Mhariri Mtendaji wa kampuni ya Free Media ambayo inachapisha
magazeti ya Tanzania Daima na Sayari, Absalom Kibanda akimpa pole
Mkurugenzi wa Jambo Concepts, Juma Pinto kufuatia kifo
cha Mhariri Mkuu wa gazeti la Jambo Leo, Willy Edward kilichotokea
mkoani Morogoro usiku wa kuamkia leo. (Picha zote na Mpiga Picha wa
Habari Mseto Blog).
Mkurugenzi wa Jambo Concepts, Juma Pinto
akilia kwa uchungu baada ya kuona gari lililokuwa limebeba mwili wa
aliyekuwa Mhariri Mkuu wa Jambo Leo marehemu Willy Edward likiingiza
mwili wa marehemu katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya
Taifa ya Muhimbili jijini Dar
Mhariri wa gazeti la
Tanzania Daima Jumapili, Salehe Mohamed (kushoto), Mhariri wa Habari
Mtanzania, Mwandishi wa Michezo Tanzania Daima, Ruhazi Ruhazi na Frank
Balile wa gazeti la Super Star
Baadhi ya Wahariri na waandishi waandamizi wakiushusha mwili wa
marehemu ili kuhifadhiwa katika hospitali ya Taifa muhimbili mara baada
ya kuwasili kutokea Morogoro.
Mwili wa marehemu ukiingizwa katika chumba cha kuhifadhia
maiti.
Baadhi ya wafanyakazi wenzake wakiwa muhimbili wakati mwili wa
marehemu ukihifadhiwa.
Baadhi ya waombolezaji wakiwa nyumbani kwa aliyekuwa Mhariri
Mkuu wa Jambo Leo marehemu Willy Edward Murahati jijini Dar es Salaam.
Wa tatu kushoto ni mke wa marehemu, Rehemaheri Willy Edward. (Picha zote
na Mpiga Picha wa Habari Mseto Blog).
Mtoto wa marehemu Willy Edward, Careen Willy Edward.
DAR ES SALAAM, Tanzania
Mhariri Mkuu wa gazeti la kila siku la
Jambo Leo Willy Edward, amefariki dunia usiku wa
kuamkia leo akiwa mjini Morogoro alikoenda kuhudhuria semina ya siku
moja iliyoandaliwa na ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na kuwashirikisha
wahariri wa vyombo mbali mbali vya habari.
Kwa mujibu wa Kulwa Karedia ambaye ni mhariri
wa gazeti la Mtanzania,alisema marehemu kabla ya kufikwa na umauti
alikuwa ni mzima wa afya na kwamba aliwaaga kuwa anaenda
kuwaona watoto wake wanaoishi mkoani humo ambapo alikaa huko
mpaka saa 6:30. Marehemu ameacha mke na watoto watatu.
Alisema muda
wa kurudi katika hoteli aliyofikia ulipowadia Marehemu alimwita dereva
wa Piki Piki ili amchukue na kwamba usafiri huo ulipofika hakuweza
kuipanda kwani alipotoka nje na kutembea kwa hatua kama sita kabla ya
kuifikia piki piki alianguka.
Karedia
aliongeza kuwa ndugu zake walimkimbiza hosipitali na baada ya vipimo vya
daktari ikabainika kuwa alikwisha fariki dunia.
Kaka wa
Marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Denis Ongiri, alisema wanatarajia
kumzika marehemu katika mji wa Mugumu Wilayani
Serengeti.
Alisema kwa
sasa Msiba upo nyumbani kwa kaka yake eneo la Mburahati NHC na kwamba
taarifa ya lini mwili utasafirishwa zitatolewa baada ya ndugu kukutana
na kutoa uamuzi wa pamoja.
“Suala hili limekuwa la ghafla sana ninachoweza kusema kwa
sasa ni kwamba tutaenda kumzika wilayani Serengeti katika mji wa
Mugumu,tunaomba ushirikiano wa watu wote katika hili kuanzia sasa mpka
safari nyake ya mwisho”alisema Ongiri kwa huzuni.
Marehemu Willy Edward (kulia) enzi za uhai wake akiwa na Rais
Jakaya Kikwete.
Na Edson
Kamukara
“WILLY twende zetu Dar, achana na Martin Malera, maana yeye
huku Morogoro ni kwao amefika, hawezi kuondoka leo”.
Sikujua kama
hayo ndiyo yalikuwa maneno yangu ya mwisho kwa kaka, rafiki na mwana
tasnia wa habari, Willy Edward, ambaye nilikuwa naye jana mjini Morogoro
kwenye semina ya siku moja kwa wahariri, iliyoandaliwa na Ofisi ya
Taifa ya Takwimu (NBS).
Nasema sikujua
kwa kuwa niliyasema kwa utani wakati tulipokuwa tukiagana na wenzangu,
ndipo nikamsogelea Willy akiwa amekaa meza moja na mhaririri wa Tanzania
Daima Jumatano, Martin Malera na James Range wa kituo cha televisheni
cha Startv, nikiwaaga na kuwauliza kama wanaondoka kurejea Dar es
Salaam.
