MCHUNGAJI AHAMISHWA KILAZIMA

UONGOZI wa Serikali ya Mtaa wa Ituha, kata ya Ilomba jijini Mbeya umemhamisha kwa lazima kimakazi Mchungaji wa Madhehebu ya Ufufuo kutokana na kutoa mahubiri yaliyoelezwa kuhatarisha uhusiano wa ndoa jamii.

Ofisa Mtendaji wa Mtaa huo, Pius Moses, akizungumza na 'Habarileo' wiki hii, alimtaja Mchungaji huyo kama John Leonard, ambaye amekuwa akitoa mafundisho ya kuzuia watu kwenda misibani, akidai madhehebu yake hayaamini katika kifo.

Lakini pia katika jambo la kushangaza, Mchungaji huyo amekuwa akihimiza waumini wake hususan wanandoa kuacha kufanya tendo la ndoa katikati ya wiki na badala yake wafanye hivyo Jumapili tu.

Alisema Mchungaji huyo pia amekuwa akikataza waumini wake kusalimiana kwa kushikana mikono kutokana na imani kwamba waumini wa madhehebu tofauti na ya kwake walikwishafariki dunia.

Mmoja wa waumini hao aliyejitambulisha kwa jina la Mama Pendo, amesema kwamba Mchungaji huyo alikuwa akiwashinikiza kutofanya tendo la ndoa katikati ya wiki kwa madai kuwa ni vema kufanya Jumapili tu kwani ndiyo siku Mungu alipopumzika baada ya kuumba Mbingu na Nchi na vyote vilivyomo.

"Sisi tunapenda mafundisho ya Mchungaji wetu, lakini hatujapendezwa na kauli zake za kutakataza kushirikiana tendo la ndoa na waume zetu, hadi Jumapili peke yake kwani hali hiyo inaweza kufanya waume zetu kutuacha na kutafuta wanawake wengine," alilalamika Mama Pendo.

Jitihada za kumpata Mchungaji huyo azungumzie tuhuma hizo zilishindikana kutokana na kuhamishia makazi yake kusikojulikana Februari mosi kabla siku waliyompangia kufanya hivyo kuwadia.

Mkoa wa Mbeya unaaminika kuwa na makanisa mengi yenye imani tofauti, zikiwamo zinazokataza waumini kuimba Wimbo wa Taifa.
Source:Habarileo newspaper


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo