
ASEMA
ATAANIKA KILA KITU BAADAYE, ASEMA ACHWE APUMZIKE, MKUU WA JOPO LA
MADAKTARI WANAOMTIBU ASEMA ALING'OLEWA KUCHA, MENO MAWILI NA KUPATA
MTIKISIKO WA UBONGO.
MWENYEKITI
wa Jumuiya ya Madaktari aliyetekwa nyara na kuumizwa vibaya usiku wa
kumkia juzi, kisha kutupwa Msitu wa Pande, Dk Steven Ulimboka amesema
atazungumza kwa kina yote yaliyomsibu baadaye na kuomba sasa aachwe
auguze maumivu makali yanayomkabili.
Dk
Ulimboka aliokotwa na wasamaria wema juzi asubuhi katika Msitu wa
Pande nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, baada ya kutekwa nyara na
watu waliokuwa na silaha akiwa katika Viwanja vya Klabu ya Leaders,
Kinondoni.
Jana,
Dk Ulimboka ambaye amelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili huku hali
yake ikiwa haijatengemaa vyema, alitoa kauli akisema ingawa ana maumivu
makali anaendelea vizuri ikilinganishwa na siku ya kwanza.
Dk Ulimboka alitoa kauli hiyo baada ya kutakiwa aeleze mkasa huo uliomfika wa kukamatwa, kuteswa na kutupwa msituni.
Hata
hivyo, hadi sasa wingu zito la nani alimteka na watekaji walitaka
kujua nini kutoka kwa kiongozi huyo wa madaktari, bado limetanda.
Siri nzito
Akisimulia
mkasa huo kupitia Kituo cha Redio cha Clouds FM, Dk Ulimboka alisema,
akiwa katika klabu hiyo ya Leaders alipigiwa simu na rafiki yake ambaye
alikuwa atokee Tandika na baada ya kumsubiri ndipo alipofika kwenye
klabu hiyo, lakini, alianza kujisikia vibaya tofauti na siku nyingine na
kuongeza; "Yaani sikuwa na amani."
Alisema,
"Mara, katikati ya maongezi tukaona mtu anaongea na simu. Ghafla
tukiwa tunasema tuagane, wakaja watu kama watano hivi na bunduki,
wakasema wewe na yule bwana mko free (huru), tunakuchukua wewe (Dk
Ulimboka)," alieleza na kuongeza:
"Sijakaa
sawa, nikaona nimeshaburutwa nikaanguka kwenye lami, wakaniinua na
kuniingiza kwenye gari nyeusi, lakini halikuwa na namba."
Hata
hivyo, jana Dk Ulimboka hakuonana na mwandishi wa habari hii, badala
yake alirekodiwa, na Mwananchi kupata sauti yake akijibu swali kuhusu
hali yake na tukio hilo, baada ya uongozi wa Taasisi ya Mifupa
Muhimbili (Moi) kuzuia watu kumwona.
Daktari huyo wa magonjwa ya binadamu, amelazwa katika chumba cha Wagonjwa Wanaohitaji Uangalizi Maalumu (ICU).
"Kidogo
najisikia nafuu ikilinganishwa na nilivyokuja ingawaje, bado nina
maumivu makali. Kwa hivyo, ingependeza niendelee na mapumziko na mtu
yeyote anayetaka kuniona pengine hilo jambo lisifanyike sasa. Hivi sasa
ni vizuri nipumzike," ilisikika sauti hiyo ya Dk Ulimboka.
Lakini,
uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa wodini alikolazwa Dk Ulimboka,
kuna ulinzi mkali wa madaktari na hairuhusiwi watu kumwona kiholela
siyo tu kwa sababu za kutaka aachwe apumzike, bali pia kutowaamini watu
ovyo.
Madaktari
wanaolinda eneo hilo walisikika jana wakisema, “Huyu tunamlinda
wenyewe na haiwezekani mtu asiyefahamika kuingia humu ndani, na hilo
tutahakikisha sisi wenyewe,”alisikika akisema mmoja wa madaktari hao.