Willy
alinijulisha kuwa anabaki na ataondoka kesho yake akimaanisha Jumapili
ya jana na wakati huo wote kwa pamoja na Malera walikuwa wakitutania
kuwa tunakimbilia wapi kwanini hatutaki kulala Morogoro?
Ndipo
nikamtania Willy nikisema twende, achana na Malera maana yeye ni
mwenyeji wa mkoani humo, hivyo amefika hawezi kuondoka…(tukacheka) na
kupeana mikono kisha tukaondoka na Range, Saleha Mohamedi (Mhariri wa
Tanzania Daima Jumapili) na David Ramadhan (Chanel ten) na hivyo
kumuacha Willy.
Kwa muda wote
tuliokuwa naye kwenye semina hiyo, alionekana mchangamfu na kwa bahati
nzuri tulikaa jirani na hivyo tulipata muda mrefu wa kuzungumza mambo
mengi.
Nilipatwa na
mshangao leo alfajiri baada ya kupokea simu ya Mhariri wangu Mtendaji,
Absalom Kibanda, akiniuliza kama nina
taarifa za kufariki kwa Willy Edward, kwa vile alidhani nami nililala
Morogoro.
Nilinyanyuka
ghafla kitandani, kwa ghafla nikakumbuka miongoni mwa wahariri
waliyobakia kule, alikuwemo pia Kulwa Karedia wa Mtanzania na hivyo
nikampigia simu kuhakikisha taarifa hiyo kama ni kweli.
Karedia baada
ya kupokea simu yangu, aliniambia kwa sauti ya kunyong’onyea akisema,
“Kamanda, Willy Edward hatunaye tena, nimejaribu kukupigia lakini simu
yako nimekuwa siipati”.
Nilijikaza
kumsikiliza Karedia huku nikibubujikwa na machozi, akanieleza kuwa Willy
alikwenda kuwaona watoto wake na alikuwa huko hadi saa sita usiku, na
kisha alimwita dereva wa pikipiki afike kumchukua kwa lengo la kurejea
katika hoteli alikokuwa amefikia.
Lakini baada ya
kutoka nje, kabla ya kupanda pikipiki alidai anasikia kizunguzungu na
kisha alianguka.Wenzake walijitahidi kumkimbiza hosipitali lakini
walipofika na kufanyiwa vipimo daktari aligundua tayari alikuwa
ameshafariki dunia.
Hivyo ndivyo
alivyozimika ghafla Willy Edward, ambaye mashabiki wa michezo
watamkumbuka daima kama mpenzi wa mpira wa miguu na zaidi shabiki wa
kutupwa wa Klabu ya Yanga kwa hapa nchini na Arsenal kwa timu za nje.
Pia Willy
alipenda sana muziki wa dansi, ule wa zamani na huu wa kisasa, akiwa
mshirika wa karibu wa bendi ya Twanga Pepeta, ambayo amefanya nayo kazi
pia kwa muda kadhaa.
Nilimfahu Willy
kwa ukaribu zaidi kuanzia 2009 tulipoanza kufanya kazi pamoja katika
gazeti la Jambo Leo, tukiwa waandishi waanzilishi wakati huo yeye akiwa
mhariri wa michezo.
Licha ya kwamba
amefanya kazi katika vyombo vya habari tofauti lakini kwa muda mrefu,
binafsi nilibahatika kufanya naye kazi katika gazeti la Jambo Leo na
hata baada ya kuhamia Tanzania Daima, tumeendelea kuwa karibu.
Kwa muda wote
wa miaka miwili na miezi mitatu niliyokaa naye Jambo Leo, nilimfahamu
kwa undani na kutambua kuwa alikuwa mpole, mtaratibu na mkimya,
aliyependa kusikiliza na kujifunza zaidi kabla ya kutenda au kuzungumza.
Willy alikuwa
mchangamfu, mwepesi wa kuelekeza na mwenye kupenda ushirikiano na watu
wengine. Alikaripia na kuonesha hasira pale ambapo ililazika kufanya
hivyo lakini haikuwa hulka yake.
Pamoja na
kubadilishwa nafasi kutoka mhariri wa michezo kuwa habari na kisha
Mhariri Mkuu wa Jambo Leo, Willy alibakia kuwa yule yule mwenye silika
ya upole na ushirikishaji wa wenzake asiyependa kujivuna.
Willy alipenda
kukuza lugha ya Kiswahili kupitia tasnia ya habari, na katika kufanya
hivyo kila mara alipenda kufanya kazi akiwa na kamusi ya Kiswahili
pembeni, akichukua baadhi ya maneno na kuyatumia kwenye gazeti mara kwa
mara kama misamiati mipya ambayo baadaye ilizoeleka.
Yako mengi ya
kuandika kumhusu Willy Edward, ambaye sasa ni marehemu lakini itoshe
kusema kuwa tumepoteza mtu muhimu katika tasnia ya habari na fani
nyingine kama michezo na muziki.
Mungu ametoa na
ametwaa, jina lake lihimidiwe. Tunamwomba ailaze pema peponi roho ya
mwenzetu Willy Edward Ogunde. Lakini kwangu itanichukua muda kumsahau
kaka yangu huyo.
NA HABARI MSETO BLOG