
Watu wasiojulikana wamevunja na kuiba nyaraka mbalimbali za jeshi la
polisi mkoani Mwanza, huku kamanda wa polisi mkoani humo naibu kamishna
Ernest Mangu akihaidi kuwafukuza kazi baadhi ya askari polisi
watakaobainika kuhusika katika tukio hilo.
Kamanda Ernest Mangu amewaambia waandishi wa habari jijini Mwanza
kwamba watu hao ambao bado hawajafahamika majina yao, usiku wa kuamkia
leo wameingia kwenye ghala la kuhifadhia vielelezo na nyaraka la kituo
kikuu cha polisi wilaya ya Nyamagana baada ya kuvunja dirisha la ofisi
za ukaguzi kanda ya ziwa, na kupora kompyuta ndogo mbili za mkononi
ambazo zilikuwa ni vielelezo, nguo za vielelezo vya kesi na kitabu cha
kumbukumbu ya matukio na kisha kutokomea kusikojulikana.
Akizungumzia tukio hilo, mkaguzi wa shule kanda ya ziwa Bibi.
Florencia Vicent amesema kuwa wezi hao wamevunja madirisha mawili ya
ofisi hiyo, ingawa hadi wakati afisa huyo alipokuwa anatoa taarifa hizo
walikuwa bado hawajapata uhakika wa kipi kilichoibwa.
Katika hatua nyingine kamanda wa polisi mkoani Mwanza naibu
kamishna Ernest Mangu amesema jeshi la polisi mkoani humo limefanikiwa
kumkamata mtu anayetuhumiwa kuhusika katika mauaji ya vikongwe katika
wilaya za magu na kwamba, ambaye ametajwa kwa jina la Seni Kayende wa
wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu.