Mpenzi msomaji, leo tugeukie mahusiano ya vijana wetu. Hivi unajua vijana huanza kutafuta wachumba wakiwa wangali shuleni? Wapo wale ambao bado wako elimu ya msingi, wengine sekondari na hata vyuo elimu ya juu.
Kundi ambalo linaleta shida zaidi ni lile la shule za msingi na sekondari(miaka 7-15) kwani hujichanganya na kudhani kuwa wameshakomaa kuingia katika anga hizo za mahusiano ya kimapenzi. Ni kundi linalotambulika kama watoto.
Lakini pia wanashindwa kuelewa kuwa bado wanalo jukumu la kukazania masomo ili huko baadaye waweze kuwa wazazi wenye upeo na uelewa mkubwa wa stadi za maisha ikiwemo mikikimikiki ya ndoa , hivyo kutodanyanyika.
Je, umewahi kukumbana na purukshani za vijana wanaopeana ahadi za kuoana lakini zinaota mbawa kwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na wivu ninaoweza kuita wa rejareja? Hebu kwanza msomaji wangu sikia kisanga hiki hapa chini, kisha nawe uchangie maoni na ushauri tuweze kusonga mbele.
Yupo msomaji mzuri wa safu hii ambaye alinasa kituko kimoja akaona atumegee ili nasi tujadili kwa lengo la kupatia ufumbuzi purukshani hizi zinazowasonga vijana wetu. Msomaji huyu kupitia ujumbe kadhaa kupitia simu ya safu hii anasimulia hivi;-
“Jioni moja nikiwa nimekaa kibarazani katika ofisi ya rafiki yangu, mara akaja kijana mmoja ambaye namfahamu kwani mara nyingi huwa tunakutana .
Na sisi kama vijana huwa tunabadilishana mawazo kwa stori mbalimbali. Baada ya salamu akaniambia; “Afadhali kaka nimekukuta.
Nikamuuliza kulikoni akaanza kunieleza hivi; “Nina mchumba ambaye tupo kama marafiki ni zaidi ya miezi sita sasa. Mwanzoni nilishamwambia kuhusu nia yangu ya kutaka kumuoa. Bahati nzuri alinikubalia, lakini kwa masharti. Nikamuuliza masharti gani aliyokupa?
Akajibu; kwanza aliniambia yeye bado anasoma na kama nataka kumuoa nimgharimie sehemu ya masomo yake yaliyobakia.
Sharti la pili, nisifike nyumbani kwao labda kama wazazi wake hawapo nyumbani. Nilimuuliza binti huyo anasoma darasa gani, akajibu kidato cha pili, kisha akaendelea na stori.
“Wiki ya jana nilienda Mwanza kikazi bahati mbaya simu yangu ikapotea hivyo nikapoteza namba zangu zote, niliweza kuzikumbuka chache tu.
Nikachukua namba ya rafiki yangu ambaye huyo binti pia anamfahamu nikampigia kumjulisha kuhusu kupotea kwa simu yangu, pia nilimuomba anitafutie mchumba wangu ili niongee nae pia.
Bahati nzuri wakati huo huo naongea na huyo rafiki yangu, huyo binti naye akawa anapita. Jamaa yangu akamsimamisha ili nimpe ile simu.
Yule binti akakataa kupokea simu na kusema hamfahamu huyo jamaa anayeambiwa aongee nae.
Mwanza nilikuwa nakaa siku tano, jana nimerudi, leo nimeenda mitaani kwa mchumba wangu nikafanikiwa kumuona nikamuuliza kwanini ulikataa kupokea simu ili uongee nami.
Jibu nililopata ndilo linaloniumiza moyo. Yule msichana alijibu hivi; “Kuanzia sasa sahabu kuhusu mimi, tafuta mwingine na nikikukuta naye popote sikuulizi nami ukinikuta na mwingine popote usiniulize.
Nilipouliza sababu msichana akajibu eti baada ya yeye kukataa kupokea simu kuna jamaa ambao walikuwa pamoja na yule rafiki yangu walianza kumtukana na kumsema vibaya.
Basi huyu rafiki yangu akaendelea kusimulia; “Sikutaka kuamini nilichosikia lakini nilimuomba msamaha anisamehe. Alikataa kutoa msamaha na akaeda mbali zaidi na kusema,”ameachana na mpenzi wake kwa sababu yangu akiamini kwamba mimi ni mwelewa zaidi ya huyo aliyeachana naye na sasa anagundua kumbe na mimi ni muhuni nina marafiki wahuni.
Jamaa anasema hao jamaa waliomtukana huyo msichana walikuwa wapita njia yaani sisi marafiki zake. Hata hivyo, pamoja na kujitetea kadiri alivyoweza, msichana hakuwa tayari kumsamehe. Sasa anaomba ushauri kwangu afanyeje?
Mimi nilimshauri nikamwambia; Sikia mdogo wangu, dunia hii ina mambo mengi. Sasa kuna vitu vingi tunavyovifahamu na tusivyo vifahamu, vinavyoonekana na visivyoonekana. Kwa hiyo kwa kifupi wewe ungali bado kijana mdogo na huyo msichana bado ni mdogo.
Hivyo sioni sababu ya ninyi kuwa katika mapenzi na hasa ukizingatia yeye msichana bado mwanafunzi na wewe bado hujaanza kujitegemea, wote mnategemea wazazi. Ni bora ukafanya mchakato wa kujitegemea na baadaye ndio uingie katika mahusiano.
Kwa ufupi hiyo ndiyo stori na nafikiri vijana kama hawa wapo wengi.Kwa ujumla kupitia safu hii naomba tumshauri pia wapate elimu.
Source:Nipashe Jumapili