Kiongozi jopo la madaktari
Katika
hatua nyingine, kiongozi wa jopo la madaktari wanaomuhudumia Dk
Ulimboka, Profesa Joseph Kahamba aliwaambia waandishi wa habari kuwa Dk
Ulimboka ana majeraha mwili mzima.
“Ingawa
kwa sasa anaendelea vizuri, Dk Ulimboka ameumia sana, kwani mwili
wake mzima una majeraha kutokana na kupigwa na watekaji hao,”alisema
Profesa Kahamba na kuongeza:
“Aliumia
mbavuni,kifuani, miguuni, mikononi ambako aling’olewa baadhi ya kucha
za vidole na kichwani na kinywani, ambako aling’olewa meno
mawili,”alisema.
Alifafanua
kwamba, kutokana na maumivu hayo ya kichwa, Dk Ulimboka alipata tatizo
la mtikisiko wa ubongo, lakini akasisitiza kuwa madaktari bingwa
wanaendelea na harakati za kuokoa maisha yake.
Uongozi wa Moi watoa neno
Uongozi
wa Taasisi ya Mifupa (Moi) umeeleza kuwa hali yake inaendelea vizuri
ingawa bado amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi cha taasisi
hiyo.
Msemaji
wa Moi, Almas Jumaa aliwaambia waandishi wa habari kuwa licha ya hali
yake kuendelea vizuri, lakini haingewezekana kwa waandishi wa habari
kuingia ndani ya chumba alikolazwa na kumwona Dk Ulimboka.
“Mgonjwa
anaendelea vizuri ukilinganisha na jana (juzi), anaongea, anawatambua
watu wanaokwenda kumwona, lakini utaratibu wa kwenda kumwona kwa ninyi
imeshindikana kwa sababu yupo (ICU) ni chumba chenye utaratibu
wake,”alisema Jumaa.
Jumaa
aliongeza kwamba ili mtu aweze kuingia wodini analazimika kuvaa vazi
maalumu na mavazi yaliyopo, yasingetosha, lakini pia wapo watu
wanaoendelea kumpatia huduma ya matibabu.
Tamko la Jumuiya ya Madaktari
Wakati
hali ya Dk Ulimboka ikiwa hivyo, madaktari wameipinga tume ya
uchunguzi iliyoundwa na Jeshi la Polisi kuchunguza suala hilo, wakidai
mazingira ya tukio hayaliondoi jeshi hilo kuhusika.
Katibu
wa Jumuiya hiyo, Dk Edwin Chitage aliwaambia waandishi wa habari kuwa
wangependa kuundwa kwa tume huru itakayofanya kazi ya kuchunguza tukio
hilo na kutoa taarifa kwa umma.
“Madaktari
kwa ujumla wetu tunalaani tukio la kutekwa nyara,kupigwa na kutupwa
katika Msitu wa Pande, lakini pia hatuna imani na tume iliyoundwa na
Jeshi la Polisi kwa sababu mazingira ya tukio hayaondoi kuhusika ama
kutohusika kwa jeshi hilo,”alisema Dk Chitage.
Chitage
alitoa msimamo wa madaktari kuwa ni kuendelea na mgomo, huku akionya
Serikali kuacha vitendo vya kuwatisha, kwa madai kuwa vitendo hivyo
haviwezi kuwa suluhu ya mgogoro kati ya pande hizo mbili.
“Kumekuwa
na vitisho kwa madaktari katika maeneo mbalimbali nchini, hususan
Dodoma, Mbeya, Arusha na Mwanza. Tunaionya Serikali kuacha mara moja na
itambue kuwa mgogoro huo hauwezi kumalizwa kwa namna nyingine yoyote
bali ni kwa Serikali kutekeleza madai ya madaktari,”alisema Chitega na
kuongeza:
“Sisi
madaktari kwa umoja wetu, tumechoka kushuhudia Watanzania wakipoteza
maisha kwa magonjwa tunayoweza kuyatibu, kufanya kazi katika mazingira
magumu huku kukiwa hakuna mipango ya kuboresha mazingira ya kazi,
kukosekana kwa dawa na vifaa tiba.”
Mgomo
huo wa madaktari leo unaingia siku ya saba tangu ulipotangazwa na
mwenyekiti huyo kuwa, ungeanza rasmi Jumamosi iliyopita.
Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz