pale pale.
Ndugu Wananchi;
Jambo la pili ambalo muafaka haukufikiwa baina ya Serikali na
madaktari ni kuhusu mshahara wa kuanzia kazi wa daktari. Madaktari
wanataka uwe shilingi 3,500,000/=wakati Serikali
inasema kiasi hicho hatukiwezi. Serikali imeeleza utayari wake wa
kuongeza mshahara kwa kati yaasilimia 15 mpaka 20 kama
ambavyo itafanya kwa watumishi wote wa umma katika mwaka huu wa fedha.
Kwa kiwango cha sasa cha mshahara wao, daktari ataanzia kati ya shilingi
1,100,000/= na 1,200,000/= kutegemea kiwango
kipi hatimaye kitaamuliwa. Madaktari wamekataa katakata na
wameng’ang’ania shilingi 3,500,000/=.
Ndugu Wananchi;
Huo ndiyo mlolongo wa mambo yaliyozungumzwa na pande zote mbili na
matokeo ya mazungumzo yenyewe. Katika kikao cha sita kilichofanyika
tarehe 30 Mei, 2012, upande wa Chama cha Madaktari ulisema kuwa kwa vile
hoja ya nyongeza ya mshahara haina mabadiliko hawakuona haja ya
kuendelea na majadiliano mpaka watakapowasiliana na wenzao. Waliahidi
kutoa taarifa ndani ya wiki mbili. Tarehe 12 Juni, 2012, Rais wa MAT
aliandika barua kwa Katibu Mkuu Utumishi ambaye ndiye kiongozi wa
majadiliano kwa upande wa Serikali, kuwa Madaktari wameikataa taarifa na
ufafanuzi waliopewa kutoka Serikalini kwa ujumla wake.
Ndugu Wananchi;
Baada ya majibu yale ya madaktari, tarehe 19 Juni, 2012, Serikali na
Madaktari walikwenda kwa Msuluhishi (CMA) kutoa taarifa kuwa mgogoro
umekosa usuluhishi kama sheria inavyotaka. Kwa pamoja pande zote mbili
zilikubaliana suala hilo lifikishwe Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi.
Wakati pande zote zinasuburi mgogoro huu kufikishwa ngazi hiyo ya juu,
upande wa Madaktari ukatangaza kuwepo kwa mgomo kuanzia saa sita ya
usiku tarehe 23 Juni, 2012. Hatua hiyo haikustahili kwani suala lenyewe
halijafika mwisho wa kushughulikiwa kwa mujibu wa Sheria za Mahusiano
ya Kazi nchini.
Ndugu Wananchi;
Tarehe 22 Juni, 2012, Mwanasheria Mkuu wa Serikali akaenda Mahakama
Kuu Kitengo cha Kazi kulifikisha suala la tishio la mgomo na kuomba zuio
la muda kufanywa. Mahakama Kuu ilikubali ombi hilo na kuagiza kuwa
mgomo usitishwe. Juhudi za kumtafuta Rais wa MAT, Dkt. Namala Mkopi na
viongozi wengine wa MAT hazikufanikiwa, Ofisi ya MAT ilikuwa imefungwa
na simu zote za viongozi wa MAT zilikuwa zimezimwa. Hatimaye tarehe 25
Juni, 2012, alipatikana na kupewa amri hiyo ya Mahakama. Tarehe 26
Juni, 2012, Dkt. Mkopi alifika Mahakamani ambapo alikana kuwa yeye
hahusiki na kuitisha huo mgomo lakini hakumtaja aliyehusika. Pamoja na
rai hiyo, Jaji alimuamuru Rais wa MAT akawatangazie wanachama wake
kusitisha mgomo. Dkt. Namala Mkopi hajafanya hivyo hadi leo na mgomo
umekuwa unaendelea kinyume cha Sheria.
Ndugu Wananchi;
Wagonjwa wanateseka na wengine kupoteza maisha kwa mgomo huu usiokuwa
halali kisheria ambao pia haustahili kuwepo hata kwa mujibu wa maadili
ya udaktari. Viongozi wa MAT na wenzao wanawaingiza Madaktari katika
mgogoro na Mahakama na waajiri wao isivyostahili. Ni vyema viongozi wa
Madaktari na madaktari wakatambua kuwa wanashiriki katika mgomo usiokuwa
halali ambao pia kiongozi wao mkuu amekana Mahakamani kuwa hahusiki
nao. Madaktari lazima watambue pia kwamba ajira zao wanaziweka
hatarini. Mfanyakazi ana kinga ya kutofukuzwa kazi na mwajiri kwa
kushiriki mgomo unaokubalika kisheria. Huu siyo. Watapoteza ajira,
hawana pa kukimbilia, hawana cha kiwalinda. Kwa madaktari interns,
wanahatarisha maisha yao kwani hawatapata cheti cha kudumu wakishiriki
mgomo usiokuwa halali. Lazima watafakari sana kwa hayo wafanyayo.
