Makete 04.04.2012
Warsha kuhusu mkakati wa kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa kutokana na kupunguza ukataji miti na uharibifu wa misitu(MKUHUMI) umefanyika katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Makete kwa lengo la kupunguza athari za mazingira wilayani humo
Akifungua warsha hiyo mkuu wa wilaya ya Makete Mh. Zainab Ahmad Kwikwega amesema utekelezaji wa mpango wa upunguzaji wa uzalishaji hewa ukaa kutokana na ukataji miti na uharibifu wa misitu (MKUHUMI) ni hatua mojawapo ya kukabiliana na hali hiyo, hivyo mpango huu umeanza kutekelezwa nchini kupitia taasisi mbalimbali kwa kushirikiana na jamii
Zipo taasisi tisa zinazoshughulikia miradi ya majaribio ya MKUHUMI hapa nchini ambapo shirika la Wildlife Conservation Society (WCS) ni moja kati ya taasisi hizo na inashughulikia mradi wa majaribio ya MKUHUMI nyanda za juu kusini ikiwemo wilaya ya Makete
Katika warsha hiyo wawezeshaji wa mafunzo kutoka programu ya uhifadhi wa mazingira nyanda za juu kusini inayoendeshwa na shirika hilo la Wildlife Conservation Society, wameelezea kuhusu umuhimu wa msitu wa kijiji wa Madihani, athari zilizopo pamoja na mapendekezo ya kupunguza athari hizo
Wawezeshaji hao wameelezea nia yao ya kutaka kuhifadhi msitu huo kwa kushirikiana na wananchi wanaozunguka eneo hilo , kutokana na msitu huo kuwa na nyani adimu duniani pamoja na nyoka wanaozaa
Katika hatua nyingine wawezeshaji hao wamewataka wananchi wanaozunguka msitu huo wa madihani kutowaua nyani wanaoharibu mazao yao kwani ni kosa kisheria na kuwa utafiti unaendelea kufanyika huko Rungwe mkoani Mbeya kuona namna ya kuwafukuza nyani na mwishoni mwa mwaka huu huenda majibu yakatolewa kwa wananchi
Akiahirisha warsha hiyo kwa niaba ya mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Makete, diwani wa kata ya Iniho Mh. Jison Mbalizi amewashukuru wawezeshaji hao pamoja na kuwataka washiriki kwa pamoja kushirikiana kuhakikisha mkakati wa kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa kutokana na kupunguza ukataji miti na uharibifu wa misitu (MKUHUMI) unatoweka