Baba wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Madaktari, mzee Steven Mwaitenda (katikati) akipokea faraja kwa niaba
ya mwanaye toka kwa wanaharakati (hawapo pichani)
Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Usu
Mallya (kushoto) akiwa na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano,
Lilian Liundi walipomtembelea Dk. Ulimboka kumfariji jana.
Baba wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Madaktari, mzee Steven Mwaitenda (kushoto) akipokea kadi yenye ujumbe
toka kwa wanaharakati walipomtembelea jana, anayetoa kadi hiyo (kulia)
ni Mkurugenzi wa TGNP, Usu Mallya.
BABA wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Madaktari, mzee Steven Mwaitenda .
Mzazi akimlilia mwanaye Dk. Ulimboka
kwa uchungu MOI.
Mzee Steven Mwaitenda (katikati)
akifarijiwa na kurejeshwa wodini baada ya kulia.
Baba wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Madaktari, mzee Steven Mwaitenda akilia na kufarijiwa.
Mwakilishi wa wanaharakati, Markos
Albania (katikati) akizungumza na wanahabari baada ya kumtembelea Dk.
Steven Ulimboka.
Usu Mallya akilia baada ya kushuhudia
mzee Steven Mwaitenda akibubujikwa na machozi mbele yao.
Baadhi ya wanaharakati anuai wakiwa na
maua walipomtembelea Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Ulimboka
kumfariji jana.
Baadhi ya wanaharakati wakiwa na nyoso
za hudhuni baada ya kilio cha baba wa Dk. Ulimboka jana MOI.
---
Na Joachim Mushi,
BABA wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Madaktari, mzee Steven Mwaitenda amejikuta akiangua kilio kwa uchungu
mbele ya wanaharakati ambao walimtembelea mwanae, Dk. Steven Ulimboka
kumpa pole kufuatia tukio la kutekwa na kujeruhiwa vibaya na watu
wasiojulikana.
Hali hiyo ilitokea jana jioni katika
Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), ambapo wanaharakati kutoka
taasisi na asasi mbalimbali za utetezi wa haki za binadamu walifika kwa
lengo la kumpa pole Dk. Ulimboka kufuatia kitendo kilichomfika.
Mzee Mwaitenda alijikuta akibubujikwa na
machozi na kushindwa kuendelea kuzungumza alipokuwa akitoa shukrani kwa
wanaharakati hao, kwa niaba ya mwanaye ambaye wanaharakati hao
walishindwa kumuona wote kutokana na hali yake ilivyo sasa.
“Niseme wazi nimefarijika sana kwa ujio
wenu kumwona mwanangu dhidi ya mambo ya kikatili aliyofanyiwa akitetea
haki za wengine…,” alisema mzee Mwaitenda kabla ya kushindwa kuendelea
na kuangua kilio mbele ya wanaharakati.
Baada ya tukio hilo baadhi ya
wanaharakati walimshika wakishirikiana na wanafamilia ya mzee Mwaitenda
na kumbebeleza kisha kumtoa mbele ya mkusanyiko huo wa wanaharakati na
kumrudisha wodini huku wakimfariji.
Wakizungumza mara baada ya tukio hilo
wanaharakati wameelezea kusikitishwa na vitendo vinavyoendelea MOI eneo
ambalo amelazwa kiongozi huyo wa madaktari ambavyo vimeendelea kutishia
usalama wa Dk. Ulimboka.
Akifafanua zaidi mwakilishi wa
wanaharakati hao, Markos Albania alisema taarifa walizozipata usiku wa
juzi kuna wagonjwa ‘feki’ ambao walijitokeza MOI huku wakitaka kulazwa
wodi ya Wagonjwa Mahututi (ICU) alipolazwa Dk. Ulimboka lakini baadaye
waligoma kuingizwa wodini.
“Wapo wagonjwa ambao waliletwa na kutaka
kupelekwa ICU moja kwa moja…kuna watu wanakuja usiku wa manane wakitaka
kumtembelea Dk. Ulimboka…matendo yanayoendelea kutokea ukilinganisha na
kauli za Serikali zilizotolewa bungeni yanatishia usalama na uhai wa
mgonjwa,” alisema Albania.
Aidha amesema kitendo cha vyombo vya
usalama kuendelea kumuhoji Dk. Ulimboka akiwa hoi hospitalini si vya
kiungwana kwani tayari muhusika amewataja hadi kwa majina watu ambao
anawashuku lakini hadi sasa hakuna aliyechukuliwa hatua yoyote.
Pamoja na hayo wanaharakati hao
wameitaka Serikali kuunda tume huru mchanganyiko na raia ambayo
itachunguza kiundani suala hilo, kwani hawana imani na Jeshi la Polisi
ambalo limedai kuunda timu ambayo inachunguza kwa kina suala hilo.
Dk. Ulimboka ambaye ni kiongozi wa
madaktari ambao wanaendelea na mgomo wan chi nzima kuishinikiza Serikali
kutekeleza madai yao alitekwa juzi na watu wasiojulikana na kupigwa na
kuteswa kikatili kabla ya kutelekezwa katika msitu wa Mabwepande.
Kwa hisani ya MPEKUZI BLOG
Kwa hisani ya MPEKUZI BLOG