Ndugu Wananchi;
Napenda kurudia maneno niliyoyasema tarehe 12 Machi, 2012, kuwa
kuboresha mishahara na maslahi ya wafanyakazi ni Sera ya Serikali yetu
kwa maelekezo ya Ilani ya Chama Tawala (CCM). Tumeitekeleza kwa vitendo
sera hiyo, hata hivyo ni ukweli ulio wazi kuwa nia yangu njema tu pekee
haitoshi, lazima uwezo wa kufanya hivyo uwepo. Kwa kulingana na uwezo
uliopo, tumeendelea kuboresha mishahara na maslahi ya wafanyakazi hatua
kwa hatua tangu tuingie madarakani. Tumefanya hivyo kwa jumla kwa
wafanyakazi wote na kwa kada mbalimbali za watumishi wa umma.
Miongoni mwa wafanyakazi wa umma walionufaika na hatua hizo za
Serikali ni madaktari na watumishi wa kada nyingine za huduma ya afya.
Tena nadiriki kusema madaktari tumewapa upendeleo mkubwa kuliko
watumishi wengine wa umma. Upendeleo upo kwenye mafunzo ambapo
wanafunzi wa udaktari wanagharimiwa na Serikali kwa asilimia mia moja
wakati wanafunzi wenzao wa taaluma nyingine hawako hivyo.
Ndugu Wananchi;
Mwaka 2004/2005, mshahara wa kuanzia wa daktari ulikuwa shilingi 178,700/=,
mwaka 2005/ 2006 tuliupandisha na kuwa shilingi 403,120/=. Tuliendelea
kuupandisha mwaka hadi mwaka mpaka kufikia shilingi 957,700/= wanazolipwa
sasa. Kiasi hicho ni mara mbili ya mishahara ya watumishi wa taaluma
nyingine wenye shahada ya kwanza wanaoanza kazi ambao kwa wastani hupata
shilingi 446,100/=.
Tunafanya hivyo kwa kutambua na kuthamini nafasi maalum ya madaktari
katika jamii na ukweli kwamba bado tunayo safari ndefu ya kuziba pengo
la madaktari nchini. Lakini inaonekana juhudi zetu zote hizo
hazithaminiwi.
Ndugu Wananchi;
Sina budi kusisitiza kwamba tunapofanya hivyo tunaongozwa na uwezo
tulio nao wa kulipa. Kwa sasa hatuwezi kuwaahidi kuwa tunao uwezo wa
kuwalipa mshahara wa kuanzia wa shilingi 3,500,000/= na
posho zote zile. Tukifanya hivyo malipo ya daktari anayeanza kazi
yatakuwa shilingi 7,700,000/=. Kwa hakika kiasi hicho
hatutakiweza. Si vyema kutoa ahadi hewa kwa watu tunaowaheshimu na
kuwathamini kama walivyo madaktari.
Kutokana na ukweli huo basi kama daktari anayeona kuwa hawezi kufanya
kazi Serikalini bila ya kulipwa mshahara huo awe huru kuacha kazi na
kwenda kwa muajiri anayeweza kumlipa kiasi hicho. Nasi tutamtakia kila
la heri. Hana sababu ya kugoma ili ashinikize kulipwa mshahara huo.
Asisumbuke, hatalipwa mshahara huo. Isitoshe, hana sababu ya kuendelea
kuwa na mgogoro na mwajiri ambaye hana uwezo wa kumlipa anachokitaka.
Huna sababu ya kumpa usumbufu mwajiri wa kukuandikia barua ya kujieleza
au kukuachisha kazi. Kwa nini upate usumbufu wa kupata barua hizo na
kuzijibu. Kwa nini upate usumbufu wa kuachishwa kazi na kutakiwa
kuondoka kwenye nyumba ya Serikali ndani ya saa 24. Jiepushe na yote
hayo kwa kujiondoa mwenyewe. Usipofanya hivyo, mwajiri anakuwa hana
jinsi bali kukuondoa kazini maana unakwenda kinyume na sheria za kazi na
maadili ya kazi ya udaktari.
Mamlaka za ajira zimeanza kuchukua hatua hizo na wataendelea kufanya
hivyo kwa wote wanaoendelea kugoma. Najua baada ya hatua hizo
kuchukuliwa kuna manun’guniko ya kuonewa. Hivyo, mlitegemea mwajiri
afanyeje? Ni bora kufanya hivyo ili ajue hana daktari aweze kufanya
utaratibu wa kuziba hilo pengo na huyo ajae awe na mahali pa kuishi.
Vinginevyo atakuwa anajidanganya kuwa anae daktari ambae hayupo kazini
na wala hataki kufanya kazi.
