Aliyekuwa mbunge wa Arusha mjini (CHADEMA) Godbless Lema
Mahakama kuu kanda ya Arusha imeamuru mbunge wa Arusha mjini kwa tiketi ya CHADEMA Mh. Godbless Lema, kuvuliwa ubunge wa jimbo hilo ikiwa ni hukumu ya kupinga ushindi wa ubunge alioupata katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010
Kesi hiyo ilifunguliwa na wanachama watatu wa chama cha Mapinduzi wakitaka mbunge Lema avuliwe madaraka kutokana na madai kwamba alitoa lugha za matusi, kashfa na udhalilishaji dhidi ya aliyekuwa mgombea wa chama hicho kwa tiketi ya CCM Dk. Batilda Buriani wakati wa kampeni za kuwania ubunge wa jimbo hilo mwaka 2010
Hukumu ya kesi hiyo imevuta hisia za watu wengi hasa wafuasi wa vyama vya CCM na CHADEMA na kuwa gumzo katika kona mbalimbali za jimbo la Arusha mjini
Kufuatia hukumu hiyo jimbo hilo la Arusha mjini lipo wazi hali itakayopelekea kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa kumpata mbunge huku chama cha CHADEMA kikisema hakina mpango wa kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo na badala yake kinasubiria uchaguzi mdogo wa jimbo hilo