MAKETE
Serikali ya kijiji cha Iwawa wilayani Makete imewaasa wananchi wake wanaokwepa kuchangia michango mbalimbali ya maendeleo kijijini hapo kuwa, hawatapata huduma yeyote kutoka serikali ya kijiji hicho pindi watakapohitaji msaada kutoka kwenye serikali hiyo
Hayo yamezungumzwa na Afisa mtendaji wa kijiji cha Iwawa Bw. Esau Pagalo wakati akizungumza na wananchi waliofika ofisini kwake, na kusema kuna baadhi ya wananchi wanaokwepa kulipa michango ya maendeleo ikiwemo ya sekondari lakini wamekuwa wakifika ofisini kwake kutaka misaada ikiwemo kuchukua barua za dhamana mahakamani
Bw. Pagalo amesema kwa sasa hatatoa huduma kwa mwananchi yeyote ambaye hashiriki katika uchangiaji wa michango ya maendeleo na mtu huyo hatapata huduma mpaka atakapokuwa amechangia michango hiyo kutokana na wanachi hao ambao hawatoi michango wanakwamisha maendeleo kijijini hapo na taifa kwa ujumla
Katika hatua nyingine Bw. Pagalo amewataka wananchi wanaokwenda ofisini kwake wahakikishe wanapitia kwa viongozi wa vitongoji vyao kwanza ili kuwaepuka matapeli wanaokuja kuhitaji misaada katika ofisi yake ilihali si wakazi wa wilaya ya Makete
Na Timotheo Swalo na Obeth Ngajilo