Ndugu Wananchi;
Napenda kuwathibitishia kwamba dhamira ya Serikali ya kuboresha
maslahi ya watumishi wa umma wakiwemo madaktari iko wazi. Tumekuwa
tunafanya hivyo, na tutaendelea kufanya hivyo kulingana na uwezo wa
kibajeti. Ni vyema watumishi wa umma wakatambua kuwa hatuwezi kutumia
fedha zote au kiasi kikubwa mno cha pesa za umma kulipana mishahara.
Tukifanya hivyo, Serikali itashindwa kutoa huduma muhimu kwa wananchi
ambao ndiyo wengi na wanastahili kuhudumiwa. Hata hizo huduma za afya
tunazosema ni duni tuziboreshe, hatutaweza kuziboresha kama tutatumia
sehemu kubwa ya pesa za Serikali kuwalipa mishahara wafanyakazi.
Hivi sasa matumizi ya mishahara ni asilimia 48 ya
bajeti ya Serikali. Kiwango hicho ni kikubwa mno. Uwiano mzuri ni kuwa
na matumizi ya mishahara yasiyozidiasilimia 35 ya
bajeti na asilimia 65 zitumike kugharimia huduma na
shughuli nyingine za maendeleo ya wananchi na taifa. Sisi tumezidi kwa asilimia
13. Hivyo, hatuna budi tukubali kujinyima kwa manufaa ya
walio wengi.
Suala
la Dkt. Steven Ulimboka
Ndugu Wananchi;
Kabla ya kumaliza hotuba yangu, napenda kuungana na Watanzania
wenzangu wote kuelezea masikitiko yangu makubwa na kuhuzunishwa kwangu
na kitendo cha kinyama alichofanyiwa Dkt. Steven Ulimboka usiku wa
tarehe 26 Juni, 2012. Kitendo hicho ni kinyume kabisa na mila na desturi
zetu. Watanzania hatujayazoea mambo hayo. Nimeelekeza vyombo vyetu vya
ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina ili ukweli ujulikane.
Nimesema kuwa ningependa ukweli huo ujulikane mapema ili tuondoe wingu
baya la kutiliana shaka na kulaumiana kunakoendelea hivi sasa.
Natambua kuwa Serikali nayo inatajwa katika orodha ya wanaotiliwa
shaka. Mimi nimeshangazwa sana na hisia hizo kwani siioni sababu ya
Serikali kufanya hivyo. Dkt. Ulimboka alikuwa mmoja wa kiungo muhimu
katika mazungumzo baina ya Serikali na Madkatari. Ni kweli kwamba yeye
si mtumishi wa Serikali, hivyo hakustahili kuwa sehemu ya majadiliano
haya. Kulikuwa na rai ya kutaka asiwepo, lakini nilisema wamuache
maadam Madaktari wanamuamini kuwa anaweza kuwasemea vizuri zaidi kuliko
wao wenyewe walioajiriwa na Serikali.
Ndugu Wananchi;
Kama nilivyoeleza, mazungumzo yalienda vizuri na mafanikio makubwa
yamepatikana. Yapo maeneo machache na hasa eneo la mshahara ambalo
hatukuweza kukubaliana. Hapo tulipofikia si pabaya na tulikubaliana
sote kurudi kwenye mkondo wa Sheria kusaidiwa. Kwa nini Serikali
imdhuru Dkt. Ulimboka? Na, kuhusu mgomo, Mahakama Kuu imekwishatoa amri
ya kusitisha mgomo. Anayekaidi amri ya Mahakama ananunua ugomvi na
mhimili huo wa dola ambao wenyewe una mamlaka ya kumtia adabu mtu huyo.
Hivi baada ya kufika hapo Serikali iwe na ugomvi na Dkt. Steven
Ulimboka kwa sababu ipi na jambo lipi hata iamue kumdhuru? Kama kuna
mtu wa Serikali kafanya, itakuwa kwa sababu zake binafsi na siyo za
Serikali au kwa kutumwa na Serikali.
Ndugu Wananchi;
Kwa niaba yangu na kwa niaba ya Serikali natoa mkono wa pole kwa Dkt.
Steven Ulimboka na kumuombea apone haraka ili aungane na familia yake
na Watanzania wenzake katika ujenzi wa taifa. Kwa namna ya pekee
namshukuru na kumpongeza Bwana Juma Mgaza, kwa moyo wake wa huruma na
upendo na kwa hatua alizochukua za kumsaidia Dkt. Ulimboka.
Naomba kumaliza kwa kuwasihi madaktari kuacha mgomo na kurejea
kazini. Watanzania wenzenu wanateseka na kupoteza maisha. Muwe na moyo
wa huruma na upendo na msaada kwa wagonjwa kama kiapo chenu
kinavyowataka.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni kwa Kunisikiliza.