Tunasikitika mno kuondokewa na
mfanyakazi wetu ambaye alikuwa mchapakazi na mwenye ueledi mkubwa
katika tasnia ya uandishi wa habari. Kwa wanaomfahamu Willy watakuwa
mashahidi wa hilo tunalosema.
Hadi sasa hatujapata taarifa rasmi
za kidaktari kuhusu kifo chake, lakini taarifa zilizopatikana kutoka
kwa ndugu wa marehemu zinasema alikuwa anasumbuliwa na tatizo la moyo.
Mwili wa marehemu utawasili leo, Juni 17, 2012 na maandilizi ya mazishi
yanaendelea.
WASIFU
Willy Edward Daniel Ogunde ambaye alikuwa
Mhariri Mkuu wa gazeti la Jambo Leo alizaliwa Machi 7, 1974 katika
Wilaya ya Serengeti mkoani Mara.
Alisoma shule ya msingi Mapinduzi
mwaka 1983 hadi 1989 kisha elimu ya Sekondari katika shule ya Serengeti
mwaka 1990 hadi 1993.Baadaye alijiunga na shule ya Sekondari Musoma
kidato cha tano na sita mwaka 1994 na 1995.
Mwaka 1996 alijiunga na Kampuni ya
uchapishaji wa magazeti ya BTL akiwa mwandishi wa gazeti wakati huo
likiitwa Majira Jioni.
Akiwa na kampuni hiyo alipata
mafunzo mafupi ya kikazi yakiwemo ya kompyuta na ya uandishi wa habari.
Mwaka 1998 alihamishwa kitendo
kutoka kwenye gazeti la Majira Jioni kwenda kwenye gazeti jipya la Dar
Leo na kuwa mwandishi wa habari wa hazeti hilo lakini pia akishikilia
nafasi ambazo alikuwa akizitumikia kwenye gazeti la Majira Jioni.
Alifanikiwa kuaminika na kutokana
na uwezo wake kazini alipanda daraja na kuwa Mhariri wa gazeti la Dar
Leo kuanzia mwaka 2002 hadi 2005.
Kipindi cha mwaka 2006 hadi 2007
alikuwa akitumikia nafasi ya Mhariri wa Msaidizi wa Michezo gazeti la
Majira na baadaye 2006 hadi 2007 akawa Mhariri wa Michezo wa gazeti
hilo .
Mwaka 2006 hadi 2007 alipata cheti
cha elimu ya uandishi wa habari katika Chuo cha Ceylon (CSJ).
Amesafiri nchi mbalimbali duniani
katika kuripoti habari za michezo na burudani ikiwemo Afrika Kusini
mwaka 2003 hadi 2006 kwenye mashindano ya Big Brother Africa.
Pia mwaka 2007, 2008 na 2009 Kenya,
Senegal na Uingereza kuripoti habari za michgezo kupitia Super Sport.
Mei mwaka huu alisafiri kwenda
nchini Uturuki kwenye kongamano la wadau wa masuala ya mawasiliano
ambako alikuwa kiongozi wa wahariri waliotoka Tanzania na kutoa mada
iliyohusu mwenendo wa vyombo vya habari nchini Tanzania.
Nje ya kazi ya uandishi wa habari
mwaka 2008 na 2009 alifanya kazi katika kampuni ya matangazo ya ZK
akiwa Ofisa Habari na Uhusiano.
Miongoni mwa vyombo vya habari
ambavyo aliwahi kufanya kazi enzi za uhai wake ni pamoja na Kampuni ya
New Habari ambayo aliitumikia mwaka 2007 na 2008 akiwa Mhariri Msaidizi
wa gazeti la Bingwa.
Hatimaye mwaka 2008 alikuwa Mhariri
Mkuu wa gazeti la Bingwa kabla hajaacha kazi katika kampuni hiyo na
kujiunga na Kampuni ya ZK.
Alijiunga na gazeti la Jambo Leo
mwaka 2010 akiwa Mhariri wa Habari na kuanzia mwaka jana hadi mauti
ilipomkuta alikuwa Mhariri Mkuu wa gazeti la Jambo Leo.
Taarifa hii imetolewa na Meneja
Mkuu wa Kampuni ya Jambo Concepts Ltd,
Ramadhan Kibanike