Katibu
Mkuu wa Wizara ya mambo ya ndani ya nchi Mbaraka Abdualwakili,
akizindua chapisho la tathmini ya Polisi Jamii nchini, hafla hiyo
ilifanyika jana Makao Makuu ya Polisi Jijini Dar es Salaam. Picha Alexander Mpeka – Jeshi la Polisi
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya ndani ya nchi Bw. Mbaraka Abdualwakil, Mwakilirishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano Sayansi na Teknolojia ambaye
ni Mkurugenzi wa utawala na rasilimali watu, Bi Selina Lyimo wakiwa
Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Abdulrahaman Kaniki pamoja timu iliyoshiriki katika utafiti wa tathmini ya Polisi jamii. Picha na Alexander Mpeka – Jeshi la Polisi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya ndani ya nchi Bw. Mbaraka Abdualwakil, Mwakilirishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano Sayansi na Teknolojia ambaye
ni Mkurugenzi wa utawala na rasilimali watu, Bi Selina Lyimo wakiwa
Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Abdulrahaman Kaniki pamoja makamishina
wa Jeshi la Polisi wakati wa hafla ya makabidhiano ya chapisho la
utafiti wa tathmini ya Polisi jamii . Picha na Alexander Mpeka – Jeshi
la Polisi.
======= ======= =======
Na. Tamimu Adam - Jeshi la Polisi.
Jeshi la Polisi nchini limetakiwa kutumia matokeo ya utafiti wa tathmini ya Polisi Jamii uliofadhiliwa
na Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia kupitia Tume ya taifa
ya Sayansi na teknolojia( COSTECH) katika kuboresha mkakati wa Polisi
jamii ili kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao kwani matokeo
hayo yana manufaa makubwa katika kubaini, kuzuia, na kutanzua uhalifu
na kero mbalimbali katika jamii.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu Bi. Selina Lymo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na teknolojia wakati wa hafla ya kukabidhi chapisho la utafiti wa matokeo ya tathmini ya Polisi jamii nchini kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi Bw. Mbaraka Abdulwakili .
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya ndani ya nchi Bw. Mbaraka Abdulwakili
alisema atahakikisha utafiti huo unafanyiwa kazi ipasavyo na amewataka
watendaji wa Jeshi la Polisi kutumia utafiti huo katika kuimarisha
usalama wa raia na mali zao kwa kuwa askari waliopo hawatoshi na Polisi
jamii imeonyesha mafanikio makubwa katika kuzuia vitendo vya uhalifu na wahalifu.
Naye, Mtaalum Mwelekezi wa Utafiti wa Tathmini ya Polisi Jamii ambaye pia ndiye Mtafiti Mkuu Dkt Haji
Semboja alisema kuwa utafiti huo ulifanyika katika kanda saba ambapo
matokeo ya utafiti huo yanaonesha kuwa uhusiano wa kiutendaji baina ya
wananchi na Jeshi la Polisi umeboreshwa kwa kiwango kikubwa kupitia
dhana ya Polisi jamii.
Alisema kuwa jambo hilo linasaidia katika kutengeneza mazingira ya amani na hivyo shughuli nyingine za kiuchumi na kijamii zinaweza kuendelea kufanyika bila hofu na kwa uhakika wa ulinzi na usalama.
Aliongeza
kuwa, utafiti huo umeonyesha kwamba, watu wengi wanaamini kuwa, matokeo
ya kuanzishwa kwa Polisi jamii katika maeneo yao kuna
mafanikio makubwa katika kuhimiza na kutia moyo uvumbuzi wa njia mpya
za kukabiliana na vitendo vya uhalifu ambapo wananchi wamekuwa
wakihimizwa utoaji wa taarifa za uhalifu kupitia njia mbalimbali ikiwemo
njia ya ujumbe mfupi.
Naye, Naibu Inspekta Jenerali wa
Polisi, Abdulrahman Kaniki aliipongeza timu nzima iliyofanya utafiti
huo na kusema kuwa Jeshi la Polisi kama watekelezaji wakuu wa Programu
ya maboresho yaliyojikita katika mihimili mikuu mitatu ambayo ni Weledi, Usasa na Polisi jamii, wanatambua
na kuthamini kazi nzuri iliyofanywa na watafiti hao na amewaomba
kuangalia namna wanavyoweza kufanya utafiti katika mihimili mingine miwili iliyobaki ambayo ni Usasa na Weledi ili Jeshi Polisi liweze kuwa na tathimini halisi ya Maboresho yake.
Kwa
upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi
na Teknolojia (COSTECH) Dr. Flora Tibazarwa alisema kuwa madhumuni ya
mpango wa utafiti huo yalikuwa ni kuimarisha uhusiano baina ya Jeshi la Polisi na wananchi katika kuzuia na kutatua matatizo ya jamii, msisitizo ukiwa kuzuia uhalifu kabla haujatokea.
Aliongeza
kuwa matokeo ya utafiti huo yatawasaidia watunga sera na watoa maamuzi
kutoa maamuzi na kutunga sera mbalimbali za usalama wa raia na mali zao
kwa faida ya taifa letu.